Kampeni maalum ya kuchangia damu kupitia vyuo vya afya yaanza rasmi

Kampeni maalum ya kuchangia damu kupitia vyuo vya afya yaanza rasmi

#1

Kampeni maalum ya kuchangia damu kupitia vyuo vya afya yaanza rasmi



Kampeni maalum ya kuchangia damu kupitia vyuo vya afya vya kati na vyuo vikuu imezinduliwa jijini Dar es Salaam, ikiwa na lengo la kuongeza upatikanaji wa damu salama kwa wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo katika hospitali mbalimbali nchini.

Uzinduzi huo umefanyika katika Kata ya Bunju, Wilaya ya Kinondoni, ambapo wakazi wa maeneo ya Boko, Tegeta, na Bunju wamejitokeza kwa wingi kushiriki zoezi hilo sambamba na wanafunzi kutoka vyuo vya afya, na kufanikisha ukusanyaji wa zaidi ya chupa 200 za damu.

Wakizungumza wakati wa zoezi hilo, baadhi ya wachangiaji damu akiwemo Frederick Mbinga, mkazi wa Bunju, amesema amekuwa akichangia damu mara kwa mara kwa kuwa anatambua thamani ya damu katika kuokoa maisha ya watu.

 “Damu ni uhai, na si lazima umjue unayemchangia. Kama una afya njema, changia damu,” amesema Mbinga.

Naye Neema Gozibart, mwanafunzi wa chuo cha afya, alisema ameguswa na kampeni hiyo na kuamua kuchangia damu kama njia ya kuonesha mshikamano na kusaidia jamii. 

“Nimeamua kutoa mchango wangu kama sehemu ya wajibu wangu kwa jamii,” amesema.

Akitoa tathmini ya kampeni hiyo, Afisa Uhamasishaji wa Damu Salama kutoka Wizara ya Afya,Evelyn Dielly, amesema mwitikio wa wananchi na wanafunzi wa vyuo vya afya ni mkubwa na wa kuhamasisha.

 “Tumevuna zaidi ya chupa 200 za damu kwa siku moja, hii ni hatua kubwa na inadhihirisha uelewa unaongezeka kuhusu umuhimu wa damu salama,” amesema Dielly.

Kwa upande wake, Daktari wa Magonjwa ya Sikoseli kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS)Dk. Hilda Tutuba, amesema damu salama ni muhimu kwa matibabu ya wagonjwa wa kisikoseli ambao mara nyingi huhitaji kupatiwa damu kutokana na hali zao. 

“Uchangiaji wa damu ni nguzo muhimu katika tiba ya wagonjwa wa sikoseli na magonjwa mengine ya dharura,” amesisitiza Dk. Tutuba.

Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Keneth Woiso, aliipongeza Wizara ya Afya na vyuo shiriki kwa kuandaa kampeni hiyo na kusisitiza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha damu salama inapatikana wakati wote.

 “Huu ni mfano mzuri wa ushirikiano kati ya serikali, taasisi za elimu na jamii. Tunahitaji kuendeleza jitihada hizi kila mara,” amesema Woiso.

Kampeni hiyo imeonyesha kuwa kwa ushirikiano na elimu sahihi kwa umma, Tanzania inaweza kufanikisha upatikanaji wa damu salama kwa mahitaji yote ya kiafya, na kuokoa maisha ya maelfu ya watu wanaohitaji huduma hiyo muhimu.

WEWE UNA MAONI GANI JUU YA MADA HII,CHANGIA HAPA [REPLY BELOW👇]


image quote pre code