Wazazi nchini Uganda wakubali chanjo ya Malaria kwa watoto

Wazazi nchini Uganda wakubali chanjo ya Malaria kwa watoto

#1

Wazazi nchini Uganda wakubali chanjo ya Malaria kwa watoto



Wazazi nchini Uganda wamekubali chanjo ya malaria kwa watoto wa chini ya umri wa miaka miwili, wakitarajia kuwa hatua hiyo itakuwa suluhu ya kudumu kufuatia shida na gharama za matibabu ya ugonjwa huo kwa watoto.

Afisa mkuu wa afya katika wilaya ya Apac Daktari James Odongo,  ameiambia DW kwamba ni vyema kuona zoezi hilo la kutoa chanjo limeanzia wilaya hiyo ambayo kwa muda mrefu imetambuliwa kuwa yenye kiwango cha juu cha visa vya wagonjwa wa malaria.

Mtu mmoja huumwa na mbu 1,500 kila mwaka

Daktari Odongo amesema kuwa katika wilaya hiyo, mtu mmoja huumwa na mbu 1,500 kila mwaka na asilimia 80 ya mbu hao wana vijidudu vya Malaria.

Wanawake wengi waliitikia mwito huo wa kuwapeleka watoto wao wenye miezi sita kupata chanjo hiyo. Kulingana na baadhi ya wazazi, licha ya kuwa na mashaka na chanjo hiyo mpya miongoni mwa chanjo zingine kwa watoto, wanasema ni afadhali kuliko madhila na gharama za kuwatibu watoto wao kila mara.

Ongezeko la aina mpya ya mbu sugu Afrika mashariki latishia vita dhidi ya Malaria

Hata hivyo, mmoja kati ya akina mama amelalamikia madhara yaliyomkumba mwanawe mara tu baada ya kupata chanjo hiyo. Mama huyo anasema , mwanawe alianza kutapika na kuendesha na akaingiwa na wasiwasi kama chanjo hiyo ilikuwa ni salama kwake.

Lakini Alfred Obote mhamasishaji wa kijiji kuhusu masuala ya afya maarufu kama VHT amesema hali hiyo hutokea ikiwa mtoto alikuwa anaugua malaria wakati alipopata chanjo.

Obote anasema hajasikia kisa chochote kuhusu madhara hayo lakini mama huyo amethibitisha kwamba mtoto huanzia kwenye hatua ya kwanza ya kupimwa kubaini ikiwa damu ina vijidudu vya Malaria.

Akina mama wajawazito ndio waathirika wakubwa wa Malaria

Akina mama wajawazito pia wametajwa kuwa waathirika wakubwa wa malaria katika wilaya hiyo. Wanakosolewa kwa kutokwenda kupata ushauri wakati wa ujauzito ili kupata kinga itakayowasaidia wao na watoto walio tumboni.

Daktari Odongo anaelezea kuwa tatizo kubwa la kuwatibu akina mama hao ni kwamba wanahitaji kuongezwa damu mwilini na mara nyingi vituo vya damu havina damu ya kutosha na iliyo stahiki kulingana na muhitaji, hali inayosababisha baadhi kufariki.

Reply


image quote pre code