Sifa za Baba Bora ni Zipi?, Fahamu hapa kwa kina
Utafiti uliochapishwa katika tovuti ya Psychology Today unaonyesha kuwa watoto ambao wapo karibu na baba zao wana hali ya kujiamini na wanaona wako salama na kadiri wanavyozidi kuwa wakubwa uhusiano wao na wazazi unazidi kuimarika.
Pamoja na umuhimu huo wakati mwingine wababa hawasimami kwenye nafasi zao hali inayofanya taratibu thamani yao kupungua na hata kutoweka kabisa na kuacha thamani hiyo itawale upande mmoja.
Mwanasaikolojia Christian Bwaya anasema katika siku za mwanzo za maisha ya mwanadamu, nafasi ya mama katika makuzi haina mjadala.
Anasema mtoto anahitaji vingi kutoka kwa mama kuanzia mahitaji ya kimwili, mahusiano, hakikisho la usalama na kadhalika, kwa msingi huo hata tabia nyingi za ukubwani zinategemea na kiwango cha ukaribu na mama.
“Kwa lugha rahisi mama ndiye anayejenga msingi wa namna tutakavyokuwa baadae kitabia. Hii ndio sababu kwa wengi wetu, mama ndiye alama ya utu wetu.
“Hata tunapojikwaa tunaita mama. Ukiangalia hata wanaume wengi, kama alikuwa na mahusiano mazuri na mama, hutafuta mke anayebeba taswira ya mama yake,”anasema Bwaya.
Hata hivyo mwanasaikolojia huyo anafafanua kuwa hali hiyo haimaanishi kuwa mtoto hamhitaji baba yake.
Anasema mwanamke anapokuwa na mahusiano yenye sonona na magomvi hawezi kuwa na furaha na hilo litaonekana ukitazama tabia ya mwanae.
“Kwa maneno mengine, kama baba anataka kuwa na ushawishi kwa mwanae, kazi kubwa ya kwanza ya kufanya ni kuhakikisha kuwa mke wake ana furaha.
“Uso wa mama wenye furaha unamjenga mtoto kuwa mtu anayejiamini. Lakini pia, mtoto anapopata ufahamu, kazi kubwa ya baba ni kumjenga mwanae kiakili.”
Baba anapaswa kufanya nini
Bwaya anasema uwezo wa mtoto kutambua mema na mabaya na kujenga msimamo wa maisha unamtegemea yeye hivyo inahitajika sauti yake kuyaingiza hayo kwenye moyo wa mtoto.
Ili sauti hii ya baba isikike vizuri na mtoto aamini kile anachoelekezwa na baba yake, ni muhimu itanguliwe na upendo na anapaswa kutambua kuwa ana nafasi ya kumjenga mtoto ikiwa atakuwa karibu na mtoto tangu mapema.
“Ukaribu una maana ya kupatikana, kuwa na mazungumzo na mtoto, kumsikiliza hisia zake na kumwelekeza pale inapobidi. Pia, baba ana kazi kubwa ya kujenga uhakikisho kwa mtoto.
“Hapa tuna maana ya baba kumhakikishia mtoto ile thamani kama binadamu, kumfanya mtoto ajione ni mtu wa maana, anayejitosheleza kama binadamu kamili. Baba akilifanya hili vizuri, mtoot hujenga hali ya kujiamini na ujasiri na matokeo yake ni kuwa karibu zaidi na baba.”anasema Bwaya.
Mwanasaikolojia huyu anaeleza kuwa baba anayemkemea mtoto mara kwa mara, anayefoka na kunyong’onyeza mtoto anamfanya mtoto ajione hana thamani na matokeo yake hujiweka mbali naye.
“Kwa msingi huo, pamoja na kukemea na kuonya pale inapobidi, ni muhimu baba kuwa mtu wa kupongeza, kuona jema kwa mtoto na kulisema. Hili likifanyika vizuri, mtoto huona thamani ya baba yake”anasema.
Mchungaji na mshauri wa masuala ya familia Richard Hananja anasema baba bora ni yule anayebeba wajibu wa familia yake na kuitunza kama ambavyo vitabu vya dini vimekuwa vikieleza.
“Baba anatakiwa kujitoa kwa moyo wake kuitunza familia yake hili anapaswa kufanywa bila kulazimishwa tofauti na ilivyo sasa ambapo wengi wamekuwa wakifanya hivyo kwa kulazimishwa. Inashangaza siku hizi unakuta baba anajiondoa kwenye jukumu la kutunza familia yake kisa mama anafanya kazi, hii si sawa baba unapaswa kuonyesha nafasi yako ili hata watoto wajifunze kutoka kwako,”
Sifa nyingine ya baba kulingana na mchungaji huyo ni kutoa majibu ya maswali yanayoikumba familia, kwa kufanya hivyo anajijengea heshima na thamani si tu kwa watoto bali hata mke.
“Sasa usitengeneze mazingira kwamba kila wanachotaka watoto wanakimbilia kwa mama yao na wanakipata ila wewe kila siku huna, hapa utaitengeneza dharau ndiyo tunasikia wanaume wanalalamika kwamba wanawake wanawadharau,”.
Anasema ni muhimu kwa baba kupata muda wa kutosha wa kuwa na watoto ili awajenge katika mfumo unaofaa kinyume na hapo atakutana na watu wengine nje watakaowapandikiza yasiyofaa.
Mchungaji Hananja anaeleza, “ Sauti ya baba ni muhimu kwenye familia, wewe kama baba una nafasi ya kumjenga mtoto wako vile unataka, mtengenezee mwelekeo wa maisha. Mtoto kuanzia mwaka 0 hadi 7 ndiyo umri wa kumtengeneza sasa kama huna muda wa kukaa naye ukapandikuza vitu vizuri ndani yake tegemea watu wengine kufanya hivyo,”.
Mawazo mchanganyiko
Deus Ngoba mkazi wa Madale anasema wababa wengi hawana muda wa kukaa na watoto wakiamini jukumu hilo ni la mama na wao kazi yao ni kuwatafutia mahitaji jambo linalowafanya wawe mbali na familia.
“Usiogope kutumia muda wako vizuri na mwanao wa kike au wa kiume na kucheza nao na kuwabembeleza wanapolia. Watoto siku zote hukumbuka matendo haya na hivyo kujenga upendo kati yenu na kuzidisha amani kwa familia. Ni vyema kuhamasishana wake kwa waume ili kila mmoja wetu ajione ana uwezo wa kutekeleza majukumu ya malezi.
“Kingine jenga heshima na upendo kwa watoto wako na siyo nguvu. Kila mtu hufurahia kupenda na kupendwa na unaweza kupata upendo wa watoto wako kwa kuwapenda na si kwa kuwaonesha mabavu. Ukiwa mbambe utaishia kupata nidhamu ya uoga na sio heshima na utii wa kweli. Ukiwa kama baba onyesha upendo, heshima na uwajibikaji kwa watoto, mwenza wako na familia kwa ujumla. Kumbuka kwa kufanya hivi unajenga msingi wa tabia za mwanao unayemtaka,”
Kwa upande wake Suzan Mhilu mkazi wa Buza anasema baba bora anapaswa kuishi kwa mfano ili watoto wake waige na kujifunza vitu kutoka kwake.
Anasema kama baba atakuwa anaonyesha vitendo vizuri mbele ya mtoto itamfanya aishi katika mfumo huo na hilo itasaidia watoto kujua umuhimu wa kufikia maamuzi kwa mazungumzo kwa maana ya kutambua kuwa kuna kukubaliana na kutokukubaliana.
Usuli
Siku hii ilianza kuadhimishwa Spokane, Washington nchini Marekani mwaka 1910 na Sonora Smart Dodd mzaliwa wa Arkansas. Baba yake William Jackson Smart alikuwa mwanajeshi wa zamani na aliwalea watoto sita akiwa kama mzazi pekee.
Baada ya miaka kadhaa tangu kuadhimishwa kwa siku hii huko Marekani hatimaye ujumbe ukafika dunia nzima na mataifa mbalimbali yakaanza kuadhimisha siku hii kwa lengo la kuwaenzi kina baba wanaojitoa kwa hali na mali katika malezi ya watoto.
Via:Mwananchi.