Patient Stories
Alikaa siku 42 bila fahamu(Coma) baada ya kuumwa na Kupe
Mwanamke alikaa kwenye koma kwa siku 42 baada ya kuumwa na kupe akiwa likizo Ugiriki
Mwanamke mmoja kutoka Anglesey, Wales, amesema maisha yake yamebadilika kabisa baada ya kuumwa na kupe wakati wa likizo nchini Ugiriki, hali iliyomfanya akae kwenye hali ya kukosa Fahamu(Coma) kwa siku 42 na baadaye kubaki na matatizo ya kupoteza kumbukumbu pamoja na kifafa.
Victoria Stellas, mwenye umri wa miaka 51, alisema alianza kupata dalili zinazofanana na mafua alipokuwa kwenye kisiwa cha Syros mwaka 2019. Aliporejea nyumbani Wales alianza kupata kifafa kinachotokea usiku, lakini madaktari hawakufahamu mara moja chanzo cha tatizo lake.
Baada ya kufanyiwa vipimo vya MRI, alihamishiwa kwa helikopta katika Hospitali ya Walton Centre nchini Uingereza, ambako aliwekwa kwenye hali ya kupoteza fahamu(koma) kitabibu kwa siku 42 ili kudhibiti hali yake.
Hatimaye aligundulika kuwa na tick-borne encephalitis (TBE), ugonjwa wa virusi unaosababisha kuvimba kwa ubongo na ambao unaweza kuhatarisha maisha.
Victoria alisema ugonjwa huo umeathiri maisha yake kwa kiwango kikubwa.
“Maisha yangu yamebadilika kabisa. Sipendi kutoka nje kama zamani, na nimepoteza kazi zangu,” alisema.
Anaamini aliambukizwa baada ya kuumwa na kupe alipokuwa nyumbani kwa shemeji yake nchini Ugiriki, ambaye hufuga mbuzi wanaoweza kuvutia kupe.
Alisema alikaa hospitalini na kupokea matibabu kwa takriban miezi sita.
Kutokana na matatizo ya Kupoteza kumbukumbu, alishindwa kuendelea na kazi zake kama mhudumu wa baa na msaidizi wa kufundisha watoto wenye mahitaji maalumu.
“Niambie kazi gani haihitaji kumbukumbu? Kila kitu maishani kinahitaji kumbukumbu—kununua, kufanya kazi na hata kusafiri,” alisema.
Aliongeza kuwa aliporudi kazini hakuweza tena kukumbuka majina ya wanafunzi na wafanyakazi, ingawa aliweza kuwatambua kwa sura.
Kwa mujibu wa NHS, TBE ni maambukizi ya virusi yanayoenezwa na kuumwa na kupe wanaopatikana katika sehemu mbalimbali za Ulaya, Urusi na maeneo ya China pamoja na Japan.
Baada ya kuumwa, dalili za awali zinaweza kujitokeza ndani ya wiki moja na kujumuisha uchovu, maumivu ya kichwa na dalili zinazofanana na mafua. Kwa baadhi ya wagonjwa, maambukizi yanaweza kuenea kwenye ubongo na kusababisha kifafa, kuchanganyikiwa, matatizo ya kuzungumza au kupooza sehemu ya mwili.
NHS inapendekeza watu wanaosafiri kwenda maeneo yenye hatari kubwa ya maambukizi wapate chanjo ya TBE angalau mwezi mmoja kabla ya safari.
Victoria, ambaye alizaliwa Ugiriki kabla ya kuhamia Wales akiwa na miaka mitano, alisema hakuwahi kujua kuwa chanjo hiyo ipo.
Sasa hutumia kati ya vidonge 15 hadi 18 kila siku ili kudhibiti dalili zake, huku kifafa chake cha usiku kikipungua ukilinganisha na awali. Pia hulazimika kulala pamoja na mama yake kwa usalama.
Anasema msaada wa familia na marafiki wake umekuwa muhimu katika maisha yake baada ya ugonjwa huo.
Mama yake, Liz Stellas, alisema watu wengi hudharau kuumwa na wadudu.
“Lazima watu wafahamu kuwa vitu vinavyoonekana havina madhara vinaweza kubadilisha maisha yako kabisa. Watu wengi hawatambui hilo.”
Mamlaka ya Afya ya Umma ya Wales (PHW) imewashauri watu wanaotembelea maeneo yenye kupe kuvaa nguo ndefu, kutumia dawa za kufukuza wadudu zenye DEET, kukaa kwenye njia rasmi wakati wa matembezi na kukagua mwili, nguo na wanyama wa kufugwa baada ya kutoka maeneo yenye nyasi au misitu. Kupe wanapaswa kuondolewa haraka kwa kutumia kifaa maalumu au kibano chenye ncha nyembamba.
Profesa Benedict Michael wa Chuo Kikuu cha Liverpool alisema idadi ya visa vya TBE imeongezeka duniani katika kipindi cha miaka 30 iliyopita, ingawa visa vingi vinapatikana Ulaya na Asia Mashariki na ni vichache sana nchini Uingereza.
Alieleza kuwa takriban asilimia 97 ya watu wanaoambukizwa hupata dalili hafifu au zinazofanana na mafua pekee, huku karibu asilimia 3 wakipata maambukizi makubwa ya ubongo.
Alisisitiza kuwa kwa sasa hakuna dawa maalumu za kuua virusi vya TBE, hivyo matibabu hulenga kudhibiti kifafa na kulinda mgonjwa dhidi ya madhara mengine. Aidha, alikumbusha kuwa ugonjwa huo unaweza kuzuilika kwa kupata chanjo kabla ya kusafiri kwenye maeneo yenye hatari.
Chanzo:
- BBC News: https://www.bbc.com/news/articles/c8rng7dkzpro
- NHS – Tick-borne encephalitis: https://www.nhs.uk/conditions/tick-borne-encephalitis/
