Siku ya Kimataifa ya Wanawake inatambua mafanikio ya wanawake, bila kujali utaifa, kabila, dini, utamaduni, lugha, hali ya kiuchumi au mwelekeo wa kisiasa.
Tangu miaka ya mwanzo, harakati la kimataifa la wanawake linalokua, lililoimarishwa na mikutano minne ya Kimataifa ya Umoja wa Mataifa,
limekuwa msingi wa kuunga mkono haki za wanawake na ushiriki wao katika muktadha wa kisiasa na kiuchumi. Ili kuelewa historia ya siku hii kwa undani, lazima tufuate tena mwendo wa saa,
tukizingatia sana tarehe kadhaa ambazo zimefanya adhimisho hili kuwa muhimu kwa mataifa yote: Awali ya yote mnamo 1909, Siku ya Kitaifa ya Wanawake nchini Marekani ilifanyika kwa heshima ya mgomo wa wafanaikazi, ambao walipinga mazingira ya kazi.
Lakini hata hivyo, harakati lilizaliwa mapema kama 1948, kwa sababu wanawake walipozuiwa kuzungumza kwenye kongamano la kupinga utumwa.
Mnamo 1910, Jumuiya ya Kimataifa ya Kijamaa, iliyokutana huko Copenhagen, ilianzisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake, ambayo ililenga kupata haki ya kupiga kura kwa wote.
Mnamo 1911, Siku hiyo, iliyoadhimishwa tarehe 19 Machi, ilikuwa njia ya kuomba haki za wanawake kufanya kazi na mafunzo ya kitaaluma, pamoja na haki ya kupiga kura.
Mnamo 1913, Siku hiyo ikawa utaratibu wa kupinga Vita vya Kwanza vya Kidunia. Mnamo 1915, mkusanyiko wa wanawake zaidi ya 1300 kutoka zaidi ya nchi 12 ulifanyika Hague, kwenye pwani ya magharibi ya Uholanzi. Mnamo tarehe 23 Februari 1917, ya kalenda ya Julian, kwa hiyo ililingana na tarehe Machi 8 ya kalenda ya Gregorian ambapo wanawake nchini Urusi waliandamana na kugoma tena kwa “Mkate na Amani.” Siku nne baadaye, Tsar, yaani Mfalme Mkuu wa Urusi alijiuzulu na kuwapa wanawake haki ya kupiga kura.
Baada ya Vita vya II vya Kidunia, Maadhimishi ya tarehe 8 Machi yalianza kuenea katika nchi nyingi. Lakini kwa nini tarehe 8 Machi? Kabla ya mapinduzi, Urusi, tofauti na nchi zingine, ilikuwa bado haijapitisha kalenda ya Gregorian.
Siku ya mapinduzi ya “Mkate na Amani”, tarehe 23 Februari 1917 katika kalenda ya Julian, kwa hiyo ililingana na tarehe Machi 8 katika kalenda ya Gregorian. Siku hiyo ilitambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa mnamo 1977, wakati iliibuka kwa mara ya kwanza kutoka katika shughuli za harakati za wafanyakazi mwanzoni mwa karne ya 20 huko Amerika Kaskazini na Ulaya. Mwaka huo, Umoja wa Mataifa ulipitisha Azimio 32/142, kutangaza Siku ya Haki za Wanawake na Amani ya Kimataifa kuadhimishwa kila siku ya mwaka.
Kwa njia hiyo maadhimisho haya ni wakati wa kutafakari juu ya mafanikio yaliyopatikana, kuomba mabadiliko mapya na kusherehekea vitendo vya ujasiri na uamuzi wa wanawake ambao wamejitofautisha katika historia.
Ulimwengu umepata maendeleo makubwa katika maeneo kadhaa, lakini hakuna nchi ambayo bado imepata usawa wa kijinsia. Bado kuna mengi ya kufanywa ili kufikia Lengo la Maendeleo Endelevu kifungu cha 5 cha Ajenda ya 2030.
Wanawake wako mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya Uviko-19. Kwa maana hii, gonjwa hilo limewezea kuakisi sana michango yao na ugumu mwingi waliokabiliana nao wanawake. Kwa upande mmoja, kiukweli, viongozi wanawake walionesha ujuzi wao, ujuzi na uzoefu ili kupambana na mgogoro huo.
Kwa mfano, nchi ambazo zilifanikiwa zaidi kukomesha janga hilo zinaongozwa na wanawake. Kwa upande mwingine, zaidi ya vikwazo vya kijamii vinavyoendelea kwa uongozi wa wanawake, wanawake wanakabiliwa na ongezeko la unyanyasaji wa kijinsia, ukosefu wa ajira na umaskini.
Ili kuunga mkono haki za wanawake na kutambua uwezo wao kamili, ni muhimu kuunganisha mitazamo yao katika kubuni na utekelezaji wa sera na programu katika hatua zote za kukabiliana majanga mengi ya ulimwengu huu, kuanzia na matatizo ya kifamilia, hadi kufika katika ngazi kuu za serikali.
Katika maadhimisho haya ya Siku ya wanawake Duniani, shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake UN Women linabainisha kuwa kuna mambo matano ya kuharakisha uwezeshaji wa wanawake kiuchumi. Kuwekeza kwa wanawake kunanufaisha wanawake na jamii kwa ujumla.
Hata hivyo, katika kiwango cha sasa cha uwekezaji, shirika hilo linasema idaidi ya wanawake na wasichana milioni 340 bado wataishi katika umaskini uliokithiri ifikapo mwaka 2030.
Shirika hili limesisitiza kuwa haijawai kuwa muhimu zaidi kuendeleza uwezeshaji wa wanawake kiuchumi, kama ilivyoainishwa na kaulimbiu ya 2024 ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake ambayo ni “Wekeza katika wanawake: Kuharakisha maendeleo”.
Shirika la UN Women linasema dunia inahitaji ziada ya dola bilioni 360 kwa mwaka kwa nchi zinazoendelea kushughulikia usawa wa kijinsia chini ya Malengo ya Maendeleo Endelevu SDGs. Na ingawa kuongeza sehemu ya wanawake ya mali na fedha ni muhimu kwa uwezeshaji wao wa kiuchumi, muhimu vile vile ni kujenga taasisi zinazokuza uwekezaji wa umma katika bidhaa za kijamii na maendeleo endelevu.
Mambo matano yatakayohakikisha kuharakisha uwezeshaji wa wanawake kiuchumi ni:
1: Rasilimali
Kuwaunganisha wanawake na rasilimali za kifedha kunaweza kuwasaidia kukidhi mahitaji yao ya msingi na kuanzisha au kukuza biashara. Hata hivyo, inakadiriwa kuwa biashara ndogo ndogo, ndogo na za kati zinazomilikiwa na wanawake duniani kote zinapungukiwa na ufadhili wa dola trilioni 1.7. UN women inasema kuziba pengo la mikopo kwa wanawake wanaomiliki biashara ndogo na za kati kungesababisha ongezeko la wastani wa asilimia 12 la mapato ya kila mwaka ifikapo 2030. Mbali na rasilimali za kifedha, wanawake wanahitaji kupata ardhi, taarifa, teknolojia na maliasili. Mwaka 2022, ilibainika watu bilioni 2.7 bado hawakuwa na fursa ya mtandao, ambao ni msingi wa kupata ajira au kuanzisha biashara.
Wanawake pia wana uwezekano mdogo kuliko wanaume kumiliki au kuwa na haki salama za ardhi ya kilimo katika asilimia 87 ya nchi ambapo takwimu zinapatikana, licha ya ukweli kwamba zaidi ya theluthi moja ya wanawake wanaofanya kazi wameajiriwa katika viwanda vya kilimo.
2: Ajira
Wanawake wanapostawi katika ulimwengu wa ajira, wanakuwa na fursa nzuri zaidi ya kutumia ushirika wao na kutambua haki zao. Lakini sio kazi yoyote tu itafanya hivyo, kazi lazima iwe na tija na katika hali ya uhuru, usawa, usalama, na heshima.
Hata hivyo, karibu asilimia 60 ya ajira za wanawake duniani ziko katika uchumi usio rasmi, na katika nchi zenye kipato cha chini ni zaidi ya asilimia 90. Na hata wakati wanawake wana kazi, wanalipwa senti 80 kwa kila dola wanayoliwa wanaume kwa wastani, na hata kwa baadhi, ikiwa ni pamoja na wanawake wenye asili ya Kiafrika na kina mama. Ukosefu wa usawa wa kijinsia katika mapato pekee unagharimu dunia zaidi ya mara mbili ya thamani ya Pato la Taifa katika masuala ya utajiri wa mtaji wa binadamu.
Hatua kama vile uwazi wa mishahara, malipo sawa kwa kazi yenye thamani sawa, na upatikanaji wa huduma za matunzo zinaweza kusaidia kuziba mapengo ya malipo ya kijinsia katika ujira na kusababisha usawa wa kijinsia mahali pa kazi. Ulimwengu unaweza kuona ongezeko la asilimia 20 la Pato la Taifa kwa kuziba mapengo ya kijinsia katika ajira. Zaidi ya hayo, wakati wajasiriamali wanawake wanafanikiwa, wanaweza kuunda ajira na kuendeleza uvumbuzi.
3: Muda
Kila mtu anahitaji huduma katika maisha yake. Mfumo wa kijamii wa huduma uliopo unaonyesha tofauti kubwa za hadhi na mamlaka na mara nyingi hutumia nguvu kazi ya wanawake na wasichana. Kwa wastani, wanawake hutumia karibu muda mara tatu zaidi kwenye huduma zisizo na malipo na kazi za nyumbani kuliko wanaume.
Tofauti za kijinsia katika kazi za huduma zisizo na malipo ni kichocheo kikubwa cha ukosefu wa usawa, kuzuia muda wa wanawake na wasichana na fursa za elimu, kazi za kulipwa zenye staha, maisha ya umma, mapumziko na muda wa kujifurahisha. Kazi za huduma bado hazijathaminiwa na zinalipwa kidogo. Thamani ya fedha ya kazi za matunzo zisizo na malipo kwa wanawake duniani kote ni angalau dola trilioni 10.8 kila mwaka, mara tatu ya ukubwa wa sekta ya teknolojia duniani.
Kuwekeza katika kubadilisha mifumo ya huduma na matunzo ni ushindi mara tatu, kutaruhusu wanawake kurejesha wakati wao wakati wa kuunda ajira katika sekta ya huduma na kuongeza ufikiaji wa huduma za matunzo kwa wale wanaozihitaji.
Inakadiriwa kuwa kuziba mapengo yaliyopo katika huduma za matunzo na kupanua wigo wa programu za kazi zenye staha kunaweza kuunda karibu nafasi za kazi milioni 300 kufikia mwaka 2035.
4: Usalama
Wanawake wanakabiliwa na vitisho vingi kwa usalama wao, ikiwa ni pamoja na unyanyasaji wa kijinsia, migogoro, uhaba wa chakula, na ukosefu wa ulinzi wa kijamii. Vurugu nyumbani au kazini ni ukiukwaji wa haki za wanawake na huzuia ushiriki wao kiuchumi.
Gharama ya kimataifa ya unyanyasaji dhidi ya wanawake inakadiriwa kuwa takriban dola trilioni 1.5 au karibu asilimia 2 ya pato la taifa. Idadi ya wanawake na wasichana wanaoishi katika nchi zilizoathiriwa na migogoro ilifikia milioni 614 mwaka 2022, asilimia 50 zaidi ya idadi ya mwaka wa 2017.
Migogoro hiyo inaweza kuzidisha tofauti za kiuchumi zilizokuwepo, kama vile sehemu kubwa ya wanawake ya kazi za huduma isiyo na malipo. Migogoro pia huongeza ukosefu wa usawa miongoni mwa wanawake, kwa mfano, wanawake wahamiaji wana uwezekano mara mbili wa kukumbwa na ukatili kuliko wasio wahamiaji.
Utafiti unapendekeza mifumo ya hifadhi ya jamii inayozingatia jinsia kama vile uhamishaji fedha, unaweza kupunguza viwango vya vifo miongoni mwa wanawake, kuonyesha uhusiano kati ya uwezeshaji wa kiuchumi na usalama. Haijalishi ni mfumo gani, ukosefu wa usalama unazuia uwezeshaji wa wanawake kiuchumi, unawaingiza katika umaskini, na kuwazuia kutambua haki zao na uwezo wao.
Ni muhimu kuwaleta pamoja wadau mbalimbali, ikiwa ni pamoja na katika sekta ya binafsi, na kupinga kanuni za kijamii zinazothamini wanawake kama wa watu wa chini kuliko wanaume watendaji wa kiuchumi.
5: Haki
Haki za binadamu ni msingi wa uwezeshaji wa wanawake kiuchumi. Mifumo isiyo ya haki ya mfumo dume wa kiuchumi huendeleza ukosefu wa usawa wa kijinsia, na kanuni za kijamii za kibaguzi zinakuwa kikwazo kwa wanawake kupata habari, mitandao, ajira na mali.
Ulimwenguni, kwa wastani, wanawake wana asilimia 77 tu ya haki za kisheria zinazofurahiwa na wanaume.
Mikakati muhimu ya kukuza haki za wanawake katika muktadha wa uwezeshaji wa kiuchumi ni pamoja na kupitishwa kwa sheria na sera zinazounga mkono uwezeshaji wa wanawake kiuchumi na kufutwa kwa sheria za kibaguzi na mifumo ya kisheria.
Ulinzi na msaada kwa wanawake watetezi wa haki za binadamu, na uwajibikaji kwa ukiukwaji wa haki za binadamu unahitajika. Hili linahitaji kuweka kumbukumbu za ukiukwaji wa haki za wanawake, kukusanya takwimu zilizogawanywa katika masuala ya kingono, na kuendeleza ushirikiano kwa ajili ya programu za pamoja za utetezi.
Ni lazima kuandaa na kutekeleza taratibu za uwajibikaji ili kulinda haki za wanawake na kuhakikisha kuwa sauti za wanawake zinapazwa katika nafasi zote za kufanya maamuzi.