Saratani
Saratani ya Matiti kwa Wanaume
Ingawa saratani ya matiti huonekana zaidi kwa wanawake, wanaume pia wanaweza kuugua ugonjwa huu. Kwa mujibu wa wataalamu, wanaume wote wana kiasi kidogo cha tishu za matiti, hivyo seli zake zinaweza kubadilika na kuwa za saratani.
Kutokana na uelewa mdogo, wanaume wengi hufika hospitalini wakiwa katika hatua za mwisho za ugonjwa, jambo linalopunguza nafasi ya matibabu kufanikiwa. Hata hivyo, ugonjwa huu ukigunduliwa mapema unaweza kutibiwa kwa mafanikio.
Saratani ya matiti kwa wanaume ni nini?
Ni ugonjwa unaotokea pale seli za matiti zinapoanza kukua bila mpangilio na kutengeneza uvimbe wenye uwezo wa kusambaa sehemu nyingine za mwili kama mifupa, mapafu, ini au ubongo.
Kwa wanaume, saratani nyingi huanzia kwenye mirija ya maziwa (ducts), hali inayojulikana kama Invasive Ductal Carcinoma (IDC).
Takwimu zinaonyesha nini?
- Saratani ya matiti kwa wanaume huchangia chini ya asilimia 1 ya saratani zote za matiti duniani.
- Marekani hukadiriwa kugundua zaidi ya wagonjwa 2,700–3,000 wa kiume kila mwaka.
- Mamia ya wanaume hufariki kila mwaka kutokana na ugonjwa huu.
- Umri wa kawaida wa kugundulika ni kati ya miaka 60 hadi 70, ingawa inaweza kutokea kwa vijana pia.
Kwa mujibu wa WHO, idadi ya wagonjwa wa saratani ya matiti duniani imeendelea kuongezeka, na wanaume pia ni sehemu ya wagonjwa hao ingawa ni wachache.
Dalili za saratani ya matiti kwa wanaume
Dalili zinaweza kujumuisha:
- Kinyama au uvimbe mgumu kwenye titi.
- Chuchu kuingia ndani ghafla.
- Kutokwa na damu au majimaji kwenye chuchu.
- Ngozi ya titi kuwa na mikunjo au kufanana na ganda la chungwa.
- Chuchu kuwa na vidonda visivyopona.
- Maumivu kwenye titi (ingawa wakati mwingine hakuna maumivu).
- Kuvimba kwa tezi za kwapani.
- Titi kubadilika ukubwa au umbo.
- Ngozi kuwa nyekundu au kuvimba.
- Kupungua uzito bila sababu katika hatua za mwisho.
Sababu na vihatarishi
Hakuna sababu moja ya moja kwa moja, lakini hatari huongezeka kutokana na:
1. Umri mkubwa
Hatari huongezeka zaidi baada ya miaka 60.
2. Historia ya familia
Ikiwa baba, mama, dada au kaka aliwahi kupata saratani ya matiti, hatari huongezeka.
3. Mabadiliko ya vinasaba
Kurithi mabadiliko kwenye jeni kama BRCA2 au BRCA1 huongeza hatari.
4. Homoni nyingi za estrogen
Hali zinazoongeza estrogen kwa mwanaume zinaweza kuongeza hatari.
5. Ugonjwa wa Klinefelter Syndrome
Hali ya kurithi inayoweza kuongeza hatari ya saratani ya matiti.
6. Magonjwa ya ini
Ini likishindwa kufanya kazi vizuri, usawa wa homoni unaweza kubadilika.
7. Unene uliopitiliza
Mafuta mengi mwilini huongeza uzalishaji wa estrogen.
8. Matumizi ya mionzi kwenye kifua
Aliyewahi kupata tiba ya mionzi kwenye kifua anaweza kuwa na hatari kubwa zaidi.
Saratani hugunduliwaje?
Daktari anaweza kufanya:
- Uchunguzi wa matiti.
- Mammogram.
- Ultrasound.
- MRI kwa baadhi ya wagonjwa.
- Biopsy (kuchukua kipande cha uvimbe kwa uchunguzi).
- CT Scan au PET Scan ikiwa inahitajika kuona kama imesambaa.
Matibabu
Matibabu hutegemea sana na hatua ya ugonjwa. Lakini kwa ujumla matibabu huweza kuhusisha Dawa,Upasuaji,Mionzi, n.k..
Uzoefu wa madaktari
Madaktari wa saratani kutoka taasisi mbalimbali, ikiwemo MD Anderson Cancer Center na Mayo Clinic, wamekuwa wakisisitiza kuwa wanaume wengi huchelewa kufika hospitalini kwa sababu hawaamini kuwa wanaweza kupata saratani ya matiti.
Kwa mujibu wa wataalamu hao, mwanaume yeyote anayegundua uvimbe usio wa kawaida kwenye titi anapaswa kufanyiwa uchunguzi mapema badala ya kusubiri maumivu.
Hadithi za wagonjwa
Richard Roundtree
Muigizaji maarufu wa Marekani Richard Roundtree aligundulika kuwa na saratani ya matiti kwa mwanaume mwaka 1993 baada ya kuhisi uvimbe kwenye titi. Alifanyiwa upasuaji na matibabu mengine, akaendelea kuishi kwa miongo kadhaa huku akitumia hadithi yake kuhamasisha wanaume kutoficha dalili.
Mathew Knowles
Mathew Knowles, baba wa mwanamuziki Beyoncé, alitangaza mwaka 2019 kuwa alipata saratani ya matiti kwa mwanaume. Alieleza kuwa aliona tone la damu kwenye shati karibu na chuchu, jambo lililompeleka hospitalini na kugundulika mapema. Baada ya matibabu, amekuwa akihamasisha wanaume kujichunguza na kufanya vipimo wanapoona dalili.
Je, saratani hii inaweza kuzuilika?
Hakuna njia ya kuizuia kwa asilimia 100, lakini unaweza kupunguza hatari kwa:
- Kudhibiti uzito.
- Kufanya mazoezi mara kwa mara.
- Kupunguza matumizi ya pombe.
- Kutibu magonjwa ya ini mapema.
- Kufahamu historia ya familia.
- Kufika hospitalini mapema ukiona uvimbe au mabadiliko yoyote kwenye titi.
References:
- World Health Organization (WHO). Breast Cancer. https://www.who.int/news-room/fact-sheets/detail/breast-cancer
- . Breast Cancer in Men. https://www.cancer.org/cancer/types/breast-cancer-in-men.html
- . Male Breast Cancer Treatment (PDQ®). https://www.cancer.gov/types/breast/patient/male-breast-treatment-pdq
- . Male Breast Cancer. https://www.mayoclinic.org/diseases-conditions/male-breast-cancer
- . Male Breast Cancer. https://www.mdanderson.org/cancer-types/breast-cancer/male-breast-cancer.html
- . Breast Cancer in Men. https://www.cdc.gov/breast-cancer/about/men.html
- – Hadithi ya uzoefu wake: https://www.cnn.com/2019/10/02/health/mathew-knowles-breast-cancer-survivor
- – Uzoefu wake: https://www.cancer.org/latest-news/richard-roundtree-male-breast-cancer-awareness.html


