Nimefanyiwa upasuaji mara 100 na siachi' Nini Ushauri wako hapa
Abby Wu alikuwa na umri wa miaka 14 tu alipofanyiwa upasuaji wa urembo bandia kwa mara ya kwanza.
Baada ya kupata matibabu ya homoni, uzito wa mwili wa Abby uliongezeka kutoka kilo 42 hadi kilo 62 ndani ya miezi miwili.
Mwalimu wake wa michezo ya kuigiza aligundua mabadiliko hayo ya mwili.
Mwalimu wangu aliniambia, ''ulikuwa nyota lakini sasa umekuwa mnene kupita kiasi. Chagua moja uondoke kwa tasnia hii au upunguze kilo,'' anakumbuka alichoambiwa kipindi hicho akisubiri kufanya mtihani wake wa tamthilia.
Mama yake Abby aliingilia kati na kuamua kumpeleka kufanyiwa upasuaji wa kuondoa mafuta tumboni na miguuni.
Abby anavuta kumbukumbu jinsi mamake alivyompa motisha akisubiri kufanyiwa operesheni hiyo.
''Kuwa mkakamavu na uingie ufanyiwe. Ukitoka hapo utakuwa mrembo zaidi.''
Upasuaji huo ulimuacha na makovu. Abby alipatiwa dawa za kupunguza uchungu lakini alikuwa macho akifanyiwa operesheni hiyo.
''Ningeona kiasi cha mafuta kilichotolewa mwilini mwangu na damu iliyokuwa ikinivuja,'' anasema.
"Upasuaji ulifanya kazi. Nilijiamini na kuwa na furaha zaidi, siku baada ya siku. Nadhani mama yangu alifanya chaguo sahihi."
Sasa Abby ana umri wa miaka 35 na amefanyiwa upasuaji wa urembo mara mia moja ikimgharimu dola nusu milioni.
Anamiliki kliniki ya ulimbwende katikati mwa mji wa Beijing na amekuwa mtu tajika katika tasnia ya upasuaji wa plastiki nchini China.
Lakini upasuaji huo pia unaathari zake kwa mwili.
Akiwa amekaa mbele ya kioo anajipodoa ili kuficha makovu ya sindano za kupunguza unene usoni, utaratibu anaoufanya kila mwezi ili kuhakikisha uchanga usoni mwake nakuhakikisha hana ngozi zilizolegea baada ya upasuaji wa kupunguza taya uliondoa mifupa mingi.
Lakini anasisitiza kuwa hajutii upasuaji wa urembo aliyofanya kufikia sasa akiamini kuwa mamake hakukosea kumuanzisha katika ulimbwende huu.