WATANZANIA wengi wana uzito uliopitiliza (mabonge) kutokana na kutozingatia ulaji unaofaa huku takwimu zikionyesha ni watu saba pekee nchini katika 100 wanaozingatia mlo kamili.
Takwimu Aidha, Mtanzania mmoja katika watatu, ana uzito uliokithiri na watu wenye elimu na uhakika wa kipato ndio waathirika zaidi.
Mkurugenzi Msaidizi wa Magonjwa Yasiyoambukiza (NCD) katika Wizara ya Afya, Dk. Omary Ubuguyu, ameyasema Dar es Salaam wakati wa kongamano la kwanza la uimara wa afya kwa ajili ya biashara endelevu, lililoandaliwa na Mtandao wa Global Compact Tanzania (GCNT) na kukutanisha wadau wa sekta binafsi.
“Katika maeneo machache ambayo tunafanya vizuri ni kwenye mazoezi kwa sababu kumekuwa kwa mfano na marathoni nyingi. Hatufanyi vizuri kabisa katika masuala ya ulaji bado ni watu saba katika 100 ambao wanazingatia ulaji unaofaa.
“Suala la uzito na unene kupita kiasi pia hali imezidi kuwa mbaya, zamani ilikuwa ni katika kila watu wanne, mmoja anauzito uliokithiri, sasa hivi ni mtu mmoja katika kila watu watatu ana uzito au unene uliokithiri, kwa hiyo hatufanyi vizuri katika eneo hili,” amesema.
Dk. Ubuguyu amesema idadi ya watu ambao wanatumia pombe nchini imepungua lakini matumizi yameongezeka.
“Bahati mbaya kuliko zote vijana wanaathirika zaidi kuliko rika linguine lolote na wanawake wanaathirika zaidi kuliko wanaume katika haya tunayoyazungumza. Watu wenye umri mdogo na wanawake ndio wako kwenye hatari zaidi,’ amesema.
Amesema utafiti unaonyesha kwamba magonjwa yasiyoambukiza kama saratani, kisukari, figo na shinikizo la juu la damu, yanaathiri zaidi watu wenye kipato cha chini, lakini ni kinyume chake katika baadhi ya nchi kama Tanzania ambako waathirika wakubwa ni wasomi na wenye uhakika wa kipato.
“Katika jamii mfano za wafanyakazi ndio wanaotumia vyakula vya viwandani zaidi, pombe zaidi, ndio watu wenye fursa ya kununua soda na vitu vingine ambavyo vinaathiri afya,” amesema.
Dk. Ubuguyu amesema wafanyakazi wanaathiri zaidi kutokana na mtindo wa maisha kwa kuwa hawana nafasi ya kupata chakula bora kwa kuwa wananunua vyakula wasivyojua namna vilivyoandaliwa na pia hawapati nafasi ya kufanya mazoezi.
“Kama taifa tuna mzigo mkubwa sana wa magonjwa yasiyoambukiza. Tukizungumzia gharama tunazozipata katika matibabu kwa mfano Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), vitu vikubwa vinavyouelemea ni kutibu magonjwa kama saratani, matatizo ya figo, shinikizo la juu la damu, kiharusi na kisukari. Hili ndilo janga kubwa katika taifa letu,” amesema.
Dk. Ubuguyu amesema serikali inapata matumaini inapoona jumuiya ya wafanyabishara na mashirika binafsi zikikutana na kujadili namna ya kukabili janga hilo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Global Compact Tanzania (GCNT), Mardha Macatta-Yambi, amezitaka kampuni binafsi na wawekezaji kuweka mazingira ya kuhakikisha afya za wafanyakazi ni nzuri, ili kukabili NCD.
Amesema wadau wote wanapawa kuunganisha nguvu kwa kuwa ongezeko la magonjwa hayo linaathiri biashara na uchumi wa nchi.
“Pamoja na serikali kuweka sera na mikakati ya kukabili magonjwa haya, makampuni yana nafasi kubwa kuhakikisha kwamba wafanyakazi wanakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu afya zao kwa kuwa hawa ndio nguvu kazi ya kuwatengenezea faida kwenye kile walichowekeza,” amesema.
Katika kongamano hilo, GCNT na taasisi ya ImpactAfya, wametia saini makubaliano ili kuendelea kutoa elimu ya uimara wa afya sehemu za kazi na kuwakumbusha wafanyakazi na umma kwa ujumla, umuhimu wa kuwa na afya njema ili kupunguza mzigo wa matibabu.
Amewataka Watanzania kuhakikisha wanafanya mazoezi kila siku, kula vyakula vyenye virutubisho, kupima afya mara kwa mara na kubadili mtindo wa maisha unaochochea NCDs.
Kongamano hilo liliongozwa na kaulimbiu ya kupunguza NCDs kwa ajili ya biashara endelevu na kuhudhuriwa na madaktari, wafamasia na wakurugenzi wa kampuni na taasisi binafsi.
Mlo kamili unaopaswa kuzingatiwa kila siku na aina yake kwenye mabano ni wanga (ugali, wali au ndizi), mboga (kabichi, spinachi, mchicha au figiri) protini (nyama, samaki, kunde, njegere na maharage), matunda (embe, chungwa, papai au tikiti), vitamini (karanga au korosho) na maji ya kutosha.