Ugonjwa wa kipindupindu waua 300 Sudan
Idadi ya vifo vinavyotokana na mlipuko wa kipindupindu nchini Sudan imeongezeka hadi kufikia 348, hiyo ni kulingana na Wizara ya Afya.
Mlipuko huo umeathiri majimbo tisa, na zaidi ya wagonjwa 11,000 wameripotiwa. Wakati huo huo, kuna wasiwasi wa uwezekano wa kuzuka kwa homa ya dengue, baada ya vifo viwili vinavyoshukiwa.
Mvua kubwa na mafuriko yamezidisha kuenea kwa ugonjwa wa kipindupindu tangu Juni.
Kudorora kwa mfumo wa huduma ya afya nchini Sudan kumefanya juhudi za kudhibiti magonjwa ya kuambukiza kuwa ngumu zaidi.
Nchi hiyo ya kaskazini-mashariki mwa Afrika imekumbwa na vita tangu Aprili 2023 kati ya jeshi la Sudan chini ya mtawala mkuu wa nchi hiyo Abdel Fattah al-Burhan na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF), kinachoongozwa na makamu wake wa zamani Mohamed Hamdan Daglo.
Mgogoro huo umeibua mojawapo ya majanga makubwa zaidi ya kibinadamu duniani, huku zaidi ya watu milioni 25 -zaidi ya nusu ya idadi ya raia wa Sudan – wakikabiliwa na njaa kali.
FAHAMU ZAIDI UGONJWA HUU,NDANI YA AFYACLASS;
Ugonjwa wa Kipindupindu husababishwa na nini? dalili,Madhara na Matibabu yake
Ugonjwa wa kipindupindu(Cholera) ni ugonjwa unaosababisha watu kuharisha, na ugonjwa huu huweza kusababisha kifo ndani ya masaa machache kama mtu hajapata Tiba.
Kwa Mujibu wa Takwimu za Shirika la Afya Duniani(WHO);
Watafiti wamekadiria kuwa kila mwaka kuna visa milioni 1.3 hadi 4.0 vya kipindupindu, na vifo 21,000 hadi 143,000 duniani kote kutokana na kipindupindu
“Researchers have estimated that each year there are 1.3 to 4.0 million cases of cholera, and 21 000 to 143 000 deaths worldwide due to cholera (1)”.
Ugonjwa wa kipindupindu ni Mojawapo kati ya magonjwa yanayohusishwa na umaskini na uchafu wa kupindukia. Inaripotiwa kuwa Kipingupindu ni miongoni mwa magonjwa ambayo huathiri jamii maskini zaidi kwa kiasi kikubwa hasa hasa kwenye nchi zinazoendelea, kiasi kwamba Shirika la Afya Duniani (WHO) limeuweka ugonjwa huu kama mojawapo ya viashiria vya maendeleo ya jamii husika. Nchini Tanzania hususani katika jiji la kibiashara la Dar es Salaam, haishangazi basi kusikia kila mwaka kuna mlipuko wa ugonjwa huu pamoja na juhudi kubwa za serikali na mamlaka zake kujitahidi kuhimiza wananchi kupambana na ugonjwa huu.
Kwanini nchi zinazoendelea?
Moja wapo ya changamoto zinazokabili nchi zinazoendelea ni jamii kutokuwa na uhakika wa kupata Maji safi na salama, pamoja na kutokuwa na mazingira safi kwa ujumla. Ndio maana mpaka leo nchi zinazoendelea ndizo zinazokumbwa na mlipuko wa kipundupindu au huwa katika hatari ya mlipuko wa ugonjwa huo.
Kipindupindu husababishwa na nini?
Ugonjwa huu hutokana na maambukizi katika utumbo mdogo wa binadamu uletwao na vimelea vya bacteria vijulikanavyo kitaalamu kama Vibrio cholerae.
Jinsi unavyoweza kuambukizwa
Kwa kawaida vimelea hawa hupendelea kuishi katika kinyesi cha binadamu. Mtu anaweza kuambukizwa ugonjwa huu kwa kunywa maji ama chakula kilichochafuliwa na kinyesi chenye vimelea hivi vya kipindupindu.
Mara baada kula chakula au kunywa maji yaliyochafuliwa, baadhi ya vimelea hivi huuwawa kwa tindikali iliyopo kwenye tumbo (stomach) pindi chakula au maji haya yanapoingia tumboni. Hata hivyo baadhi ya vimelea hawa hufanikiwa kukwepa ukali wa hii tindikali na hivyo kuendelea kuishi. Vimelea waliofanikiwa kuepukali tindikali ya tumbo la binadamu, hujongea kwenda kwenye ukuta wa utumbo mdogo kwa kutumia ‘maumbo’ maalum yaliyo kwenye miili ya ambayo huwawezesha kusafiri ama kwa kitaalamu hitwa flagella. Wawapo kwenye ukuta wa utumbo mdogo Vibrio cholerae hutoa sumu iitwayo CTX au CT (cholera Toxin) ambayo husababisha mtu kuharisha choo chenye majimaji, papo hapo kuendelea kutoa kizazi kingine cha vimelea hao nje kwa njia ya haja kubwa. Iwapo choo hicho cha mtu aliyeambukizwa kipindupindu kitachanganyika na chanzo cha maji au chakula, watu wengine huambikzwa kirahisi. Hali kadhalika iwapo ni kwenye choo ambacho hakipo kwenye mazingira ya usafi kuna hatari ya choo cha mwambukizwa kuchanganyika na chanzo cha maji au chakula na hivyo kupelekea watu wengi zaidi kuambukizwa ugonjwa huu.
Dalili za kipindupindu ni zipi?
Dalili za mwanzo kabisa za kipindupindu ni
• Kuanza Kuharisha ghafla choo chenye majimaji (ambacho rangi yake ni kama maji ya mchele) na chenye harufu mbaya kama shombo ya samaki.
• Kutapika
Aidha mgonjwa wa kipindupindu huonesha dalili zakupungukiwa maji mwilini kama vile
• ngozi huwa kavu,
• midomo kukauka,
• mgonjwa kuhisi kiu kikali,
• machozi kutoweza kutoka,
• kupata mkojo kidogo sana,
• Kuishiwa nguvu na kujisikia mchovu sana.
• Macho kutumbukia ndani hasa kwa watoto.
SOMA Zaidi hapa;
Dalili za Ugonjwa wa kipindupindu
Kipindupindu ni ugonjwa wa kuhara unaosababishwa na maambukizi ya bakteria wa Vibrio cholerae kwenye Utumbo.
Watu wanaweza kuugua kipindupindu wanapokula chakula au maji yaliyochafuliwa na bakteria wa kipindupindu. Maambukizi mara nyingi huwa hafifu au hayana dalili, lakini wakati mwingine yanaweza kuwa makali na ya kutishia maisha;
DALILI ZA UGONJWA WA KIPINDUPINDU
Kipindupindu – Maambukizi ya Vibrio cholerae
Daktari akimchunguza mgonjwa ataona dalili zote za upungufu wa maji mwilini
Takriban mtu 1 kati ya 10 aliye na kipindupindu atapata dalili kali, ambazo, katika hatua za mwanzo, ni pamoja na:
– kuhara kwa maji mengi, wakati mwingine hufafanuliwa kama “kinyesi cha maji ya mchele”
– Mgonjwa kutapika sana
– Mgonjwa kupata kiu sana
– Kupata maumivu ya miguu
– kutotulia au kuwashwa n.k
Wahudumu wa afya wanapaswa kuangalia dalili za upungufu wa maji mwilini wanapomchunguza mgonjwa aliye na kuhara kwa maji mengi. Hizi ni pamoja na:
– moyo kwenda mbio
– Ngozi ya mwili kuwa kavu sana na kupoteza elasticity ya ngozi
– utando wa mucous kavu
– shinikizo la chini la damu
Watu walio na kipindupindu kikali wanaweza kupata upungufu mkubwa wa maji mwilini, ambayo inaweza kusababisha kushindwa kwa figo. Ukikosa kutibiwa, upungufu mkubwa wa maji mwilini unaweza kusababisha mshtuko, kukosa fahamu na kifo ndani ya saa chache.
Shida hii ya kuharisha kutokana na Ugonjwa wa kipindupindu huambatana na kiasi kikubwa cha vijidudu vya kuambukiza vya Vibrio cholerae vinavyoweza kuwaambukiza watu wengine wakivimeza. Hii inaweza kutokea wakati bakteria huingia kwenye chakula au ndani ya maji.
Ili kuzuia bakteria kuenea, kinyesi (takataka za binadamu) kutoka kwa watu walio wagonjwa kinapaswa kutupwa kwa uangalifu ili kuhakikisha kuwa hakiambukizi chochote kilicho karibu.
Watu wanaowahudumia wagonjwa wa kipindupindu lazima wanawe mikono kabisa baada ya kugusa kitu chochote ambacho kinaweza kuwa na kinyesi cha wagonjwa (kinyesi).
Wagonjwa wa kipindupindu wanapotibiwa haraka, kwa kawaida hupona bila matokeo ya muda mrefu. Wagonjwa wa kipindupindu kwa kawaida hawawi wabebaji wa bakteria ya kipindupindu baada ya kupona, lakini huwa wagonjwa ikiwa wataambukizwa tena.
Vipimo vya utambuzi wa Kipindupindu
Kwa kawaida kipindupindu huweza kugunduliwa na kutambuliwa kwa kutumia dalili. Hata hivyo ili kuthibitisha kuwa mlipuko uliotokea ni kweli kipindupindu, vipimo vifuatavyo huweza kufanyika
Kupima damu kwa ajili ya kuotesha vimelea vya kipindupindu maabara.
Kuchunguza choo kwa kutumia darubini (dark field microscope) ambapo vimelea hivi vya V. cholerae huweza kuonekana. Vile vile choo hiki hutumika kuotesha vimelea vya v. cholerae kwa ajili ya utambuzi zaidi.
Tiba ya Kipindupindu
Lengo kuu katika kutibu kipindupindu ni kurejesha maji na madini ambayo mgonjwa wa kipindupindu hupoteza kwa wingi baada ya kuharisha na kutapika.
Njia kuu zitumikazo katika kumrejeshea mgonjwa wa kipindupindu maji na madini aliyopoteza ni kwa kumpatia maji maalum yenye madini hayo kwa njia ya mdomo, yaani kwa kumpa anywe au kwa njia ya mshipa wa damu ambayo kitaalamu huitwa intravenously (i.v)
ORS
Pamoja na ORS hiyo ambayo imetengenezwa na kuwekwa kwenye paketi tayari kwa matumizi, Shirika la afya duniani (WHO) limetoa pia mwongozo wa kutengeneza maji yenye madini yanayohitajika mwilini (oral rehydration fluid) ambao ni rahisi na usio na gharama.
ORS ya kutengeneza nyumbani kwa kadiri ya muongozo huo huitaji kuchanganya na
• Lita moja ya maji safi na salama,
• Changanya na vijiko vidogo vinane vya sukari, kisha
• Ongeza na kijiko kidogo kimoja cha chumvi
• Aidha, unaweza kuongeza nusu glasi ya juice ya machungwa au nusu ya ndizi (tunda) lilipondwapondwa kwa kila lita, ili kuongeza madini ya potassium na pia kuboresha ladha.
Kwa wagonjwa wenye hali mbaya na wale waioweza kunywa wenyewe, hupewa maji yenye madini mbambali kwa njia ya mshipa wa damu. Maji haya huitwa kitaalamu kama Ringer’s Lactate.
Mwongozo wa kufuata katika kutibu kipindupindu
Baada wa mgonjwa kuwasili katika kituo cha afya, hupimwa kiwango cha upungufu wa maji kilichopo mwilini.
Kisha muhudumu wa afya husahihisha upungufu wowote wa maji utakaonekana kwa awamu mbili. Kwanza kwa kati ya masaa 4-6 ya kwanza tangu kuwasili kituoni na kuendelea mpaka hali ya kuishiwa kwa maji mwilini itakapoonekana imekwisha.
Mhudumu wa afya hutakiwa kurekodi kwenye chati maalum kiasi cha maji anayokunywa mgonjwa na kiasi cha mojo anachokojoa.
Njia ya mshipa hutumika pale tu, hali ya mgonjwa inapokuwa mbaya sana au pale ambapo mgonjwa hawezi kunywa chochote mwenyewe. Aidha kiasi cha maji kitolewacho kwa njia hii ya mshipa wa damu hwa ni kati ya 50-100 mL kwa kilo za uzito wa mgonjwa kwa saa.
Baada ya hapo, mgonjwa huendelea kupewa ORS anywe kwa kiwango cha 800 mpaka lita moja kwa saa
Matumizi ya dawa katika kutibu kipindupindu
Ieleweke kuwa tiba sahihi na makini ya ugonjwa huu wa kipindupindu ni kumrejeshea mgonjwa maji na madini aliyopoteza wakati wa kuharisha na kutapika kwa njia ambazo zimeelezwa hapo juu. Matumizi ya dawa (antibayotiki) husaidia tu kufupisha muda wa kuwatoa wadudu na wala yasitumike kama tiba kuu ya ugonjwa huu.
Baadhi ya dawa ambazo hutumika katika matibabu ya ugonjwa huu ni Azithromycin naTetracycline.
Jinsi ya kuzuia kipindupindu
Mara kwa mara serikali na taasisi zake zimekuwa zikihimiza watu jinsi ya kujikinga na ugonjwa huu wa kupindupindu. Miongoni mwa njia zinazofaa katika kuzuia milipuko ya ugonjwa huu ni
Upatikanaji wa maji safi na salama, watu hawana budi kuhakikisha kuwa maji ya kunywa yanachemshwa vyema kabla ya kuyanywa. Vile vile wanaweza kutumia chlorine katika maji ambayo huua vimelea hawa wa V. cholerae.
Ni muhimu kunawa mikono baada ya kutoka chooni na kabla ya kula
Tunashauriwa kufunika chakula kikiwa mezani ili nzi wasitue juu yake
Inashauriwa kujenga choo umbali wa angalau mita 30 kutoka chanzo cha maji
Inashauriwa kwa wasafiri watokao nchi zilizoendelea kupata chanjo iitwayo Dukoral, pindi wanaposafiri kwenda nchi zinazoendelea.
KWA USHAURI ZAIDI,ELIMU AU TIBA JUU YA TATIZO LOLOTE TUWASILIANE KWA NAMBA +255758286584.