Connect with us

magonjwa

Tatizo la Kiuno kuuma ni DALILI ya nini? Fahamu yote hapa

Doctor Ombeni

Published

on

379 Views
0 Comments

Kiuno kuuma(Waist Pain) ni DALILI ya nini? Fahamu yote hapa

Tatizo la Kiuno Kuuma au Waist pain,huhusisha maumivu yanayoweza kutokea katika sehemu ya chini ya mgongo, kuanzia chini ya mbavu kuelekea juu ya makalio na kuzunguka eneo hilo. Kwa watu wengine maumivu haya huwa katikati ya Sehemu ya chini ya mgongo(Lower back pain), wengine upande mmoja, na wakati mwingine huenea hadi kwenye makalio au miguuni.

Ni muhimu kutambua kwamba maumivu ya kiuno si ugonjwa moja kwa moja, bali ni dalili inayoweza kusababishwa na matatizo ya misuli, mishipa ya fahamu, diski za uti wa mgongo, viungo vya mgongo au, wakati mwingine, matatizo ya figo na viungo vya uzazi.

Takwimu za Tatizo hili

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), mwaka 2020 takribani watu milioni 619 duniani waliishi na tatizo la maumivu ya sehemu ya chini ya mgongo. Na WHO inatarajia idadi hiyo kufikia takribani milioni 843 ifikapo mwaka 2050.

Sababu za Waist Pain au Maumivu ya Kiuno

1.Sababu inayowapata watu wengi ni maumivu yasiyo maalumu ya sehemu ya chini ya mgongo (non-specific low back pain). Hapa daktari anaweza asipate ugonjwa mmoja maalumu wa kusema ndiyo chanzo, kwa sababu maumivu yanaweza kuhusisha misuli, mishipa, viungo na namna mwili unavyofanya kazi kwa ujumla. Guy’s and St Thomas’ NHS Foundation Trust inaeleza kwamba zaidi ya watu 80 kati ya 100 hupata low back pain wakati fulani katika maisha yao.

Maumivu haya yanaweza kuanza baada ya:

  • kubeba mzigo mzito,
  • kuinama muda mrefu,
  • kukaa muda mrefu,
  • kufanya kazi kwa muda mrefu,
  • kugeuka ghafla,
  • kufanya mazoezi makali au kukaa katika mkao mmoja kwa muda mrefu.

Misuli au mishipa inayozunguka eneo hili la Kiuno inaweza kuvutika na kusababisha maumivu. Cambridge University Hospitals inaeleza kuwa msongo unaorudiwa kwenye eneo fulani la mgongo, harakati za ghafla au kurudia harakati fulani kunaweza kuchangia maumivu.

2.Sababu nyingine ni diski za mgongo kuvimba au kuchanika (herniated disc). Diski zipo kati ya mifupa ya uti wa mgongo na husaidia kupunguza hali ya mshtuko. Sehemu ya ndani ya diski inapojitokeza na kugusa au kubana mshipa wa fahamu kwenye eneo hili, mtu anaweza kupata maumivu ya kiuno pamoja na maumivu yanayoshuka kwenye mguu.

Hali hii inaweza kusababisha sciatica. Mgonjwa anaweza kueleza kwamba maumivu yanaanzia kiunoni au kwenye makalio na kushuka nyuma ya paja hadi kwenye mguu au hata kwenye nyayo. Anaweza pia kupata ganzi, Kuhisi hali ya kuchomachoma kama sindano au Miguu kukosa nguvu. NHS inaeleza kuwa sciatica kwa kawaida huathiri upande mmoja na hutokana na mshipa wa fahamu kuguswa au kubanwa.

Hata hivyo, si kila mtu mwenye maumivu ya kiuno ana sciatica. Guy’s and St Thomas’ NHS Foundation Trust inaonyesha kwamba takribani mtu 1 kati ya 20 wenye low back pain hupata sciatica.

3.Umri pia unaweza kuwa sababu. Kadiri mtu anavyozeeka, viungo vya mgongo vinaweza kupata mabadiliko yanayohusiana na uchakavu (degenerative changes), ambayo yanaweza kuambatana na maumivu na kukakamaa. Katika baadhi ya watu, nafasi ambazo mishipa ya fahamu hupita inaweza kuwa nyembamba na kusababisha maumivu ya Kiuno.

4.Tatizo la Uzito mkubwa, kutofanya mazoezi, kukaa muda mrefu, au kukaa vibaya vinaweza pia kuchangia au kuongeza hali ya maumivu ya Kiuno. Hii haimaanishi kwamba maumivu yote yanatokana na “kukaa vibaya”; mara nyingi huwa ni mchanganyiko wa mambo mbalimbali ya mwili, maisha na mazingira.

5.Wakati mwingine kile ambacho mgonjwa anakiita “kiuno kuuma” kinaweza kuwa tatizo ambalo halianzii kwenye mgongo au Kiuno chenyewe bali ikiwa matatizo kwenye maeneo mengine kama vile kwenye;

  • Figo
  • Tumbo
  • Njia ya Mkojo n.k

Kwa mfano, Tatizo la mawe kwenye figo au maambukizi ya njia ya mkojo yanaweza kusababisha maumivu upande wa nyuma ya mwili au Maumivu ya Kiuno. Ikiwa maumivu yanaambatana na homa, maumivu wakati wa kukojoa, damu kwenye mkojo, kukojoa mara kwa mara au kichefuchefu, ni muhimu kuchunguzwa.

6.Kwa wanawake, maumivu ya sehemu ya chini ya mgongo au Maumivu ya Kiuno yanaweza wakati mwingine kuhusishwa na matatizo ya mfumo wa uzazi, hasa kama yanaambatana na maumivu ya tumbo chini ya kitovu, hedhi nyingi au zisizo za kawaida, maumivu wakati wa tendo la ndoa au kutokwa damu kusiko kawaida.

Kwahiyo,Mwanamke anaweza kupata Maumivu ya Kiuno kwa Sababu tu ya Hedhi, au matatizo mengine kwenye mfumo wake wa uzazi.

7. Sababu nyingine ni Mtu kupata ajali au kuanguka na kuumia kwenye Eneo hili la Kiuno, Hii huweza kusababisha Maumivu ya Kiuno.

Hospitalini, daktari haangalii tu sehemu inayouma. Anaweza kuuliza maumivu yalianza lini, kama yalitokea baada ya kuumia, kama yanashuka mguuni, kama kuna ganzi au udhaifu wowote, na kama kuna matatizo ya mkojo au choo. Uchunguzi wa mwili unaweza kusaidia kuamua kama mgonjwa anahitaji vipimo zaidi kama X-ray au MRI. Si kila mtu mwenye maumivu ya kiuno anahitaji MRI au X-ray.

Wagonjwa huielezaje hali hii ya Maumivu ya Kiuno au Waist Pain?

Mgonjwa mwenye maumivu ya kawaida anaweza kusema, “Kiuno kinauma nikikaa muda mrefu,” au “Nikiinama au nikibeba kitu kizito maumivu yanaongezeka.” Mwingine anaweza kusema, “Maumivu yanaanzia kiunoni na kushuka mpaka mguuni.” Maelezo haya ni muhimu kwa daktari kwa sababu yanaweza kusaidia kutofautisha maumivu ya misuli na maumivu yanayohusisha mshipa wa fahamu.

Kwa ujumla, hali nyingi za low back pain huboreka ndani ya muda wa wiki kadhaa. Cambridge University Hospitals inaeleza kuwa maumivu mengi yanayohusiana na msongo kwenye sehemu za mgongo huanza kupungua ndani ya takribani wiki 2–6.

Katika hali nyingi, mgonjwa hahitaji kulazwa hospitalini. Anaweza kusaidiwa kwa kuendelea kufanya shughuli zinazowezekana, mazoezi yanayofaa, physiotherapy na dawa za maumivu kulingana na ushauri wa mtaalamu. NHS inashauri watu wenye back pain waendelee kuwa active kadiri wanavyoweza badala ya kukaa kitandani kwa muda mrefu.

Wakati Waist Pain Inapokuwa Hatari na Inahitaji Hospitali

Ingawa maumivu mengi ya kiuno si hatari, kuna hali chache ambazo zinahitaji uchunguzi wa haraka. Guy’s and St Thomas’ NHS Foundation Trust inaeleza kuwa chini ya mtu 1 kati ya 100 wenye low back pain huwa na tatizo kubwa la mgongo linalohitaji huduma ya haraka.

Nenda hospitali haraka ikiwa maumivu ya kiuno yanaambatana na ganzi sehemu za siri au kuzunguka njia ya haja kubwa, kushindwa kukojoa, kushindwa kudhibiti mkojo au choo, udhaifu au ganzi kwenye miguu yote miwili, au mabadiliko mapya katika uwezo wa tendo la ndoa. Dalili hizi zinaweza kuashiria kubanwa kwa mishipa muhimu ya chini ya uti wa mgongo na zinahitaji tathmini ya dharura.

Pia ni muhimu kumuona daktari ikiwa maumivu yalianza baada ya ajali au kuanguka, yanaongezeka haraka, yanaambatana na homa au kujisikia mgonjwa sana, unapungua uzito bila sababu, au maumivu yanakuwa makali zaidi usiku.

Kwa mtu ambaye hana dalili hizo, lakini maumivu yanaendelea kwa wiki kadhaa, yanarudia mara kwa mara au yanamzuia kufanya kazi za kawaida, ni vizuri kwenda hospitali kwa uchunguzi. Anaweza kupewa rufaa kwa daktari wa mifupa, daktari wa mishipa ya fahamu au physiotherapist, kulingana na chanzo kinachoshukiwa.

Kwa hiyo, Waist Pain si lazima iwe ugonjwa wa figo wala tatizo la uti wa mgongo. Kwa watu wengi ni maumivu yasiyo maalumu yanayohusisha misuli, viungo na mifumo mbalimbali ya mgongo, na hupona bila upasuaji. Lakini maumivu yanayoshuka mguuni, yanayoambatana na ganzi au udhaifu, au yanayokuja pamoja na matatizo ya mkojo/choo yanahitaji uchunguzi wa kitaalamu.

Je,Una changamoto hii? Kwa Ushauri Zaidi na Tiba tuwasiliane +255758286584.

References:

  • World Health Organization (WHO): WHO guideline for non-surgical management of chronic primary low back pain — WHO – Low Back Pain Guidelines
  • NHS: Back pain — NHS – Back Pain
  • NHS: Sciatica — NHS – Sciatica
  • Guy’s and St Thomas’ NHS Foundation Trust: Low back pain — Guy’s and St Thomas’ NHS – Low Back Pain
  • Cambridge University Hospitals: Back Pain — Cambridge University Hospitals – Back Pain
  • NELFT NHS Foundation Trust: Back Pain — NELFT NHS – Back Pain
379 Views
0 Comments

Medical Disclaimer

Medical Disclaimer: Taarifa kwenye makala hii ni kwa ajili ya Updates au elimu ya jumla tu na haichukui nafasi ya uchunguzi,Tiba au ushauri wa kitaalamu wa daktari kwa mtu mmoja mmoja. Kama una dharura au tatizo lolote la kiafya, tafadhali Wasiliana na Daktari moja kwa moja hapa.

Je, unahitaji ushauri binafsi au matibabu ya tatizo lolote?

💬 Wasiliana na Daktari Hapa

🏆Certified| Doctor from Afyaclass. Maudhui haya ni kwa ajili ya elimu ya jumla ya afya. Unapohitaji ushauri wa kina, uchunguzi, au matibabu binafsi, wasiliana na daktari kupitia namba:+255758286584.Pia tufwatilie kupitia: @Facebook | @Instagram | @YouTube.

LATEST POSTS

magonjwa1 year ago

Ugonjwa wa genital warts,Chanzo,Dalili na Tiba

🩺Medically reviewed by Afyaclass Teams,MD's, Written by Doctor Ombeni Ugonjwa wa genital warts,Chanzo,Dalili na Tiba Genital warts ni ugonjwa gani,Soma...

magonjwa2 years ago

Vipele Sehemu Ya Siri,Vipele Ukeni, Vipele Kwenye Uume

🩺Medically reviewed by Afyaclass Teams,MD's, Written by Doctor Ombeni VIPELE SEHEMU YA SIRI,VIPELE UKENI, VIPELE KWENYE UUME Vipele kwenye Uume:...

magonjwa ya wanawake5 years ago

PID NI NINI? Na Dalili zake ni Zipi?(magonjwa ya Wanawake)

🩺Medically reviewed by Afyaclass Teams,MD's, Written by Doctor Ombeni  PID • • • • • PID NI NINI? Na Dalili...

afyatips1 day ago

Dalili za kidonda cha operation kupona

🩺Medically reviewed by Afyaclass Teams,MD's, Written by Doctor Ombeni DALILI ZA KIDONDA CHA OPERATION KUPONA Baada ya kufanyiwa operation, mwili...

Utafiti1 day ago

Desogestrel yahusishwa na Kuongezeka kwa Hatari ya uvimbe wa ubongo

🩺Medically reviewed by Afyaclass Teams,MD's, Written by Doctor Ombeni Mamlaka ya Dawa na Bidhaa za Afya ya Ufaransa (ANSM) imewaonya...

magonjwa5 years ago

UGONJWA WA BRUCELLA(chanzo,dalili na tiba)

🩺Medically reviewed by Afyaclass Teams,MD's, Written by Doctor Ombeni UGONJWA WA BRUCELLA(chanzo,dalili na tiba) Huu ni ugonjwa ambao kwa kitaalam...

magonjwa ya watoto2 years ago

Ugonjwa wa Surua kwa Watoto: Sababu, Dalili, Matibabu na Kinga

🩺Medically reviewed by Afyaclass Teams,MD's, Written by Doctor Ombeni Ugonjwa wa Surua kwa Watoto: Sababu, Dalili, Matibabu na Kinga Ugonjwa...

Afya News2 days ago

Vifo vya Watoto Wachanga Katika Mlipuko wa Surua Pennsylvania na Mjadala wa Afya ya Umma

🩺Medically reviewed by Afyaclass Teams,MD's, Written by Doctor Ombeni Mlipuko wa ugonjwa wa surua (measles) unaoendelea katika jimbo la Pennsylvania,...

Afya News2 days ago

Wauguzi Kenya Wasitisha Mgomo Baada ya Makubaliano na Serikali

🩺Medically reviewed by Afyaclass Teams,MD's, Written by Doctor Ombeni Wauguzi nchini Kenya wamesitisha mgomo wao wa siku 43 baada ya...

WHO3 days ago

Uvutaji Sigara Unaongeza Uwezekano wa Ugumba

🩺Medically reviewed by Afyaclass Teams,MD's, Written by Doctor Ombeni Uvutaji Sigara Unaongeza Uwezekano wa Ugumba Shirika la Afya Duniani (WHO)...

380
0