Viongozi wa dunia pamoja na wawakilishi wa mashirika ya afya na makampuni ya dawa wamejumuika pamoja siku ya Alhamisi mjini Paris, Ufaransa katika mkutano wa kilele unaojadili masuala ya chanjo.
Katika mkutano huo, kumetangaza ufadhili wa dola bilioni 1.2 zitakazowezesha kuzalisha chanjo huko Afrika, bara ambalo linakabiliwa na matatizo mengi ya kiafya ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa magonjwa ya milipuko kama kipindupindu.
Mbali na viongozi wa Magharibi, mkutano huo umehudhuriwa pia na viongozi kutoka nchi kadhaa za Kiafrika kama Botswana, Rwanda, Senegal, Ghana, Mataifa mengine yamewakilishwa na mawaziri.
Katika hotuba ya ufunguzi wa mkutano huo, rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema kitendo cha kupiga jeki utengenezaji wa chanjo barani humo, itakuwa hatua muhimu kuelekea kuanzishwa kwa soko la kweli la chanjo Afrika.
Macron ameendelea kusema kuwa robo tatu ya fedha hizo zitafadhiliwa na mataifa ya Ulaya. Ujerumani itachangia dola bilioni 318 kama alivyoeleza Kansela Olaf Scholz katika ujumbe wa video. Ufaransa itatoa dola milioni 100, Uingereza dola milioni 60, huku wafadhili wengine wakiwa ni pamoja na Marekani, Canada, Norway, Japan na Wakfu wa Bill na Melinda Gates.
Kauli za viongozi mbalimbali wakiwemo wa Afrika
Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat aliuambia mkutano huo kwamba mpango huo unaweza kuwa kichocheo cha kukuza sekta ya dawa barani Afrika na kuimarisha ushirikiano kati ya nchi wanachama. Mahamat amesema Afrika huagiza nje ya bara hilo asilimia 99 ya chanjo zake na kwa gharama kubwa.
Janga la UVIKO-19 liliweka bayana hali ya kutokuwepo usawa katika usambazaji wa chanjo ulimwenguni, kwani nchi tajiri zenye makampuni mengi makubwa ya dawa zilijipatia dozi nyingi za chanjo na kuiacha Afrika ikiwa nyuma. Mpango huo mpya unalenga kuanzisha uzalishaji wa chanjo barani Afrika ili kuliwezesha bara hilo kuwa na uhuru zaidi na kuepusha kujirudia kwa hali iliyoshuhudiwa wakati wa janga la corona.
Waziri wa Mambo ya nje wa Uingereza David Cameron, aliuambia mkutano huo kwamba wakati kutakapotokea janga jingine, na hata kama viongozi katika nchi tajiri za Magharibi watakuwa na nia njema kama malaika, bado kutakuwepo shinikizo la kujihifadhia chanjo kwa ajili ya watu wetu, na kwamba hilo halitazuilika kila wakati.
Kuibuka tena kwa ugonjwa la kipindupindu hivi karibuni katika maeneo mengi ya Afrika, kumeonyesha hitaji la kuwepo wazalishaji zaidi wa chanjo ndani ya Afrika. Kwa sasa, ni kampuni moja tu duniani ya EuBiologics ya Korea Kusini ndio hutengeneza dozi za chanjo kwa bei nafuu ili kukabiliana ugonjwa huo hatari.
Macron amesema mlipuko wa kipindupindu kwa sasa unaathiri karibu nusu ya Afrika huku akitoa wito kwa kuufanya ugonjwa huo kutokomezwa kabisa. Alitangaza pia msururu wa uzalishaji wa chanjo za kipindupindu utakaozinduliwa barani Afrika na kampuni ya biopharmaceutical ya Afrika Kusini ya Biovac.
Muungano wa Gavi unaoyajumuisha mashirika mbalimbali yenye jukumu la kusaidia kusambaza chanjo za zaidi ya magonjwa 20 kwa nchi maskini , ulikuwa mmoja wa waandaaji wa Jukwaa hilo la Kimataifa kuhusu uhuru na ubunifu wa Chanjo. Katika kongamano hilo, muungano wa Gavi ulitangaza kuwa unalenga kukusanya dola bilioni 9 ili kufadhili programu zake za chanjo kuanzia mwaka 2026 hadi 2030.
Mwenyekiti wa Gavi Jose Manuel Barroso amesema kitendo cha kuwapa chanjo watoto milioni moja tangu mwaka 2000 ni mafanikio ya ajabu, na kwamba mtoto anayezaliwa zama hizi, anaweza kufikisha kwa urahisi miaka mitano kuliko hapo awali katika historia.
Hata hivyo, Barroso ameongeza kusema kuwa bado kuna mamilioni ya watoto ambao hawajapata chanjo dhidi ya ugonjwa wowote huku mamia ya mamilioni ya wengine wakihitaji kupatiwa chanjo zaidi.
Hadi sasa, asilimia mbili tu ya chanjo zinazotolewa barani Afrika ndizo hutengenezwa katika bara hilo. Umoja wa Afrika unalenga kuongeza idadi hiyo hadi kufikia asilimia 60 ifikapo mwaka 2040.
(Chanzo: AFP)