#PICHA:Mtoto wa mwaka mmoja anatibiwa utapiamlo katika Kituo cha Afya cha Abu Sunun nchini Sudan.
SUDAN: Zaidi ya visa 10,000 vya kipindupindu vyaripotiwa na visa 5,000 vya surua.
Nchini Sudan ambako kaimu mwakilishi wa shirika la afya Duniani, WHO nchini humo Peter Graaff, akizungumza mjini Cairo Misri hii leo kuhusu hali ya Sudan amesema miezi kumi ya vita imetumbukiza mamilioni ya watu katika janga lisiloelezeka la kibinadamu huku mapigano yakiendelea kusambaa katika maeneo mapya na kufurusha watu zaidi wengine mara kadhaa.
Bwana Graaff amesema ameshuhudia moja kwa moja kuhama kwa maelfu ya watu Sudan na wengine kukimbia Chad watu waliolazimika kukimbia makazi yao mara nyingi na walipata makazi katika maeneo yenye msongamano wa watu ambako kulikuwa na ukosefu wa huduma za msingi kama maji na vyoo, chakula, na huduma za afya.
Mamilioni wametawanywa na kukimbia
Amesema watu milioni 8 wametawanywa na kufanya mgogoro wa Sudan kuwa mkubwa zaidi wa watu kutawanywa duniani,wengi wakikosa huduma za msingi kama afya, chakula, afya na elimu na takriban watu milioni 25 wanahitaji msaada wa kibinadamu hivi sasa.
Ameongeza kuwa watu wengine milioni 18 kati yao walikuwa wanakabiliwa na njaa kali na milioni tano walikuwa katika viwango vya dharura vya njaa.
Pia kumekuwa na wasiwasi kwamba msimu ujao wa muambo utasababisha viwango vya janga la njaa katika maeneo yaliyoathiriwa zaidi.
Ugonjwa wa utapiamlo umekuwa na uhusiano wa pamoja kwani watu wenye utapiamlo, hasa wajawazito na watoto, walipata matokeo mabaya zaidi ya ugonjwa huo, watoto wenye utapiamlo walikuwa katika hatari kubwa ya kufa kutokana na magonjwa kama vile kuhara, nimonia, na surua, hasa katika mazingira ambayo walikosa huduma za afya za kuokoa maisha.
Afya Sudan ni zahma kubwa
Bwana Graaff amesisitiza kuwa hali nchini Sudan imekuwa dhoruba kamili kwani mfumo wa afya haufanyi kazi tena, na mpango wa chanjo ya watoto umekuwa ukisambaratika na magonjwa ya kuambukiza yanaenea.
Ameongeza kuwa zaidi ya visa 10,000 vya kipindupindu viliripotiwa, visa 5,000 vya surua, takriban visa 8,000 vya homa ya kidingapopo na zaidi ya visa milioni 1.2 vya ugonjwa wa malaria.
Hivyo amesisitiza kwa jumuiya ya kimataifa kutoipa kisogo Sudan na kusaidia kukabiliana na changamoto lukuki za kibinadamu.