TANZANIA YAVUNJA REKODI MATIBABU YA MOYO
Na Mwandishi wetu – Dar Es Salaam.
Upasuaji mdogo wa moyo wa kubadilisha valvu ya mshipa mkubwa wa damu (Aortic Valve) bila kufungua kifua (Transcatheter Aortic Valve Implantation procedure – TAVI)
Upasuaji huo wa historia umefanyika kwa wagonjwa watatu wenye umri wa zaidi ya miaka 70 katika kambi maalumu ya matibabu ya siku mbili iliyofanywa na wataalamu wa magonjwa ya moyo na mishipa ya damu wa JKCI na wenzao wa Hospitali ya Starcare ya nchini India.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. John Jingu alisema uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika sekta ya afya hii ikiwa ni pamoja na kujenga majengo ya kisasa, kusomesha wataalamu na kuunua vifaa tiba vya kisasa kumewezesha kufanyika kwa upasuaji huo.
Dkt. Jingu alisema kutokana na umuhimu mkubwa wa sekta ya afya Serikali itaendelea kuboresha huduma ya afya ikiwa ni pamoja na kusomesha wataalamu katika nchi mbalimbali ambao watakuja kutoa matibabu ya kibingwa nchini.
Kwa Julai hadi Disemba mwaka huu alidokeza kuwa JKCI imehudumia zaidi ya wagonjwa 3,000 katika kufanya upasuaji mkubwa na mdogo wa moyo na kusisitiza Serikali itaendelea kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kibingwa za matibabu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge aliishukuru Serikali kwa kuiwezesha Taasisi hiyo ambayo imeweza kufanya matibabu hayo ya kihistoria ambapo kwa nchi za Afrika hakuna hospitali ya Serikali inayotoa huduma hiyo.
“Serikali ya awamu ya sita imetuwekea vifaa vingi ambavyo vimewezesha wagonjwa Wagonjwa wa namna hii ambao ni wengi na walikuwa hawajui waende kutibiwa wapi kufanyiwa matibabu, hata wenzetu walifurahia aina ya vifaa tulivyonavyo ambavyo vimewawezesha wataalamu wetu kufanya upasuaji wenyewe kwa asilimia 90”,alisema Dkt. Kisenge.
Aidha Dkt. Kisenge alisema JKCI imeendelea kuwa kituo cha utalii tiba ambapo wagonjwa kutoka nchi 20 za Afrika zinafika kwenye taasisi hiyo kupata matibabu kutokana na wingi wa wagonjwa, aliiomba Serikali jengo lingine kwaajili ya kuwahamishia wagonjwa ombi ambalo Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Jingu alisema linafanyiwa kazi.