Miili ya watoto wawili kufanyiwa vipimo vya DNA Hanang
Maporomoko ya tope, magogo, mawe, maji na miti yalitokea alfajiri ya Desemba 2, 2023 katika Mji Mdogo wa Katesh, wilayani Hanang.
Dar es Salaam. Serikali imesema miili ya watoto wawili wa kike wa mwaka mmoja na miaka mitatu iliyoopolewa kwenye maporomoko ya tope mkoani Manyara, inafanyiwa vipimo vya vinasaba (DNA) ili kujiridhisha na utambuzi wake.
Vifo vya watu 87 vimethibitishwa na Serikali na miili ya wahusika imeshatambuliwa na kuchukuliwa na familia zao.
Hayo yameelezwa na Msemaji wa Serikali, Mobhare Matinyi kupitia taarifa aliyoitoa kwa umma leo Desemba 13,2023.
“Bado utafutaji unaendelea. Serikali inaendelea kugharamia mazishi na kutoa mkono wa pole wa Sh1 milioni kwa kila mwili kwa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan,” amesema.
Kuhusu majeruhi, Matinyi amesema idadi inaendeelea kupungua na hadi kufikia saa tisa alasiri ya leo Desemba 13,2023 wamebakia 15 kutoka 139 waliofikishwa hospitalini na kupatiwa matibabu.
Amesema katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara majeruhi wapo tisa, Hospitali ya Wilaya ya Hanang (Tumaini) wapo watatu, na Kituo cha Afya Gendabi, watatu. Matibabu ya majeruhi wote yanagharamiwa na Serikali.
Kuhusu waathirika walio kwenye makambi, Matinyi amesema wamebaki 96 ambao Serikali inaendelea kuwaunganisha na ndugu zao.
Amesema kila kaya inayoondoka inapewa chakula na mahitaji muhimu ya kuwasaidia kuendelea na maisha.
“Hadi sasa waathirika 438 wa kaya 119 wameunganishwa na ndugu na jamaa zao. Kuna mchakato wa kuziunganisha na ndugu zao kaya zingine 31 zenye watu 96,” amesema.
Matinyi amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea kusimamia suala la afya kwa umma, na kuhakikisha magonjwa ya mlipuko hayatokei katika eneo lote lililoathirika na maafa.
Amesema juhudi hizo zinahusisha kuzitembelea kaya, na hadi sasa kaya 5,410 zimeshafikiwa na dawa 102,405 za kutibu maji zimeshagawiwa.
“Waathirika wengine 1,853 wameshapatiwa msaada wa kisaikolojia na timu ya wataalamu wa Wizara ya Afya, wakiwamo wauguzi wawili, madaktari bingwa watatu wa afya ya akili na maofisa ustawi wa jamii 91 kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu,” amesema.
Kwa wanaotaka kutoa msaada, amesema Kamati ya Maafa ya Taifa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, imetoa akaunti ya benki ya kutuma fedha kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 6 ya mwaka 2022.