Panya wa Tanzania aweka rekodi ya Dunia kwa kufichua mabomu Zaidi ya mia moja

Panya wa Tanzania aweka rekodi ya Dunia kwa kufichua mabomu Zaidi ya mia moja

#1

Panya wa Tanzania aweka rekodi ya Dunia kwa kufichua mabomu Zaidi ya mia moja



Panya mmoja wa kiume anayenusa mabomu ya ardhini nchini Cambodia ameweka rekodi mpya ya dunia, kwa kuwa panya wa kwanza kufichua zaidi ya mabomu mia moja ya kutegwa ardhini na mabaki mengine ya zana za kivita ambayo yanaweza kusababisha maafa.

Shirika la kutoa misaada ya kutegeua mabomu yaliyotegwa ardhini lililo na makao yake nchini Ubelgiji, la APOPO, linasema panya huyo kwa jina la Ronin, ni panya kutoka bara la Afrika, amekuwa akifanya kazi katika jimbo la Preah Vihear kaskazini mwa Cambodia kwa zaidi ya miaka mitatu na kugundua mabomu 109 na vifaa vingine hatari 15.

APOPO limesema katika taarifa yake kwamba Ronin mwenye umri wa miaka mitano, anaweza kuendelea na jukumu hilo la kugundua mabomu ya kutegwa ardhini kwa miaka mingine miwili.

"Mafanikio yake ya kipekee yamemfanya apate taji la Rekodi za Dunia za Guinness kwa kuwa panya aliyegundua mabomu mengi ya ardhini," imesema APOPO.

Ronin aliyezaliwa August 13, 2019, Morogoro nchini Tanzania ameipiku rekodi ya awali, iliyokuwa ikishikiliwa na panya Magawa ambaye naye pia alitokea Tanzania, ambaye aligundua mabomu 71 ya ardhini wakati wa utumishi wake wa miaka mitano kabla ya kustaafu mwaka 2021.

Magawa, alitunukiwa medali ya dhahabu kwa ushujaa kwa kugundua mabomu katika takribani mita za mraba 225,000 za ardhi, sawa na viwanja 42 vya mpira, alikufa mwaka 2022.

Taifa la Cambodia bado limejaa maelfu ya mabomu yaliyotegwa ardhini kufuatia miongo mitatu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyomalizika mwishoni mwa miaka ya tisini.

Nchini Tanzania shirika hilo la Apopo pia linatumia panya wa kunusa ili kutambua watu wanaougua ugonjwa wa kifua Kikuu.

Vifo kutokana na migodi na silaha zilizotegwa ardhini hutokea mara kwa mara Cambodia, na karibu vifo 20,000 vimetokea tangu 1979, na mara mbili ya idadi hiyo wamejeruhiwa.

Watoto wawili wa Cambodia waliuawa mwezi Februari wakati guruneti la tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo lililopuka karibu na makazi yao kaskazini magharibi mwa mkoa wa Siem Reap.

TOA MAONI YAKO HAPA(REPLY BELOW👇)


image quote pre code