Mloganzila; Fahamu haya kabla ya kurekebisha Maumbile.
Hospitali ya Mloganzila ilitangaza inaanza kutoa huduma hizo za upasuaji, ikiwamo kupunguza uzito na kuongeza makalio.
Akizungumza na Mwananchi, Daktari bingwa mbobezi wa upasuaji wa kurekebisha maumbile, Hospitali ya Muhimbili, Nadir Meghji anasema kabla ya kumfanyia mtu upasuaji, wanafanya vipimo vya awali kwa mhusika na kumpa ushauri ili kupata matokeo mzuri.
Anasema upasuaji wa kubadili maumbile sio wa siku moja, bali inachukua muda mrefu na inaweza kufika hata mwaka kutokana na vipimo vya awali walivyovifanya. “Tunamfanyia vipimo vya awali kuangalia kama uzito wake unaruhusu na endapo kutakuwa na kasoro tunatoa muda kwa mteja kufuata tulichomuelekeza,” anasema Dk Meghji.
Anasema si kila mtu anaweza kufanyiwa upasuaji wa kubadilisha maumbile kwa sababu wanakwenda wakiwa wazima, hivyo hawawezi kumfanyia kama dharura kwa sababu tu amejipanga kuboresha maumbile yake.
“Hili huwezi kumwambia mgonjwa (mhusika) aje haraka na kufanyiwa upasuaji baada ya siku tatu ya kuonana na daktari, bali anatakiwa kufuata utaratibu wa matibabu.
“Kitu cha msingi ni kuangalia hali ya mgonjwa (mhusika) kuhakikisha kama atakuwa salama na akifanyiwa upasuaji unaisha salama na kuleta matokeo mazuri,” anasema Dk Meghji.
Kuhusu matatizo kutokea kwa baadhi ya watu, anasema inawezekana hawahudhurii kliniki katika nchi walizofanyiwa upasuaji, hivyo kupata matokeo tofauti na matarajio yao.
“Kosa linalofanyika ni wagonjwa (wahusika waliofanyiwa upasuaji wa kubadili maumbile) kushindwa kurudi kuangaliwa maendeleo yao, utaratibu unajulikana, ukifanyiwa upasuaji unatakiwa kuhuduhuria kliniki hadi pale daktari atakapojiridhisha kuwa maendeleo ni mazuri na kuruhusu mgonjwa kuendelea na shughuli zake,” anasema Dk Meghji.
Anasema kutokana na uwezo wa watu inakuwa ngumu kurudi sehemu aliyofanyiwa upasuaji, hivyo kupata changamoto.
“Wale wote wanaopenda kufanyiwa upasuaji wa maumbile wakubali kufanyiwa nchini kwa ajili ya uangalizi wa karibu.”
Alipoulizwa na Mwananchi kuhusu upasuaji huo, mdau wa masuala ya afya, Dk Benjamin Elkana anasema kila kiungo kimeumbwa kwa makusudi, inapotokea kutengenezwa tena maana yake zinakwenda kusumbuliwa seli za kawaida za mwili.
Anasema seli zina tabia ya kuzaliwa na kufa, inapotokea zikaongezewa kitu kingine zinaondolewa sifa ya kufa na kubaki zikiongezeka, hivyo kuna uwezekano wa kupata maradhi yatakayosababisha saratani.
“Wanaobadili maumbile wanaweza kupata magonjwa ya kansa (saratani) na magonjwa yasiyokuwa na tiba kwa sababu wameweka vitu mahali siyo sahihi,” anasema Dk Elkana.
Anasema kwa sasa nchi zilizoendelea wanapambana na magonjwa makubwa yanayotokana na aina ya maisha wanayokwenda nayo katika jamii husika.
Mwanasaikolojia Ramadhani Massenga aliiambia Mwananchi kuwa, chanzo cha watu kubadilisha maumbile hutokana na jamii inayowazunguka.
Anasema wengi wao wamebadilisha maumbile kwa ajili ya kuwafurahisha watu fulani, wakiwamo wapenzi wao na maneno wanayotamkiwa na familia zao kupitia makosa waliyofanya.
“Wakati yanazungumzwa masuala ya afya ya akili, hili la kubadilisha maumbile limesahaulika, zaidi wanazungumzia mtu kujiua, matukio ya ubakaji ila tumesahau hili kwa watu mbao wamejikataa maumbile yao,” anasema Massenga.
“Ukichunguza zaidi unapata majibu kuwa huyo mtu hajikubali jinsi alivyo na kukubali maumbile ya mtu mwingine. Hii ni wazi kuwa hiyo ni afya ya akili.” Pia, anasema watu wamekuwa wagonjwa na wanahitaji kutibiwa, lakini imebadilishwa kwa kuita urembo wakati wanaharibu maumbile kutoka katika uhalisia wake.
Kwa mujibu wa Chama cha Madaktari Bingwa wa Upasuaji wa Plastiki Marekani, idadi ya watu wanaojihusisha na ubadilishaji wa maumbile ya kukuza au kupunguza makalio, matiti, nyusi, nywele, kubadili sura au ngozi, imeongezeka kutoka milioni 7.5 mwaka 2000 na kufikia watu milioni 14, 2011.
Uingereza pekee kati ya wanawake 20,000 hadi 30,000 hukuza matiti kila mwaka, biashara hiyo huiingiza pato la zaidi ya Dola150 milioni za Marekani (Sh240 bilioni) kwa mwaka.
Zipo nchi nyingi, mathalani Venezuela na Ufaransa, ambako ukuzaji makalio na matiti vimeshika kasi na kusababisha wananchi kuzipigia Serikali zao kelele ili zidhibiti vitendo hivyo.
Upasuaji wa maumbile
Oktoba 10, 2023 Hospitali ya Mloganzila ilitangaza kufanya huduma za kibingwa bobezi za upasuaji wa kupunguza uzito na rekebishi kuanzia Oktoba 27, 2023.
Upasuaji huo unahusisha kupunguza mafuta mwilini na kurekebisha maungo, ikiwamo kuongeza ukubwa wa matiti na makalio, kupunguza tumbo au nyama kwenye mikono na sehemu nyingine za mwili.
Hivi karibuni, Mkuu wa Idara ya Upasuaji, Dk Erick Muhumba alithibitisha hilo kwa kusema upasuaji unafanywa na wataalamu wa Mloganzila kwa kushirikiana daktari bingwa wa upasuaji kutoka India.
Licha ya kuwa ni matibabu, lakini huduma hiyo inaingia katika uchumi kwa sababu inaongeza kipato cha sehemu husika kwa kuwatoza watu gharama za upasuaji.
“Upasuaji utafanyika kwa bei nafuu ukilinganisha na mtu ambaye angeenda kutafuta huduma hizi nje ya nchi, hivyo tumeamua kuwasogezea wananchi huduma hizi na kuwapunguzia usumbufu wa kusafiri nje ya nchi kutafuta huduma hizi,” alisema Dk Muhumba.
Mbali na Mloganzila, hospitali nyingine zimekuwa zikishirikiana katika kubadilisha baadhi ya maumbile bure.
Hivi karibuni, daktari bingwa wa upasuaji na kiongozi wa timu ya Reconstructing Women International (RWI), Dk Andrea Pusic alisema wameweza kuhudumia mamia ya wanawake na wasichana waliojeruhiwa ili kuboresha utendaji wa kimwili na muonekano wao.
Naye daktari bingwa wa upasuaji Aga Khan, Dk Aidan Njau alisema changamoto iliyopo kwa watu hao ni kukosa kujiamini baada ya kupata matatizo. “Mtu anashindwa kujiamini hata kwenda sokoni, kanisani au msikitini hivyo msaada huo unawarudishia kujiamini,” alisema.
Mkuu wa upasuaji wa kurekebisha maumbile kutoka Muhimbili, Dk Edwin Mrema anasema wanufurahia zaidi pale wanaposaidia kurejesha tabasamu na hali ya kujiamini iliyopotea kwa wanawake na watoto.