Kidato cha 4 wapewa muda wa mwezi kubadilisha Tahasusi
DODOMA; SERIKALI kupitia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imetoa mwezi kwa wanafunzi waliohitimu kidato cha nne mwaka 2024 wabadili tahasusi au kozi.
Muda uliotolewa umeanza Machi 31, na utakwisha Aprili 30, mwaka huu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais -Tamisemi, Mohamed Mchengerwa alisema wametoa fursa kwa wanafunzi kubadili machaguo ya tahasusi za kidato cha tano na vyuo vya kati na elimu ya ufundi kwenye mfumo wa kielektroniki wa uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga na kidato cha tano na vyuo.
“Hatua hii ni maandalizi ya awali ya uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga Kidato cha Tano na Vyuo vya Serikali kwa mwaka 2025,” alisema Mchengerwa alipozungumza na waandishi wa habari Dodoma jana.
Alisema serikali kupitia Ofisi ya Rais-Tamisemi imekamilisha utaratibu wa awali wa kuingiza kwenye kanzidata taarifa zilizo kwenye fomu za uchaguzi za wanafunzi kama zilivyojazwa na wanafunzi wakiwa shuleni.
“Baada ya wanafunzi kufanya marekebisho yao, kanzidata hiyo ndiyo itakayotumika kuwachagua na kuwapangia nafasi za Kidato cha Tano na Kozi mbalimbali katika Vyuo vya Kati na vya Elimu ya Ufundi kwa kuzingatia sifa za ufaulu na machaguo yao,” alisema Mchengerwa.
Aliongeza: “Ofisi ya Rais – TAMISEMI inatoa fursa kwa wahitimu wa elimu ya sekondari Kidato cha Nne, mwaka 2024 kubadili machaguo yao ili kutoa nafasi zaidi kwa mwanafunzi kusoma tahasusi au kozi itakayomwandaa kuwa na utaalamu stahiki katika maisha yake ya baadaye”.
Mchengerwa alisema hatua hiyo pia itatoa fursa zaidi ya wanafunzi kuongeza machaguo na kufanya machaguo mapya ya tahasusi na kozi.
“Napenda kuwasihi wazazi na walezi kushauriana kikamilifu na watoto wao na kupata ushauri wa kitaalamu na kabla ya kufanya machaguo sahihi ya tahasusi na kozi kulingana na ufaulu wao,” alisema.
Alihimiza wanafunzi, wazazi na walezi kushauriana kikamilifu ikiwa ni pamoja na kupata ushauri wa kitaalamu na kitaaluma kabla ya kufanya mabadiliko ya tahasusi au Kozi.
Mchengerwa alihimiza wahitimu kufanya marekebisho ya machaguo ya tahasusi na kozi kulingana na ufaulu wao kwa kuingia kwenye mfumo wa uchaguzi wa wanafunzi unaopatikana kupitia kiunganishi cha selform.tamisemi.go.tz.
Alisema mhitimu anapaswa kuandika jina lake la mwisho, mwaka wa kuzaliwa na alama za ufaulu alioupata kwenye somo atakaloulizwa na mfumo au swali lolote atakaloulizwa.
“Ni matumaini yangu kuwa wahitimu wote watatumia kwa ukamilifu fursa waliyopewa ya kubadilisha tahasusi na kozi kulingana na ufaulu waliopata. Pia wataweza kusoma tahasusi au kozi ambazo wamefaulu vizuri ama wana malengo nazo zaidi,” alisema Mchengerwa.
Alisema baada ya kukamilika kwa utaratibu huo na wanafunzi kupangiwa shule na vyuo, hakutakuwa na fursa ya wazazi na wanafunzi kubadili tahasusi na kozi zao.
“Ninawasisitiza wanafunzi, wazazi na walezi kutumia muda huo vyema ili kuepusha changamoto zinazoweza kujitokeza mara baada ya matokeo ya uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na Kidato cha Tano na Vyuo kutangazwa,” alisema Mchengerwa.
Aliongeza: “Baada ya matokeo ya kujiunga na Kidato cha Tano na Vyuo kutangazwa, Ofisi itashughulika na huduma ya kubadilisha tahasusi na kozi ni bure.”
TOA MAONI YAKO HAPA(REPLY BELOW👇)
image quote pre code