Uchimbaji wa Mchanga wahatarisha maisha ya Watu

Uchimbaji wa Mchanga wahatarisha maisha ya Watu

#1

Uchimbaji wa Mchanga wahatarisha maisha ya Watu



TAKRIBAN nyumba 48 katika eneo la Tegeta Msufini, Dar es Salaam, ziko hatarini kubomoka kutokana na uchimbaji wa mchanga.

Mbali  ya hatari hiyo, uchimbaji huo unasababisha uchafuzi wa mazingira na ni chanzo cha umasikini kwa wakazi wa eneo hilo.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hii jana, baadhi ya wakazi wa eneo hilo walisema maisha yao yako hatarini hasa wakati huu wa mvua na kwamba shughuli hiyo inasababisha mmomonyoko wa ardhi.

Mkazi wa eneo hilo, Victoria Aume, alisema wakati wa mvua mwaka jana, nyumba yake ya vyumba sita ilibomoka na kubaki masikini, akiwa hana makazi wala fedha kidogo ya wapangaji aliyokuwa anaipata.

“Wakati nyumba hiyo inabomoka, nilikuwa ndani. Ilikuwa majira ya saa 1:00 usiku ndipo mjukuu wangu alisema kwa sauti bibi tutoke nje nyumba inabomoka. Nilipata mshtuko na nilipotoka nje ndipo nilipopatwa ugonjwa wa kiuno na mgongo. Tulikuwa tunakimbia, tunakimbizana na matofali yaliyokuwa yanadondoka.

 “Uchimbaji unaoendelea umeniletea umasikini, nimetoka kwenye nyumba yangu na sasa nimepanga na sina hata uwezo wa kulipa kodi. Naumwa kama unavyoniona na sijui hatima ya maisha yangu,.” Alisema. 

Mjumbe wa Shina Na. 11 katika eneo hilo, Modest Francis, alisema uchimbaji huo ulianza takribani miaka 10 iliyopita na kwamba jitihada za kuwazuia wachimbaji zimekwama.

Alisema kwa siku, malori ya mchanga kati ya matano hadi 10 yanaingia eneo hilo kubeba mchanga, hali inayotishia makazi ya wakazi wa Msufini.

“Kwa upande wangu zimeathirika nyumba 35, ikiwamo yangu mwenyewe. Tunaiomba serikali itusaidie kwa sababu hapa kuna wananchi wengi ambao hawana eneo mbadala,” alisema.

Alisema ili kuzuia mmomonyoko, wakazi wa eneo hilo wameamua kutupa taka kama njia ya kunusuru nyumba zilizosalia

“Tumejaribu kutupa taka lakini hazifui dafu, zaidi tunaona ni uchafuzi wa mazingira, hivyo tunaomba msaada kwa serikali yetu na mbunge wetu,” alisema.

Mjumbe wa Shina Na. 10, Edward Sungura, alisema uchimbaji huo unasababisha uharibifu wa mazingira na kuna hatari ya kuharibu pia miundombinu.

“Kwenye shina langu zimeathirika nyumba 13 pamoja na mimi mwenyewe kwani vyumba vinne vya wapangaji vimeanguka hivyo nipo hatarini kufukuzwa na adha hii na sijui nitaelekea wapi,” alisema.

Alisema vijana wanaoingiza malori ya kubeba mchanga katika eneo hilo, hawazuiliki kwa madai kuwa ni wakorofi na kila wakielezwa uharibifu wanaousababisha huishia kuwatukana wananchi.

Mkazi mwingine, Zainabu Barinyandi, alisema athari za uchimbaji huo zimevunja nyumba yake ya vyumba vinne na kulazimika kwenda kuhifadhiwa kwa rafiki yake tangu mwaka jana.

“Biashara yangu ni mihogo ya kukaanga ambayo faida yake ni ndogo sana. Kwa kweli hali yangu ni mbaya na sijui hatima ya maisha yangu,” alisema.

Reply


image quote pre code