magonjwa
Maambukizi ya Utumbo Yanayoweza Kusababisha Damu Kwenye Haja Kubwa
Kuona damu kwenye haja kubwa si jambo la kawaida. Ingawa wakati mwingine inaweza kusababishwa na bawasiri, maambukizi ya utumbo pia yanaweza kusababisha hali hii. Damu inaweza kuwa nyekundu angavu au yenye rangi ya kahawia hadi nyeusi, kulingana na sehemu inayovuja damu kwenye mfumo wa mmeng’enyo wa chakula.
Soma Sababu Zaidi za Kuona damu kwenye haja kubwa.

1. Kuharisha damu kutokana na bakteria
Baadhi ya bakteria wanaweza kuharibu ukuta wa utumbo na kusababisha vidonda vinavyotoa damu. Bakteria hawa ni pamoja na:
- Shigella
- Campylobacter
- Salmonella
- Baadhi ya aina za Escherichia coli (E. coli)
Dalili:
- Kuharisha mara kwa mara, wakati mwingine kukiwa na damu kwenye choo chako
- Maumivu makali ya tumbo
- Homa
- Kichefuchefu na kutapika
2. Amebiasis
Ugonjwa wa Amiba au Amoeba Husababishwa na kimelea kiitwacho Entamoeba histolytica. Kimelea hiki hushambulia ukuta wa utumbo na kusababisha vidonda vinavyoweza kutoa damu.
Dalili:
- Kuharisha choo chenye damu au ute au Vitu kama Makamasi
- Maumivu ya tumbo
- Homa wakati mwingine
- Kupungua uzito ikiwa maambukizi yatadumu muda mrefu
3. Clostridioides difficile (C. difficile)
Maambukizi haya yanaweza kutokea baada ya kutumia antibiotiki kwa muda, ambapo bakteria hawa huzaliana kupita kiasi na kusababisha kuvimba kwa utumbo.
Dalili:
- Kuharisha sana
- Maumivu ya tumbo
- Homa
- Wakati mwingine damu kwenye haja kubwa
4. Maambukizi mengine ya vimelea
Baadhi ya maambukizi ya minyoo au vimelea wengine yanaweza kusababisha kutokwa na damu ikiwa yataharibu ukuta wa utumbo, ingawa hali hii si ya kawaida.
Unapaswa kufanya nini?
- Kunywa maji ya kutosha ili kuzuia upungufu wa maji mwilini.
- Epuka kutumia dawa za kuzuia kuhara bila ushauri wa daktari, hasa kama kuna damu kwenye haja kubwa.
- Nenda hospitali haraka kwa uchunguzi wa kinyesi na vipimo vingine ili kubaini chanzo halisi na kupata matibabu sahihi.
- Au Wasiliana na afyaclass kupitia namba +255758286584.
Wasiliana na Wataalam wa afya au wahi hospital mara moja ikiwa:
- Damu ni nyingi au inaendelea kutoka.
- Una homa kali.
- Unahisi kizunguzungu au kuzimia.
- Una maumivu makali ya tumbo.
- Dalili zinaendelea zaidi ya siku 2–3 au unapata upungufu wa maji mwilini.
Reference:
- Mayo Clinic – Dysentery (kuhara damu) https://www.mayoclinic.org/diseases-conditions/dysentery/symptoms-causes/syc-20371295
- MSD Manual Professional – Infectious Colitis https://www.msdmanuals.com/professional/gastrointestinal-disorders/gastroenteritis/infectious-colitis
- Merck Manual Consumer – Gastroenteritis https://www.merckmanuals.com/home/digestive-disorders/gastroenteritis/overview-of-gastroenteritis
- Centers for Disease Control and Prevention (CDC) – Shigella (Shigellosis) https://www.cdc.gov/shigella/index.html
- CDC – Campylobacter Infection https://www.cdc.gov/campylobacter/index.html
- CDC – Salmonella https://www.cdc.gov/salmonella/index.html
- CDC – Amebiasis (Entamoeba histolytica) https://www.cdc.gov/parasites/amebiasis/index.html
- World Health Organization (WHO) – Diarrhoeal Disease Fact Sheet https://www.who.int/news-room/fact-sheets/detail/diarrhoeal-disease


