Kimbunga Hidaya na kinachoendelea kwa sasa
Pwani ya Afrika Mashariki hususan Tanzania inatazamiwa kukumbwa na Kimbunga Hidaya ambacho kitasababisha mvua kubwa.
Mapema wiki hii Mamlaka ya hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitangaza kuwepo kwa mgandamizo mdogo wa hewa ambao ulitarajiwa kutawala na kusababisha mvua kubwa na upepo mkali katika mikoa mitano nchini ikiwa ni pamoja na Mtwara, Dar es Salaam, Lindi, maeneo ya Tanga, Morogoro, visiwa vya Pemba na Unguja pamoja na maeneo jirani.
Kimbunga Hidaya kilianza kujitengeza siku ya Jumatano kusini mwa Bahari ya Hindi kuelekea mashariki mwa Tanzania na kaskazini-mashariki mwa visiwa vya Komoro.
Kwa mujibu wa TMA, kufikia sasa mienendo ya mifumo ya hali ya hewa baharini bado inaonesha uwezekano mkubwa wa Kimbunga Hidaya kuendelea kusogea karibu na pwani ya Tanzania na kuendelea kuwepo hadi Jumatatu, Mei 6 2024.
Kulingana na mamlaka hiyo, kimbunga hicho kinaendelea kuimarika na kwamba hadi kufikia usiku wa kuamkia leo kasi yake ilikuwa imeimarika na kufikia kilomita 110 kwa saa.
Taarifa ya mamlaka hiyo aidha ilisema kwamba kimbunga hicho kitaendelea kuimarika na kuwa kikubwa zaidi katika saa 24 zijazo.
Tahadhari zilizotolewa na TMA?
Serikali imewashauri wananchi kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri wa hali ya hewa ili kupata ushauri na mwongozo wa wataalamu katika sekta husika kwa lengo la kujikinga na athari zinazoweza kuibuka.
TMA imesema kwamba ongezeko la mvua na upepo mkali utakaoambatana na mawimbi makubwa baharini vinatarajiwa kusambaa katika maeneo mengi ya ukanda wa pwani kuelekea tarehe 4 hadi 6 mwezi Mei 2024.
Kutokana na hilo, TMA imetoa tahadhari kwa wananchi katika maeneo husika na wote wanaojihusisha na shuguli mbalimbali baharini .
Vilevile Mamlaka hiyo imewataka Watanzania kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri wa hali ya Hewa.
Kenya imesema nini?
Serikali ya Kenya siku ya Alhamisi tarehe 2, Mei ilionya kwamba eneo la Pwani huenda likakumbwa na kimbunga Hidaya ndani ya siku chache zijazo kutokana na mvua kubwa inayoshuhudiwa kwa sasa kote nchini humo.
Onyo hilo lilitolewa baada ya kikao maalum cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika Alhamisi kujadili hatua za ziada za kukabiliana na athari mbaya zinazoendelea za mafuriko, maporomoko ya udongo na maporomoko ya ardhi.
Baraza la Mawaziri lilifahamishwa kuhusu utabiri wa hali ya hewa kwa muda wa miezi mitatu ijayo, ambao ulionyesha kuwa mvua za wastani hadi juu ya wastani zitaendelea kunyesha katika maeneo yote ya nchi.
Kimbunga ni nini?
Kulingana na Shirika la Hali ya Hewa Ulimwenguni, kimbunga cha kitropiki – ni dhoruba inayozunguka kwa kasi ambayo huanza juu ya bahari ya kitropiki.
Kimbunga cha Kitropiki katika Bahari ya Hindi kina nguvu zaidi kuliko dhoruba ya kitropiki.
Ilipewa jina la ‘Hidaya’ na Meteo France La Reunion, huku mifano ya utabiri ikiifuatilia magharibi-kaskazini-magharibi kati ya Mei 2-4, 2024.
Kimbunga cha mwisho kuikumba Tanzania ilikuwa mwaka 1952 (wakati huo koloni la Tanganyika) na kilitua mkoani Lindi katika pwani ya kusini ya Tanzania.
Kimbunga cha mwisho kuikumba Zanzibar kilikuwa mwaka 1872 na athari zake zilifika mpaka upande wab ara katika eneo la Bagamoyo, kaskazini mwa Dar Es Salaam.
Ikiwa Kimbunga Hidaya kitatua kwa kasi, itakuwa ni mara ya kwanza katika historia kwa Dar Es Salaam kukumbwa na kimbunga.
Katika miaka ya hivi karibuni, Tanzania pia ilikuwa katika ya kupigwa na vimbunga vingine viwili, mwaka 2019 Kimbunga Kenneth kilitabiriwa kupiga mkoa wa Mtwara lakini hata hivyo kilibadili mwelekeo na kutua nchini Msumbiji.
Mwaka 2021 ilitolewa tahadhari ya Kimbunga Jobo lakini hata hivyo kilipunguza makali na hakikusababisha maafa yeyote makubwa.