Kampeni ya chanjo dhidi ya polio kwa watoto yazinduliwa ukanda wa Ziwa Chad
Mawaziri wa afya kutoka Cameroon, Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, Niger, Nigeria na Chad wamekutana leo huko N'Djamena Chad kuzindua kampeni ya pamoja ya chanjo dhidi ya polio kwa watoto zaidi ya milioni 83 walio na umri wa chini ya umri wa miaka mitano katika Ukanda wa Ziwa Chad.
Hii ni hatua muhimu katika kukabiliana na kirusi cha polio cha aina ya pili kinachosambaa katika eneo hili. Imesema taarifa iliyotolewa leo na Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani WHO huko N'Djamena mji mkuu wa Chad.
Katika kipindi cha miezi 12 iliyopita, WHO inasema kirusi hiki kimegunduliwa katika mazingira ya maji taka na kwa watu waliopatwa nacho katika nchi za Cameroon, Niger, Nigeria na Chad, ambapo jumla ya visa 210 viliripotiwa, 140 kati ya hivyo vikisababisha ugonjwa wa kupooza.
Ingawa Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, haijaripoti kisa chochote, bado kuna hatari kubwa ya maambukizi kuvuka mipaka limeonya shirika la WHO.
Limeongeza kuwa Kampeni za chanjo kati ya Aprili 2024 na Januari 2025 zilifanikiwa kuwafikia watoto milioni 12. Ili kuongeza kinga, kampeni nyingine ya pamoja itafanyika kuanzia tarehe 24 hadi 28 Aprili 2025, ikilenga maeneo ya mipakani yenye hatari kubwa na usimamizi hafifu wa afya.
Wahudumu wa afya zaidi ya milioni moja kushiriki kampeni
Kwa mujibu wa WHO kampeni hii itaendeshwa na wahudumu wa afya wapatao milioni 1.1, wakiwemo watoa chanjo, watoa elimu ya afya na wasimamizi.
Mawaziri wa afya pia watafanya kikao cha ndani kujadili changamoto, takwimu za ugonjwa huo na ushirikiano wa kuvuka mipaka, kwa mujibu wa Mpango wa Kikanda wa Kutokomeza Polio Afrika 2024-2025.
Waziri wa Afya wa Chad, Mhe. Dkt. Abdelmadjid Abderahim amesema “Ukanda wa Ziwa Chad unasalia kuwa eneo muhimu katika mapambano yetu dhidi ya polio. Kwa kushirikiana kama kanda, tunaimarisha dhamira yetu ya kuutokomeza ugonjwa wa polio kabisa.”
Mashirika ya kimataifa kama WHO, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF, Wakfu wa Gates, Muungano wa chanjo duniani Gavi na Rotary International yanaunga mkono juhudi hizi, pamoja na jamii na viongozi wa maeneo husika. Mkutano huo unaambatana na Wiki ya Chanjo Afrika yenye kaulimbiu “Chanjo kwa wote inawezekana”.
WHO imesema mpango huu ni mfano wa mshikamano katika afya ya kimataifa ili kujenga mustakabali usio na polio kwa watoto wa Ukanda wa Ziwa Chad na zaidi.
Reply
image quote pre code