Ukimwi
Dunia iko Hatarini Kushuhudia Kuongezeka kwa Maambukizi ya VVU kutokana na Kupungua kwa Ufadhili – UNAIDS
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na UKIMWI (UNAIDS) limeonya kuwa dunia inaweza kushuhudia ongezeko jipya la maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU) baada ya ufadhili wa kimataifa wa programu za mapambano dhidi ya ugonjwa huo kupungua kwa kiwango kikubwa.
Katika ripoti iliyotolewa wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa UKIMWI uliofanyika nchini Brazil, UNAIDS imesema ufadhili wa kimataifa ulipungua kwa karibu asilimia 20 mwaka uliopita na kufikia takriban dola bilioni 7 za Marekani, kiwango cha chini zaidi kuwahi kushuhudiwa katika karibu miongo miwili.
Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS, Winifred Byanyima , amesema hali hiyo inahatarisha mafanikio yaliyopatikana kwa miongo kadhaa katika kudhibiti maambukizi ya VVU. Amesema dunia ina ushahidi wa kisayansi unaoonyesha kuwa UKIMWI unaweza kutokomezwa, lakini kupungua kwa misaada kunazidisha pengo la upatikanaji wa huduma na kuhatarisha haki za binadamu.
Byanyima alisisitiza kuwa changamoto kubwa kwa sasa si ukosefu wa sayansi au tiba, bali ni maamuzi ya kisiasa kuhusu uwekezaji katika huduma za afya. Alieleza kuwa swali la msingi si kama dunia inaweza kumaliza UKIMWI, bali kama viongozi wataamua kuendelea kuwekeza katika mapambano hayo.
Ripoti hiyo pia inaangazia kuwa Marekani ilikuwa ikitoa karibu robo tatu ya ufadhili wa kimataifa wa programu za VVU kupitia misaada ya kimataifa kabla ya mabadiliko ya sera yaliyofuatia kurejea kwa Rais Donald Trump madarakani mwezi Januari 2025. Kupungua kwa michango hiyo kumeathiri nchi nyingi zinazotegemea misaada kwa ajili ya upatikanaji wa dawa za kufubaza VVU, huduma za kinga, vipimo na ufuatiliaji wa wagonjwa.
UNAIDS imeonya kuwa bila hatua za haraka za kuziba pengo la ufadhili, dunia inaweza kushuhudia kuongezeka kwa maambukizi mapya, vifo vinavyohusiana na UKIMWI na kudorora kwa mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mingi ya mapambano dhidi ya ugonjwa huo.


