Wagonjwa wa moyo kutoka Sierra Leone kutibiwa Tanzania
Ujumbe wa wataalamu wa Wizara ya Afya kutoka Sierra Leone, wameingia makubaliano na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), kwa ajili ya kutibu wagonjwa wanaotoka nchini humo.
Wataalamu hao walikuja nchini kwaajili ya kujifunza namna ya kuanzisha matibabu ya moyo nchini kwao huku wakishangaa uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali, Taasisi ya JKCI.
Akizungumza wakati wa kupokea ujumbe huo, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk. Peter Kisenge, amesema ziara hiyo inalenga kuendeleza ushirikiano wa matibabu ya moyo kati ya Tanzania na Sierra Leone ikiwa ni dhamira ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kutangaza utalii tiba kimataifa.
“Ujumbe huu umefika hapa nchini kujifunza uwekezaji wa matibabu ya moyo na usambazaji wa dawa na vifaa tiba kutoka kwa Bohari ya Dawa (MSD), ikiwa ni uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali ya Rais Dk. Samia,” amesema Dk. Kisenge.
Amesema ujumbe huo wa wataalamu kutoka Sierra Leone umekiri kujifunza mambo mengi kutoka JKCI na wataleta wagonjwa na wao kwenda kuanzisha taasisi yao kwa ushirikiano na taasisi ya JKCI.
Dk. Kisenge amesema wataalamu hao wa Sierra Leone, wamejifunza utendaji kazi mkubwa na imara kutoka kwa watumishi wa JKCI, ikiwamo namna ya kuhudumia wagonjwa mahututi.
Amesema kuwa ugeni huo ni hatua kubwa ambayo inatimiza malengo ya Rais Dk. Samia ya kukuza tiba utalii nchini kutokana na uwekezaji mkubwa alioufanya kwenye sekta ya afya.
Ameongeza kuwa, mbali na huduma za upasuaji wanazofanya hospitalini hapo, wanaendelea kutoa huduma za upimaji wa moyo kupitia mpango wao wa Dk. Samia, Tiba Mkoba.
Amesema mpango huo unasogeza huduma hizo karibu na wananchi huku wakizijengea uwezo hospitali zingine za kanda ikiwamo Benjamin Mkapa pia Chato na Geita.