Afya News
Kenya yaimarisha huduma za afya ya akili kwa wanawake na watoto
Kenya imeendelea kuimarisha huduma za afya ya akili kwa kuzijumuisha katika sera na mipango yake ya afya, hatua inayolenga kuboresha ustawi wa wanawake, watoto na familia kwa ujumla. Serikali imeweka afya ya akili ya mama kuwa sehemu muhimu ya huduma za afya kupitia Sera ya Afya ya Akili ya Kenya 2015–2030 pamoja na Mpango wa Uwekezaji wa RMNCAH-N, unaolenga kuboresha afya ya uzazi, mama, mtoto mchanga, watoto, vijana na lishe.
Katika kuimarisha utekelezaji wa sera hizo, Wizara ya Afya ya Kenya kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini Kenya imewapa mafunzo wataalamu 37 wa afya kutoka kaunti tisa kuwa wakufunzi wa wakufunzi kuhusu Mwongozo wa WHO wa mhGAP. Mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha wahudumu wa afya wa mstari wa mbele kutambua mapema, kutathmini na kushughulikia matatizo ya afya ya akili katika vituo vya afya.
Kaimu Mwakilishi wa WHO nchini Kenya, Dkt. Neema Rusibamayila Kimambo, amesema afya ya akili ya mama ni msingi muhimu wa familia zenye afya na jamii zinazostawi. Amesisitiza kuwa Kenya inaonyesha uongozi kwa kuitambua afya ya akili ya mama kama sehemu ya huduma bora za afya ya mama na mtoto, huku WHO ikiendelea kuunga mkono juhudi hizo za mageuzi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Afya ya Akili katika Wizara ya Afya ya Kenya, Dkt. Mercy Karanja, amesema mustakabali wa huduma za afya ya akili unategemea kuzijumuisha katika huduma zote za afya. Ameeleza kuwa kila mwananchi anapowasiliana na mfumo wa afya, kuanzia kipindi cha ujauzito hadi ukuaji wa mtoto mdogo, ni fursa muhimu ya kutambua changamoto za afya ya akili, kutoa msaada na kuhakikisha huduma zinazohitajika zinapatikana kwa wakati.
Licha ya hatua hizo, changamoto bado zinaendelea kujitokeza. Washiriki wa mafunzo wameeleza kuwa wanawake wengi wajawazito na akina mama, hasa vijana na wale wanaokabiliwa na changamoto za kijamii na kiuchumi, bado hukosa huduma na msaada wa afya ya akili. Aidha, athari za mabadiliko ya tabianchi zimeongeza msongo wa mawazo katika jamii za wafugaji, huku unyanyapaa na imani za kitamaduni zikiendelea kuwafanya baadhi ya watu kuchelewa kutafuta matibabu.
Ili kupanua huduma hizo, wataalamu 37 waliopata mafunzo wanatarajiwa kuwafundisha wahudumu wengine wa afya katika kaunti zao. Hatua hiyo inalenga kuongeza uwezo wa vituo vya afya kutoa huduma za afya ya akili kwa wanawake, watoto na familia katika ngazi ya jamii.
Afisa wa Kiufundi wa WHO anayeshughulikia Afya ya Watoto na Vijana nchini Kenya, Dkt. Makeba Shiroya, amesema huduma za afya ya akili hazipaswi kupatikana katika vituo maalumu pekee. Amefafanua kuwa kupitia Mwongozo wa WHO wa mhGAP, wahudumu wa afya wa mstari wa mbele wanawezeshwa kutoa huduma za msingi za afya ya akili na kuwaunganisha wagonjwa na huduma za kibingwa pale inapohitajika, hatua inayosaidia kusogeza huduma karibu zaidi na familia na jamii.
Kupitia juhudi hizi, Kenya inalenga kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya ya akili katika jamii, kuboresha ustawi wa akina mama na kuhakikisha watoto wanapata mwanzo bora wa maisha.
Reference:
