Man United dhidi ya Man City, Ni Siku ya Jumapili kila kitu kitajulikana
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER United itaingia uwanjani Jumapili kwenye kipute cha Manchester derby dhidi ya mahasimu wao Manchester City ikiwa na mpango wa kuzoa pointi zote sita kutoka kwa wapinzani wao hao msimu huu.
Makocha Ruben Amorim na Pep Guardiola wote wana kitu cha kufanya kutokana na timu zao kutokuwa na mambo matamu kwa msimu huu. Man City inatafuta pointi za kuingia kwenye Top Four, wakati Man United inataka kujitoa kimasomaso kutokana na kuwa na msimu mbaya.
Manchester derby hii inaonekana kuwa na umuhimu mkubwa kwa pande zote mbili. Na kwenye hilo, ndilo linaloibua maswali mengi kuhusu mpango wa makocha wa vikosi hivyo wakienda kuonyesha ubabe uwanjani Old Trafford, Jumapili.
Kwa nini Amorim anamchezesha Garnacho kushoto?
Huu ni mjadala mkubwa Man United. Alejandro Garnacho anawatibua mashabiki kwa sababu amekuwa akipata nafasi nzuri sana za kufunga na hafungi. Eneo analochezeshwa linaonekana kwenda sambamba kabisa na uwezo wake na amekuwa akisaidia pia kwenye ulinzi na wakati mwingine amekuwa akiingia kwenye kiungo kuongeza idadi ya watu. Mwanzoni alikuwa akiteseka kupata mpira, lakini sasa kocha Amorim anajua namna bora ya kupata huduma yake.
Garnacho anapata mipira ya kutosha kutoka pembeni, kama ambavyo amekuwa akipenda na hivyo kupata muda wa kukimbia na mpira kuelekea kwenye eneo la wapinzani, lakini shida yake kubwa anashindwa kutumia nafasi. Upande wa kushoto anaochezeshwa ndio hasa unamfanya aonyeshe kiwango bora kabisa ndani ya uwanja. Man United inahitaji mtu wa kukimbia na mpira kutoka kwenye eneo hilo na hicho ndicho kitu anachofanya Garnacho.
2. Je, Man United itaichapa Man City bila kumiliki mpira?
Kwenye mechi dhidi ya Nottingham Forest iliyomalizika kwa kichapo cha bao 1-0, Man United ilimiliki mpira karibu kwa asilimia 70. Kwenye mechi dhidi ya Man City iliyofanyika raundi ya kwanza, vijana hao wa Guardiola ilimiliki mpira sehemu kubwa ya mchezo na Man United ilikuwa safi tu kwa kucheza bila ya mpira muda mwingi uwanjani. Man United imekuwa ikipanga vizuri sana kwenye safu yake ya ulinzi, eneo ambalo ndilo wamekuwa wakianzisha mashambulizi ya kushtukiza. Shida ya Man United inapocheza na timu inayokabia chini kama Nottingham Forest - lakini kwenye mechi hii ya Man City hilo haliendi kuwa tatizo, kwa sababu wenyewe ndiyo watakaokuwa wamiliki wa mpira muda mwingi.
Man City inaweza kuwa kwenye muundo wa 2-3-5 au 3-2-5 inaposhambulia na mabeki wa Man United ni hodari kwenye kukaba mtu kwa mtu. Huku ikitumia mawinga wake na wing-back kuhamishia mipira haraka kwenda kwa wapinzani.
3. Je, Marmoush ataiweza Man United kumzidi Haaland?
Hili ni swali gumu. Itakuwa nafuu kiasi gani kwa Man United endapo wapinzani wao watamkosa Erling Haaland mchezajo? Lakini, hilo limetokea mara nyingi kwa Man City msimu huu, kucheza bila ya huduma ya Haaland.
Na katika mechi hizo, silaha yao kubwa kwenye kusumbua mabeki wa timu pinzani, ni uwepo wa Omar Marmoush. Kwenye mechi ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Leicester City, ambayo Haaland hakuwepo, Marmoush alisimama imara sambamba na Doku na Savinho kwenye ile safu ya washambuliaji watatu.
Ilipocheza na Newcastle mapema msimu huu, Marmoush alifunga hat-trick, wakati alipokuwa kweye fowadi sambamba na Haaland - lakini anapokwenda kukabiliana na Man United, mambo yanaweza kuwa magumu kwake kwa sababu wapinzani wana mabeki watatu wa kati.
Hivyo, Haaland angekuwapo uwanjani, Man United ikakaa chini zaidi, lakini kwa kuwa na mshambuliaji mmoja, Marmoush, hilo litawapa ahueni kubwa Man United, labda kama tu wachezaji watakaokuwa pembeni, Savinho, Doku au Grealish kuitanua safu ya ulinzi ya timu hiyo na kutoa nafasi kwa Marmoush kuleta madhara.
4. Utamu upo kati ni De Bruyne au Fernandes?
Kevin De Bruyne na Bruno Fernandes. Manahodha wawili, mafundi wawili wa boli. Bila shaka ufundi wote na utamu wa mechi utakwenda kuamriwa na wakali hao.
Vita kali kabisa itakwenda kuonyeshwa na wachezaji hao wawili. Kwa siku za karibuni, Fernandes amekuwa akitumika kwenye kiungo ya kati na kama Garnacho ataanzishwa kwenye upande wowote ule iwe kulia au kushoto, unamfanya Mreno huyo kuwa na nafasi ya kupanda mbele kushambulia kwenye nafasi. Kwa kiungo De Bruyne, matazamio makubwa ni kumwona akipangwa kwenye eneo la kulia, ambako atakuwa na kazi ya kupiga krosi kwenye boksi.
Kutokana na hilo na kwa sababu Fernandes atakuwa kiungo ya kati, moja ya kazi yake kubwa itakuwa kwenda kumdhibiti De Bruyne, jambo litakalofanya mechi kuwa tamu. Man City wataomba Fernandes asipewe majukumu ya kumdhibiti De Bruyne, awe huru kufanya mambo yake hilo litawafanya wawe na wakati mzuri.
Kinachowatisha Man City kuhusu Fernandes kwa sasa ni kutokana na kiwango bora kabisa anachocheza mkali huyo, anakabaa huku muda wote yupo kwenye eneo la kushambulia. Fernandes na De Bruyne ndiyo walioshikilia mechi hiyo.
5. Mechi nyingine wikiendi hii zipi?
Mchakamchaka wa Ligi Kuu England utaanzia Jumamosi na Everton ya David Moyes itakuwa nyumbani kukipiga na Arsenal ya Mikel Arteta. Arsenal itahitaji kushinda mechi hiyo ili kuchelewesha sherehe za ubingwa huko Liverpool.
Crystal Palace itakipiga na Brighton, wakati Ipswich Town itakuwa na kibarua kigumu mbele ya Wolves, huku West Ham ikiwa na kasheshe zito kwa Bournemouth na Aston Villa itaonyeshana ubabe na Nottingham Forest kwenye mbio za kusaka Top Four ili kukamatia tiketi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kwa Jumapili, ukiweka kando kipute cha Manchester derby, Brentford itakuwa nyumbani kucheza na Chelsea, wakati Fulham itakuwa na kazi nzito ya kuituliza Liverpool katika moja ya mechi kali kabisa, huku Tottenham Hotspur itakuwa nyumbani kucheza na Southampton katika mechi nyingine yenye kuvutia kutazama. Jumatatu kutakuw ana mechi moja tu, Leicester City itakuwa King Power kucheza na Newcastle United.
MAVITU YA BRUNO vs DE BRUYNE
-Mechi: Bruno 29, De Bruyne 20
-Nafasi: Bruno 72, De Bruyne 41
-Pasi: Bruno 1,619, De Bruyne 715
-Mabao: Bruno 8, De Bruyne 2
-Asisti: Bruno 9, De Bruyne 6
-Tackles: Bruno 68, De Bruyne 11
TOA MAONI YAKO HAPA(REPLY BELOW👇)
image quote pre code