Fahamu hatari ya kutumia mafuta yaliyotumika
Wataalamu wa afya wameonya kuwa kutumia mafuta zaidi ya mara moja kukaangia chipsi, samaki, maandazi, kuku na vyakula vingine kumetajwa kuwa chanzo cha magonjwa yasiyoambukiza na saratani.
Ununuaji wa vyakula, hasa vilivyokaangwa tayari imeelezwa kuwa hatari zaidi ikiwa hufahamu mafuta yaliyotumika.
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, mafuta yakichemka yanafika nyuzi joto ya juu, yanaungua na kupoteza ufanisi kazi wake na hivyo hutengeneza sumu, inayozalisha kemikali inayoenda kukaa katika leya ya ndani ya utumbo ambayo matokeo yake hutengeneza uvimbe unaogeuka kuwa saratani.
Ofisa muuguzi muelimishaji, Elizabeth Likoko anasema mafuta yanapochemshwa kwa muda mrefu yanatengeneza sumu ambayo inaingia kwenye chakula kinachopikwa wakati huo na mtu akila zile kemikali zinaingia kwenye leya ya utumbo kila siku, zikizidi zinatengeneza uvimbe unaogeuka kuwa saratani.
Anataja ulaji wa mafuta mengi kuwa na athari kubwa. “Kwenye familia ya watu wanne ile chupa ndogo ya mafuta ya kula ya mililis 500 tuitumie kwa mwezi mmoja na katika kukaanga kwa mfano unakaanga kuku au samaki inatakiwa ukadirie kwa kadiri samaki unaokaanga, usiweke mengi ili yale mafuta baada tu ya kukaanga uyamwage. Hayafai kutumika tena.”
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Tatizo Waane anasema mafuta yanapotumika zaidi ya mara moja husababisha kuzalishwa kwa kemikali hatari mwilini ambazo ni chanzo cha magonjwa mengine yasiyoambukiza, ikiwemo saratani ya utumbo mpana.
Sayansi ya mapishi
Kutokana na ulaji usiofaa wa vyakula vyenye mafuta mengi, wengi wamejikuta wakiwa na vitambi na uzito usiokuwa sawia na urefu wao ‘BMI’ na hivyo kujiweka hatarini kupata maradhi hayo yanayokua kwa kasi nchini.
Daktari kutoka Taasisi inayoshughulika na masuala ya chakula na lishe ya Nsambo Healthcare Polyclinic, Boaz Nkumbo anasema katika sayansi ya mapishi zipo familia zinazozalisha vyakula vinavyokwenda kuwa janga kwa walaji.
Dk Nkumbo anataja makosa madogo madogo ambayo hufanywa na mpishi wakati wa kuandaa chakula jikoni, yanayoleta matokeo hasi katika afya ya binadamu.
“Ninaiona jamii ina uwezo wa kupika chakula kizuri chenye madoido mengi, kitamu, pilau likipikwa pale na samaki nazi huyo ndiyo unamla vizuri. Lakini huyu samaki akiwa amekaangwa pale na mafuta ya mbegu yaliyokaangiwa maandazi jana, wali umepikiwa mafuta ya mbegu yaliyokaangiwa samaki jana,” anasema.
Dk Nkumbo anasema wengi wamekuwa wakikosa kuwa na ufahamu wa sayansi ya mapishi, hivyo kujikuta wakipika vyakula vyao kimakosa.
Anasema ni makosa makubwa kupikia mafuta ambayo tayari yalishapikiwa chakula kingine, kwani huwa yamechemka kufikia kiwango cha juu cha joto na hayatakiwi kupikiwa kwa mara nyingine, kwani yana athari.
“Mkeo anaweza akawa anajua kupika, lakini hajui sayansi ya kile anachokipika, anaweza kuwa anakupikia chakula kitamu lakini chakula kile kinakuletea kisukari, kinakunenepesha, kinakutolea nguvu za kiume, chakula hicho kinakuletea saratani na magonjwa mengine,” anasisitiza.
Dk Nkumbo anasema kuna umuhimu mkubwa wa kujua kile kinachoendelea kwenye mwili wako na msukumo wa kujitathmini na kuona nini unapaswa kufanya ili kuboresha afya yako.
“Kitambi kinatokana na wewe kukosa elimu jinsi ya kuishi na fedha ulizo nazo, chakula ulichonacho, kukosa elimu ya jinsi ya kujaza chakula chako kwenye sahani yako, unapokosa elimu ya hayo mambo ndipo unapopata uzito mkubwa na kitambi,” anasema.
Changamoto hiyo imekuwa ikitiliwa mkazo zaidi na maofisa lishe mbalimbali nchini, ambao wamekuwa wakitoa elimu ya namna ya kukiandaa na kuchanganya chakula ili kupata matokeo bora.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Dk Grace Magembe anasema sayansi ya kupika ni jinsi unavyokiandaa chakula chako, kwani kuna baadhi ya vyakula ambavyo virutubisho vyake vinapotea haraka sana kwenye joto kubwa.
Anataja mboga za majani kwamba wengine huziunga na nazi, mchicha kupikwa kwa saa zima kuna virutubisho hupotea, huku akisema vipo vyakula vinavyoshauriwa kupikwa kwa muda mrefu ili vilainike, yakiwemo makande.
“Unapika chakula unajaza mafuta mengi sana au chumvi nyingi kinakuwa si chakula na badala yake kinaleta madhara, lakini wakati mwingine unatengeneza chakula hukipiki kikaiva vizuri kinabaki na wadudu, minyoo, kwa hiyo anavyokula anapata minyoo, wakati mwingine nyama zinapikwa haziivi vizuri, kunakuwa na wadudu kama minyoo, baadaye wanahamia kwenye mwili wa binadamu,” anasema.
Anasema wakati mwingine chakula kinapikwa cha aina moja, huku akielezea umuhimu wa kuchanganya na kitu kingine. “Kande watoto wanakula siku nzima na ni mahindi ya kuchemsha pekee, weka maharage mule ndani, njugu mawe, unaweza ukaweka njegere, carrot, hoho, kitunguu, wengine wanaweka mpaka nyama kwenye makande, hayo yanakuwa mlo kamili, mtoto akila anapata afya njema.”
Dk Magembe anasema wengine wanawapikia watoto uji wa dona peke yake bila kuchanganya na vitu vingine kama soya, karanga na kwa wafugaji hawaongezi maziwa au mayai ili watoto wapate afya.
Anasema changamoto kubwa nchini watu wanaweza kuwa na chakula lakini namna ya kukichanganya ili kiweze kutoa virutubisho vyote vinavyohitajika ikawa ni changamoto, lakini elimu inaendelea kutolewa.
“Tumewaagiza maofisa lishe waweze kutoa elimu. Wakati mwingine ni ukosefu wa chakula, wakati mwingine tuna chakula hatujui namna ya kukipika, namna ya kukichanganya. Chakula bora ni kilekile kilichopo kwenye mazingira yako, ni vizuri tu ukivichanganya, kwa mfano Wahaya wanapika ndizi wanaweka na kitunguu, hoho, nyanya chungu, maharage, mchicha kinakuwa chakula bora,” anasema Dk Magembe.
Athari za mafuta mwilini
Miongoni mwa athari ni pamoja na kuongeza uzito wa mwili, kuziba mishipa ya damu na baadaye mtu kupata presha na huchangia unene kupita kiasi.
Dk Waane anasema mtu mmoja anatakiwa kutumia mafuta ujazo wa nusu dolegumba kwa siku na asizidishe zaidi ya hapo, hivyo mtu anapokula mafuta mengi, uwezekano wa kupata shinikizo la damu ni mkubwa.
“Ni muhimu katika chakula, usile chukuchuku, umuhimu wa mafuta mwilini upo na yaliwe kiasi kwa kuwa vitamin aina nne A, B, C na E zinaingia mwilini iwapo chakula kina mafuta lakini yasiwe mengi,” anasema.
Mkurugenzi wa Kinga kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) Dk Crispin Kahesa, anasema ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi ni chanzo cha magonjwa ya saratani.
“Mafuta na sukari vyote kwa ujumla wake vinachangia kwa kiasi kikubwa kusababisha unene kupita kiasi na hivyo ndivyo visababishi vya saratani zilizo nyingi,” anasema Dk Kahesa.
Mwenyekiti wa chama cha wagonjwa wa kisukari nchini, Profesa Andrew Swai anasema ni mafuta kiasi kidogo yanayohitajika mwilini, kwani yakivunjwavunjwa kilocarolies zinazohitajika ni kiasi kidogo kutoka kwenye hicho kiini lishe, kwani mwili unahitaji kilocaloris 9 ambazo ni nyingi na unapozidisha unaupa mwili calori nyingi na masalia mengi yanabaki mwilini.
Licha ya mafuta yaliyorudiwa, virutubisho vya mafuta ‘transfat’ ambavyo mara nyingi hupatikana katika vyakula vya vitafunio, bidhaa zilizookwa na baadhi ya mafuta ya kupikia, navyo vimethibitishwa kuwa huziba mishipa ya damu, kusababisha mshtuko wa moyo na kifo.
Daktari bingwa wa magonjwa ya fiziolojia ya homoni na mazoezi na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Muhas, Dk Fredrick Mashili ambaye amefanya tafiti kadhaa katika eneo hilo, anasema takwimu zinaonyesha kila mwaka, wastani wa watu 10,000 barani Afrika hufa mapema kutokana na ugonjwa wa moyo unaosababishwa na matumizi ya virutubisho vya mafuta.
Kwa mujibu wa Dk Mashili, katika uchunguzi walioufanya walipima kiwango cha mafuta kwenye vyakula vilivyokaangwa sana kwa kuchemshwa kwa nyuzi joto kubwa, hali ambayo husababisha asidi hiyo kujizalisha na kugundua baadhi ya mafuta yana viwango vikubwa vinavyozidi asilimia 2.
“Tulibaini baadhi ya vyakula vina mpaka viwango vya asilimia 8 vya asidi hiyo ambayo inaleta athari kubwa kwa kusababisha magonjwa ya moyo na mishipa ya damu kuziba,” anasema.
Anasema walibaini kiwango kikubwa cha asidi hiyo kwenye mafuta yaliyochakatwa kiwandani katika aina 10 maarufu ya mimea kwa matumizi Dar na Zanzibar baada ya kuyachunguza.
Chanzo: mwanachidigital