Matumizi ya Dawa Za Asili,changamoto zake na Faida kwa Jamii
Baadhi ya tafiti kama zile zilizofanywa na Shirika la Afya Duniani, WHO, mwaka 2021 na 2022 na African Journals Online, AJOL, pamoja na WHO Afro Health Monitor ya mwaka 2021 zimezitaja changamoto za matumizi ya tiba za asili kama vile ukosefu wa uthibitisho wa kisayansi, uelewa mdogo wa jamii kuhusu usalama na ufanisi wake, ukosefu wa mifumo thabiti ya udhibiti, na changamoto za kisheria zinazokwamisha matumizi yake rasmi.
Serikali ya Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zimekuwa zikichukua hatua ili kudhibiti matumizi holela ya dawa za asili, ikiwa ni pamoja na kudhibiti ubora wa dawa hizo kupitia usajili wa waganga wa tiba hizo.
WHO: Tiba za asili zina mchango mkubwa katika huduma za afya
Mwaka 2022, WHO lilibainisha kuwa ni dhahiri tiba za asili zina mchango mkubwa katika huduma za afya, ikiwa ni sehemu muhimu ya urithi wa kitamaduni na njia za asili za kutibu magonjwa hususan katika maeneo ya vijijini ambapo huduma za kisasa ni nadra.
Ukosefu wa elimu rasmi kwa waganga wa tiba za asili, pamoja na uhaba wa tafiti za kina kuhusu madhara na mwingiliano wa dawa za asili na za hospitali, huathiri matumizi yake. Khalid Hussen, mganga wa tiba za asili na mwanachama wa Chama cha Waganga wa Tiba za Asili Tanzania, anasema mchango wa dawa za asili katika jamii ni pamoja na wananchi kuzitumia dawa hizo na wengi wamekuwa wakirudisha majibu mazuri na ndio maana kumekuwa na mwamko mzuri.
''Kama unavyoona hizi dawa zimejaa viungo vya mboga vya kawaida ambavyo tunavila siku zote kwa hiyo hata madhara yake ni madogo sana kwa mtu kupata madhara,'' alifafanua Khalid.
Mziray Mwita, Afisa kutoka Kitengo cha Tiba za Asili na Tiba Mbadala nchini Tanzania, anasema Serikali ya Tanzania imechuka hatua ili kudhibiti matumizi holela ya dawa asili, ikiwa ni pamoja na udhibiti wa ubora wa dawa hizo.
''Mara nyingi sisi tunatumia vyombo vya habari kwa ajili ya kuwafikia wananchi sehemu mbalimbali na kutoa elimu kwa hao waganga wa tiba za asili, hasa kuhusu viwango vya ubora wa hizo dawa, lakini pia tunashirikiana na taasisi mbalimbali katika tafiti kama Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu, NIMRI na tunashirikiana pia na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, MUHAS,'' alibainisha Mziray.
Pamoja na ukosefu wa uthibitisho wa kisayansi, uelewa wa jamii kuhusu usalama na ufanisi wake unachukuliwaje na wananchi? Baadhi ya watu ambao wameshawahi kutumia dawa za asili wameelezea jinsi dawa hizo zinavyowasaidia.
''Kwa kweli kwa mtazamo wangu mimi kweli dawa za asili zimenisaidia. Nilikuwa na changamoto sioni kama ni mbaya, kikubwa ni kufuata masharti unayopewa ni namna gani ya kutumia dawa hizo,'' alisisitiza Judith Anthon, kutoka Mwanza.
Dawa zawasaidia wenye kipato cha chini
Aidha, Lucas Mhago anasema kwa ufupi dawa hizo zinawasaidia wananchi wenye kipato cha chini, na hivyo anaomba wananchi wazipate kwa wingi.
Mziray anaongeza kusema kuwa moja ya athari ya dawa za asili katika mfumo mzima wa afya ni baadhi ya mimea ya dawa ina viambata vyenye sumu vinavyoweza kuathiri ini, figo, au mfumo wa fahamu.
Dawa zisitumiwe kiholela
Kulingana na afisa huyo kutoka Kitengo cha Tiba za Asili na Tiba Mbadala nchini Tanzania, kuna madhara makubwa sana endapo mtu atatumia dawa hizo kiholela bila kufuata utaratibu na bila kufahamu kama dawa hizo zimethibitishwa na wataalamu.
''Kwa kutumia dawa kiholela unaweza ukapata shinikizo la damu, lakini pia kuna kiharusi kwa sababu dawa inapokuwa imeingia katika mwili wa binadamu hasa hizi dawa za asili kuzokana na kwamba hazina vipimo maalum tofauti na hizi za kizungu unaandikiwa tumia kimoja asubuhi, mchana na jioni au kwa vidonge viwili,'' alisema Mziray.
Utafiti unaainisha kuwa dawa za asili zina nafasi muhimu katika mfumo wa afya, lakini zinahitaji kutumiwa kwa uangalifu na kwa mwongozo wa wataalamu wa afya.
TOA MAONI YAKO HAPA(REPLY BELOW👇)
image quote pre code