Linapokuja suala la afya ya wanaume, saratani ya Tezi dume inachukua nafasi kubwa. Ni aina ya pili ya saratani inayogunduliwa kwa wingi kwa wanaume duniani kote, ikifuatiwa na saratani ya mapafu.
Kwa sababu tezi dume ni kiungo cha uzazi ambacho kazi yake kuu ni kusaidia kuzalisha mbegu za kiume – yaani majimaji ambayo hubeba manii wakati wa mshindo.
Watafiti kwa muda mrefu wamekuwa wakijiuliza kuhusu athari za tendo la ndoa kwenye saratani ya tezi dume.
Je, kumwaga mbegu za kiume hukulinda dhidi ya hatari ya saratani ya Tezi dume?
Tafiti za Kisayansi Zinasemaje?
Kuna ushahidi unaounga mkono swali hili. Utafiti uliofanywa katika kipindi cha miaka 33 iliyopita ulionesha kuwa tafiti saba kati ya 11 – ziliona kuna manufaa ya kumwaga mbegu dhidi ya kujilinda na saratani ya tezi dume.
Vile vile, kumwaga manii kunaweza kuongeza kinga ya mwili na kupunguza hatari ya maambukizi – ambapo ni miongoni mwa chanzo cha kukua kwa saratani hii.
Kumwaga mbegu za kiume pia kunaweza kupunguza shughuli za mfumo wa neva, na huzuia seli fulani za kibofu kugawanyika, na kupunguza hatari ya kuwa na saratani.
Umri ni muhimu pia. Kumwaga mbegu mara nyingi hutoa kinga zaidi kwa watu kati ya umri wa miaka 20 na 50 na kuendelea. Lakini kuna hatari kwa vijana wa umri wa miaka 20 na chini ya hapo.
Kumwaga manii kwa kiwango kikubwa wakati wa ujana – kibofu bado kikiwa hakijakomaa, kuna hatari ya kupata saratani ya kibofu miongo kadhaa baadaye.
Utafiti kutoka Chuo Kikuu cha Harvard nchini Marekani ulionesha kuwa wanaume wanaomwaga manii mara 21 au zaidi kwa mwezi wana hatari ndogo ya kupata saratani ya tezi dume kwa 31% kuliko wanaume wanaomwaga mara nne hadi saba kwa mwezi.
Matokeo kama hayo yalipatikana nchini Australia, ambapo saratani ya tezi dume ilikuwa chini ya 36% kwa wanaume walio chini ya umri wa miaka 70, kwa wanaume waliomwaga mara tano hadi saba kwa wiki, ikilinganishwa na wanaume waliomwaga chini ya mara tatu kwa wiki.
Lakini utafiti mwingine unaeleza kuwa kumwaga mbegu zaidi ya mara nne kwa mwezi kunahesabiwa ni kumwaga mara kwa mara na hilo hutoa kinga kwa rika fulani la watu.
Kumwaga mbegu kunaweza kukulinda dhidi ya saratani ya kibofu, lakini pia yawezekana wanaume wanaomwaga manii mara kwa mara wana maisha bora, ambayo hupunguza uwezekano wa kupata saratani.
Kuwa na mzungumko mdogo wa kumwaga mbegu, kunaweza kuhusishwa na kupungua kwa shughuli za kimwili– hayo ni mambo ambayo yanaweza kuchangia kukua kwa saratani.
Homoni za testosterone ni muhimu
Homoni ya testosterone, inafahamika kwa kuongeza hamu ya tendo la ndoa, hivyo mwanaume mwenye viwango vya chini vya testosterone anaweza asiwe na hamu ya tendo.
Maoni ya zamani yalikuwa; viwango vya juu vya testosterone kwa wanaume huongeza hatari ya saratani ya Tezi dume, maoni ya sasa yanaonesha haiongezi hatari hii, na badala yake kiwango cha chini cha testosterone ndicho huongeza hatari.
Wanaume walio na saratani ya Tezi dume, huonyesha kuwa viwango vya testosterone ni vya chini. Hivyo kuwa na homoni nyingi za testosterone hupunguza hatari ya saratani ya Tezi dume kwa wanaume na kuongeza hamu ya kushiriki tendo la ndoa.
Utafiti mwingine ulionyesha kuwa wanaume ambao humwaga mara kwa mara – wana viwango vya juu vya homoni ya testosterone. Na hawa ndiyo wanaume ambao pia wana hatari ndogo ya kupata saratani ya Tezi dume.
Kufanya tendo la ndoa na kumwaga mbegu za kiume kuna faida kwa Tezi dume, ikiwa ni pamoja na faida kwenye moyo, ubongo, mfumo wa kinga, usingizi na hisia.
Uhusiano kati ya kumwaga manii na kuzuia saratani ya Tezi dume haueleweki kikamilifu – Hivo tafiti zaidi zinahitajika – lakini ukweli unabaki kuwa kumwaga kuna faida kwa afya ya mwanaume.