#PICHA:Mvulana mwenye umri wa miaka 2 aligunduliwa kuwa na saratani ya damu na kutibiwa kwa mionzi ya chemotherapi akisubiri kuonana na daktari katika hospitali moja nchini Ghana.
Ikiwa Jana dunia inaadhimisha siku ya kimataifa ya saratani ya utotoni, shirika la Afya duniani WHO; limesema ni vyema wazazi wakapatiwa uelewa wa dalili za saratani za utotoni ili waweze kubaini ugonjwa huo mapema kwani hakuna aliye tayari kuwekeza kila kitu kwa mustakbali wa watoto kuliko wazazi.
Hivyo shirika hilo limesisitiza kwamba kwa kutambua mapema ishara na dalili za aina za saratani na kuchukua hatua muafaka kunaweza kuokoa maisha ya m toto.
WHO imesema mbali ya wazazi pia madaktari wa familia na madaktari wa watoto nao wananchango mkubwa kwenye kugundua mapema saratani kwa watoto.
Saratani ya utotoni ni nini?
Kwa mujibu wa WHO “Saratani ya utotoni” inamaanisha aina mbalimbali za saratani ambazo huwakumba watu walio chini ya umri wa miaka 20.
Aina hizi za saratani ni tofauti na saratani ambazo mara nyingi hugunduliwa kwa watu wazima.
Leukemia, lymphomas, na uvimbe wa mfumo mkuu wa neva ndizo aina za saratani zinazojulikana zaidi kwa watoto.
Uwiano wa aina tofauti za saratani hubadilika kila mwaka watoto wanapokuwa wakubwa, na matukio ya jumla yanaonesha vilele viwili tofauti, katika umri wa miaka 0-4 na kati ya umri wa miaka 15-19.
Kufikia mwaka wake wa kwanza maishani, Nikol alilazimika kutoroka nyumbani kwake huko Ukraine na akagunduliwa kuwa na aina fulani ya saratani.
Kwanini watoto wanapata saratani?
Baadhi ya sababu za kimazingira, kama vile mionzi, zinajulikana kuongeza hatari ya watoto kupata saratani, lakini sababu za saratani nyingi za utotoni bado hazijajulikana.
Utafiti zaidi ni muhimu ili kuboresha uelewa wa jinsi na kwa nini saratani hukua kwa watoto.
Watafiti wa Shirika la Kimataifa la Utafiti wa Saratani – IARC huchangia katika kufanya utafiti kwa njia nyingi, kama vile kwa kuchunguza maelezo mafupi ya epijenetiki ya watoto walio na saratani, kuchunguza vitu katika mazingira, kutathmini mambo ya mtindo wa maisha ambayo yanaweza kuathiri ukuaji wa saratani ya utotoni, na kusawazisha uainishaji wa saratani ya utotoni ili kutambua vyema na kutibu magonjwa hayo.
Utofauti wa kipato cha nchi unamchango mkubwa kwa watoto kuishi
WHO imesema duniani kote watoto zaidi ya 1000 wanabainika kuwa na saratani kila siku.
Maendeleo ya hivi karibuni ya kimatibabu yanaleta nafasi kubwa sana za watoto katika nchi za kipato cha juu kupona saratani ambapo zaidi ya asilimia 80 ya watoto waliogunduliwa na saratani wananusurika.
Hata hivyo watoto kutoka nchi za kipato cha chini na cha kati ni karibu asilimia 20 tu ya watoto waliogunduliwa na saratani ndio wanafanikiwa kuishi.
Juhudi zinafanyika
Mwaka 2018, WHO ilizindua Mpango wa Kimataifa wa Saratani ya Utotoni (GICC). Lengo lake kuu ni kupunguza pengo la kuishi ifikapo 2030, kwa kuhakikisha kuwa angalau asilimia 60 ya watoto walio na saratani ulimwenguni kote watapona baada ya kutambuliwa kuugua.
GICC ni juhudi za ushirikiano zinazohusisha WHO katika kiwango cha kimataifa, kikanda na kwa nchi mahususi, kwa kushirikiana na Hospitali ya Utafiti ya Watoto ya St. Jude.
Nao wanasayansi kutoka Shirika la Kimataifa la Utafiti wa Saratani (IARC) wanashiriki katika Mpango wa GICC kupitia Timu ya IARC GICC na miradi mingi inayoongozwa na watafiti wa IARC inalenga kuelewa na kupunguza mzigo wa kimataifa wa saratani ya utotoni.
Lengo hili adhimu linaweza kufikiwa hasa kwa kuimarisha mifumo ya afya, ili watoa huduma za afya ya msingi – au hata wazazi – waweze kutambua dalili za awali za saratani ya utotoni, na mifumo ya rufaa inaweza kuwaelekeza mtoto mahali kwenye huduma maalum muhimu kwa maisha yao.
Pamoja na matibabu, watoto pia wanahitaji uangalizi makini kwa ajili ya ukuaji wao unaoendelea wa kimwili na kiakili na ustawi wa lishe. Hii inahitaji uangalizi wa timu iliyojitolea, yenye taaluma nyingi.