Afya News
Mbinu za kutokomeza udumavu Njombe,Daktari aeleza
Mbinu za kutokomeza udumavu Njombe,Daktari aeleza
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Dk. Juma Mfanga, amewataka watoa huduma za afya kuhakikisha wajawazito wanapata huduma bora za lishe ili kupunguza tatizo la udumavu kwa watoto. Amesema huduma hizo zinapaswa kujumuisha elimu ya lishe, ushauri, upimaji wa hali ya lishe, utoaji wa dawa kinga pamoja na virutubishi muhimu kwa afya ya mama na mtoto.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya wakufunzi wa Mradi wa Kuboresha Huduma za Lishe kwa Mama Mjamzito (IMAN II), Dk. Mfanga alisisitiza umuhimu wa kuwapatia wajawazito virutubishi vya madini na vitamini kwa usahihi, huku matumizi yake yakifuatiliwa ili kuhakikisha yanaleta matokeo yaliyokusudiwa.
Pia aliagiza Timu za Afya za Halmashauri kuendelea kuwajengea uwezo watoa huduma kupitia usimamizi na kutumia takwimu kufuatilia utekelezaji wa huduma za lishe na kubaini maeneo yanayohitaji maboresho. Aidha, alizitaka halmashauri kuanza mapema maandalizi ya kuhakikisha huduma hizo zinaendelea kwa kutenga fedha katika bajeti za mwaka wa fedha 2027/2028.
Kwa mujibu wa takwimu za TDHS-MIS 2022, Mkoa wa Njombe una kiwango kikubwa cha udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano, jambo linaloonyesha umuhimu wa kuwekeza zaidi katika lishe ya mama mjamzito na mtoto, hususan ndani ya siku 1,000 za mwanzo za maisha. Dk. Mfanga amesema kuimarisha huduma za lishe ni hatua muhimu ya kujenga kizazi chenye afya na kupunguza utapiamlo katika jamii.
Credits:Ipp Media,Via Elizabeth John.
Medical Disclaimer
Medical Disclaimer: Taarifa kwenye makala hii ni kwa ajili ya Updates au elimu ya jumla tu na haichukui nafasi ya uchunguzi,Tiba au ushauri wa kitaalamu wa daktari kwa mtu mmoja mmoja. Kama una dharura au tatizo lolote la kiafya, tafadhali Wasiliana na Daktari moja kwa moja hapa.
Je, unahitaji ushauri binafsi au matibabu ya tatizo lolote?
💬 Wasiliana na Daktari Hapa