BUNGE LAPITISHA BAJETI YA WIZARA YA AFYA KWA KISHINDO
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeridhia na kupitisha kwa kishindo Bajeti ya Wizara ya Afya ya jumla ya Shilingi Shilingi trilioni moja, bilioni mia tatu kumi na moja, milioni mia nane thelathini na saba, laki nne na sitina na sita elfu (1,311,837,466,000.00) ili kuweza kutekeleza malengo na vipaumbele iliyojiwekea kwa Mwaka wa Fedha 2024 /2025.
Waziri wa Afya Mhe Ummy Mwalimu amesema Serikali imeendelea kuimarisha huduma za uchunguzi ambapo imeendelea kuimarisha huduma za Radiolojia nchini ambapo katika kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024, Wizara imenunua na kusimika mashine za Digital X-ray zenye thamani ya Shilingi 875,750,006. Aidha, usimikaji utakapokamilika utawezesha Sekta ya Afya kuwa na jumla ya Digital X-Ray 349.
Aidha, Wizara imekamilisha ununuzi wa mashine ya Ultrasound 125 zenye gharama ya Shilingi 4,695,000,000 ambapo zote zimesimikwa na kuanza kutoa huduma katika vituo vya kutolea huduma za Afya na Vyuo vya mafunzo ya watalaam wa mionzi na picha ambapo ongezeko hilo la Ultra Sound 125 utawezesha Sekta ya Afya kuwa na jumla ya Ultrasound 677.
Pia, Waziri Ummy amesema hadi kufikia Machi 2024 usimikaji wa mashine za CT scan 27 ulikuwa umekamilika na huduma kuanza kutolewa katika Hospitali za Rufaa za Mikoa ambapo jumla ya vipimo 44,646 vilikuwa vimefanyika.
“Kwa upande wa MRI usimikaji ulikamilika na kuwezesha jumla ya vipimo 18,056 kufanyika katika ngazi ya Taifa, Kanda na Maalum. Kuanza kupatikana kwa huduma hizo kumewawezesha wananchi kuokoa gharama za kufuata huduma hizo umbali mrefu”. Amesema Waziri Ummy Mwalimu wakati wa uwasilishaji wa bajeti ya wizara ya afya kwa mwaka wa fedha 2024/25 bungeni jijini Dodoma.