Jumla ya noti za Zamani 22 zaondolewa na kutotambulika tena kuanzia Leo

Jumla ya noti za Zamani 22 zaondolewa na kutotambulika tena kuanzia Leo

#1



Jumla ya noti za Zamani 22 zaondolewa na kutotambulika tena kuanzia Leo

Jumla ya noti za zamani 22 zitatolewa katika mizunguko na kutotambulika kama fedha halali za Tanzania ikiwa wamiliki wake hawatakamilisha mchakato wa kuzibadilisha leo.

Oktoba 26, 2024 Benki Kuu ya Tanzania (BoT) iliutaarifu umma juu ya matoleo ya fedha hizo yaliyotakiwa kubadilishwa kuanzia Januari 6, 2025 hadi leo Aprili 5 ambayo ni pamoja na ya mwaka 1985 hadi mwaka 2003 pamoja na baadhi ya mwaka 2010.

Noti hizo za zamani zitakazositishiwa matumizi ni za shilingi ishirini (20), mia mbili (200), mia tano (500), elfu moja (1,000), elfu mbili (2,000), elfu tano (5,000) na elfu kumi (10,000) kwa matoleo ya mwaka 1985 hadi mwaka 2003.

Nyingine ni noti ya shilingi mia tano (500) iliyotolewa mwaka 2010 zenye sifa zilizoainishwa kwenye Tangazo la Serikali Na. 858 la tarehe 11 Oktoba 2024.

Kufuatia tangazo hilo BoT imewatoa.hofu baadhi ya Watanzania wanaoshindwa kutofautisha noti za Sh5,000 na Sh 10,000 zinazotolewa kwenye mizunguko na zile ambazo bado zinatumika na kubainisha kuwa zitakazondolewa ni toleo la mwaka 2003.

“Noti za Shilingi 10,000 na 5,000 ambazo ni toleo la 2010 na marejeo yake zinaendelea kutumika na hivyo hazihusiki kwenye zoezi hili la ubadilishwaji linaloendelea…

…Noti hizo zina makundi ya sahihi za Waziri wa Fedha na Gavana wa Benki Kuu ambazo ni kati ya Mh. Saada Mkuya na Prof. Benno Ndulu, Mh. Mustafa Mkulo na Prof. Benno Ndulu, Dkt. Philip Mpango na Prof. Florens Luoga Pamoja na Dkt. Mwigulu Nchemba na Gavana Emmanuel Tutuba.,”imesema taarifa ya BoT iliyotolewa Aprili 4,2025.

Hii itakuwa mara ya tano kwa BoT kuondoa noti za zamani katika mzunguko wa sarafu. Mara ya kwanza zoezi hilo lilifanyika mwaka 1977 kwa noti ya Shilingi 100 iliyochapishwa kuanzia 1966 hadi 1977. Pia iliendesha zoezi hilo tena mwaka 1979 kwa kuondoa uhalali wa noti ya Shilingi 10 na Shilingi 20 zilizochapishwa kati ya mwaka 1966.

Mwaka 1980, BoT iliondoa katika mzunguko noti ya Shilingi 5 na Shilingi 20 zilizochapishwa kati ya 1966 hadi 1979.Zoezi la nne lilifanyika mwaka 1995 ambapo noti ya Shilingi 50 na Shilingi 100 zilizochapishwa kati ya mwaka 1979 hadi 1995 ziliondolewa katika mzunguko.


TOA MAONI YAKO HAPA(REPLY BELOW👇)


image quote pre code