Matatizo makubwa wanayokutana nayo wajawazito huko Goma, DRC

Matatizo makubwa wanayokutana nayo wajawazito huko Goma, DRC

#1

Matatizo makubwa wanayokutana nayo wajawazito huko Goma, DRC



Katika wilaya ya Kyeshero ya Goma, Chance Azina, mwanamke mjamzito anazungumza na Amani, mfanyakazi wa shirika la kijamii linayoungwa mkono na UNFPA katika kituo cha afya kilicho karibu.

Akiwa anatembea, kwenye kona iliyofuata alikutana na Amani, mfanyakazi wa kuelimisha jamii kutoka kituo cha afya cha Kyeshero Christian Centre for the Light. Amani alikuwa akizungumza na wapita njia ili kutoa elimu kuhusu huduma za afya ya uzazi zilizopo.

“Aliponiuliza kuhusu maumivu ya kichwa na miguu, nilihofia. Hivyo ndivyo nilivyokuwa nikihisi,” Bi. Azina ameiambia UNFPA.

Alienda haraka kupimwa, akipokea huduma ya bure kutoka kwa wakunga waliopatiwa mafunzo na msaada wa UNFPA.

“Alikuwa na maumivu makali ya kichwa na miguu, lakini hakuwa ameonana na mtoa huduma ya afya tangu mwanzo wa ujauzito wake,” ameeleza  Justine, mmoja wa wakunga kwenye kituo hiki akiongeza kuwa,  “tulifanya vipimo mara moja ili kuondoa uwezekano wa kifafa cha mimba.”

Baada ya kuondoka kambini amejisitiri kwa wenyeji

Huduma ya kabla ya kujifungua ilikuwa haiwezekani kupatikana katikati ya ghasia ambazo zimelazimisha mamia kwa maelfu ya watu mjini Goma, mashariki mwa DRC kukimbia kwa hofu.

Kijiji chake cha Kanihi, wilayani Masisi, kilishambuliwa mwezi Desemba mwaka 2024, na Bi. Azina pamoja na watoto wake wanne walitembea zaidi ya kilomita 90 hadi kufika kambi ya wakimbizi ya Bulengo mjini Goma.

Lakini walifukuzwa baada ya maeneo mengi yaliyokuwa yakiwahifadhi wakimbizi kufungwa na waasi wa M23 mwezi Februari, wakitaka raia warejee kwenye vijiji vyao.

Familia hiyo ilihamia katika kambi nyingine pamoja na maelfu ya watu wengine. Hatimaye, familia mwenyeji ilimruhusu yeye na watoto wake kuishi pamoja kwenye chumba chao kidogo huko Kyeshero. Na tangu mumewe atoweke miezi michache iliyopita, amekuwa akikabiliana na ujauzito wake peke yake.

Hali halisi inayowakumba maelfu ya wanawake

Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, huduma za afya ya uzazi zilikuwa haba hata kabla ya mzozo huu wa karibuni, na nchi hii ina viwango vya juu sana vya vifo vya akina mama wajawazito.

Sasa, huko Kivu Kaskazini na Kusini, hospitali tatu tu ndizo zinazofanya kazi, zote zikiwa zimelemewa na uhaba wa vifaa muhimu, wafanyakazi, umeme na mafuta ya magari ya wagonjwa. Hii ina maana kuwa wanawake wengi wanalazimika kujifungua nyumbani bila msaada wowote.

Wajawazito huchelewa kuanza huduma ya kliniki

Ripoti zinaonesha kuwa chini ya nusu ya wanawake wajawazito kabla ya kujifungua wanaweza kuhudhuria kliniki mara 4, idadi inayopendekezwa; na kati yao, wengi huenda kwa mara ya kwanza wakiwa tayari wamechelewa mno kuzuia matatizo. Wengi zaidi hawana elimu kuhusu dalili hatarishi kama vile uzito mdogo, upungufu wa damu, shinikizo la juu la damu, na maumivu makali ya kichwa – yote yakiwa ishara za matatizo ya afya yanayoweza kuhatarisha maisha.

Kabla ya kukutana na Amani, Bi. Azina hakujua kuwa maumivu aliyokuwa nayo yangeweza kuhatarisha maisha yake na ya mtoto wake.

“Wanawake wengi huhisi hawawezi tena kusaidiwa baada ya kutoka kambini,” ameeleza Dkt. Solange N. Ngane, anayefanya kazi na UNFPA huko Kivu Kaskazini. “Wafanyakazi wetu wa jamii wana jukumu muhimu la kutoa elimu na mwongozo kwa wanawake walioko hatarini zaidi.”

Wahudumu wa kijamii wanaofadhiliwa na UNFPA, hutoa elimu, na kuwaelekeza wanawake wajawazito kwenye vituo vya afya washirika kwa ajili ya huduma za kabla ya kujifungua, upangaji uzazi, na matibabu kwa waathiriwa wa ukatili wa kijinsia. Hii huwezesha waliotengwa kabisa kurejeshwa kwenye mfumo wa huduma za afya, hata nje ya kambi za wakimbizi.

Madhara ya kukatwa kwa usaidizi kutoka Marekani

Marekani imekuwa mfadhili muhimu kwa programu hizi, lakini kusitishwa kwa ufadhili hivi karibuni kutawaathiri watu takribani milioni 11 – zaidi ya milioni 3 huko Kivu Kaskazini pekee – huku washirika wakilazimika kupunguza shughuli katika moja ya migogoro isiyofadhiliwa vya kutosha duniani.

Kliniki tembezi za afya pia zimesitishwa katika maeneo kadhaa kutokana na hali ya usalama, na viwango vya juu kabisa vya njaa kali vilivyowahi kurekodiwa nchini vinamaanisha kuwa wanawake na wasichana – hasa wajawazito na akina mama wapya – wanakabiliwa na vitisho vikubwa zaidi kwa maisha yao. Via UN-Swahili

TOA MAONI YAKO HAPA(REPLY BELOW👇)


image quote pre code