Watoto wengi zaidi kufa kwa Utapiamlo na ukimbizi Sudan kuliko hata vita yenyewe: UNICEF
Vita nchini Sudan ikitimu siku 300 hii leo, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF linasema bila rasilimali za kutosha, na njia za kusambaza misaada ya kiutu kuwa wazi, watoto wengi zaidi watakufa nchini humo kutokana na utapiamlo na magonjwa kuliko hata kutokana na vita yenyewe.
Shirika hilo kupitia taarifa yake iliyotolewa leo huko Port Sudan nchini Sudan linasema kwa sasa utapiamlo umesambaa nchini humo, ukimbizi wa ndani ni mkubwa kuliko eneo lolote duniani na mfumo wa afya umesambaratika na hivyo vigezo hivyo kutishia kuwa sababu ya vifo miongoni mwa watoto kuliko vita yenyewe.
UNICEF inasema inaona viwango vya juu vya matibabu dhidi ya unyafuzi au utapiamlo uliokithiri kwenye maeneo yanayoweza kufikiwa na misaada ya kiutu, na kwamba kwenye maeneo yasiyofikika kutokana na mazingira ya mapigano hali inaweza kuwa mbaya zaidi.
Takribani watoto milioni 3.5 wanatarajiwa kukumbwa na unyafuzi mwaka huu, wakiwemo zaidi ya 700,000 ambao wanatarajiwa kukumbwa na unyafuzi mkali zaidi na hivyo kuhitaji tiba kamilifu ya kuokoa maisha yao.
Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Catherine Russell akinukuliwa kwenye taarifa hiyo amesema mchanganyiko hatari wa utapiamlo, ukimbizi na magonjwa unaongezeka kila siku na kwamba “tuna muda mdogo sana kuzuia vifo.”
Wanawake na watoto waliokimbia makazi yao katika eneo la Wakimbizi wa Ndani huko Darfur Magharibi kutokana na mapigano nchini Sudan.
Amesema “tunahitaji njia salama, endelevu na ha uhakika ya kufikisha misaada ya kiutu huko kwenye mapigano na mipakani na tunahitaij msaada wa kimataifa ili kuweza kuendeleza huduma na mifumo ambayo watoto wanategemea ili waweze kuishi.”
Ameongeza kuwa “hatuwezi kuwatelekeza watoto wa Sudan. Bila hatua ya dharura Sudan inaweza kuwa na janga la kizazi na zaidi ya yote, watoto wa Sudan wanahitaji sitisho la mapigano na amani.”
Maeneo ambako UNICEF inataka kufikia zaidi ni Darfur ambayo imeshuhudia mapigano makali zaidi na sasa ina wakimbizi zaidi ya theluthi moja ya watu wote milioni 8 waliofurushwa makwao tangu kuanza kwa mapigano Aprili mwaka jana.
UNICEF inasema inahitaji dola milioni 840 kufikia watu milioni 9.9 wakiwemo watoto milioni 7.6 walioko hatarini zaidi. Hadi sasa UNICEF imepokea asilimia 28 tu ya fedha hizo.
Soma Zaidi hapa kuhusu tatizo la Utapiamlo,Chanzo,dalili na Tiba