TAFITI:Watu wazima Asilimia 77% wana tatizo la kuoza meno

TAFITI:Watu wazima Asilimia 77% wana tatizo la kuoza meno

#1

TAFITI:Watu wazima Asilimia 77% wana tatizo la kuoza meno



WIZARA ya Afya imesema asilimia 76.5 ya watu wazima kuanzia miaka 15 na kuendelea wana tatizo la kuoza meno wakati asilimia 31.1 ya watoto wameoza meno yao ya utotoni.

Hayo yameelezwa jana Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Tiba na Huduma za Kinywa na Meno, Wizara ya Afya, Dk Baraka Nzobo alipokuwa akizungumza katika ufunguzi wa maonesho ya afya ya kinywa na meno yanayotarajiwa kufanyika Mei 30 hadi 31, mwaka huu Dar es Salaam.

Alisema magonjwa ya kinywa na meno nchini ni kati ya magonjwa ambayo yanasumbua kwa kiwango kikubwa na kuwa pamoja na idadi hiyo ya tatizo la kuoza meno pia magonjwa ya fizi yanaikumba asilimia 67 ya watu wazima na asilimia 57 kwa watoto.

Alisema Watanzania wengi hawana elimu ya kutosha kuhusiana na namna sahihi ya kulinda afya ya kinywa na meno jambo linalosababisha kuwa na asilimia kubwa ya watu wanaopata matatizo mabalimbali ya kinywa na meno.

Alitolea mfano wa kitu ambacho watu wengi hawakifahamu ni pamoja na namna sahihi ya upigaji mswaki ambapo alisema wengi wao huswaki na kusukutua vinywa kwa kutumia maji jambo ambalo si sahihi na kuwa usahihi ni kutema povu la dawa ya meno bila kuosha kinywa kwa maji ili kuacha dawa ya meno kulinda kinywa.

“Ili kukinga meno yako kutoboka, piga mswaki asubuhi baada ya kunywa chai na usiku kabla ya kwenda kulala kwa kutumia dawa ya meno, ukimaliza kupiga mswaki tema povu la dawa kisha usukutue mdomo kwa nje, usisukutue ndani ya mdomo ili ile dawa iweze kuzunguka ndani ya kinywa chako kwa saa 12 kutoa ulinzi wa meno,” alisema Dk Nzobo.

Aliongeza kuwa matatizo ya meno yanaweza kutibiwa kwa njia mbalimbali kama vile kuziba meno kwa muda mfupi au mrefu, tiba ya mzizi wa jino, kuondoa kiini cha jino na kuondoa ncha ya mzizi wa jino.

“Ni baada ya njia hizi zote kushindikana ndipo kung’oa jino kunapaswa kuzingatiwa kama suluhisho la mwisho,” alisema.

Alisema maonesho hayo ya afya ya kinywa yatasaidia kutoa elimu kuhusu afya ya kinywa na meno kwa Watanzania, kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa kuwa na bima za afya ili kupata huduma bora za matibabu ya meno, pamoja na kuhamasisha uwekezaji katika vifaa tiba vya kisasa kwa matibabu ya kinywa na meno.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Maonesho ya Afya ya Kinywa na meno Tanzania, Dk Ambege Mwakatobe alisema maonesho hayo yatatoa nafasi ya kujifunza teknolojia mpya na kuimarisha ushirikiano wa wadau mbalimbali wa afya ya kinywa na meno.

“Maonesho haya ni fursa ya kuimarisha ushirikiano wa kimkakati, kuongeza uwekezaji na kuchochea ubunifu wa kiteknolojia ambao utaamua mustakabali wa sekta ya kinywa na meno nchini Tanzania,” alisema.

Aidha, maonesho hayo yanafanywa kwa ushirikiano na taasisi mbalimbali za serikali na sekta ya afya ikiwemo Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), Wizara ya Afya, Chama cha Madaktari wa Meno Tanzania (TDA) na kutarajiwa kuhudhuriwa na wadau wa sekta hiyo kutoka mataifa mbalimbali ndani na nje ya Bara la Afrika.

TOA MAONI YAKO HAPA(REPLY BELOW👇)


image quote pre code