Virusi Vya Ukimwi (VVU) kwa mama Mjamzito
Kama wewe ni mwanamke unayeishi na virusi vya UKIMWI (VVU) haupaswi kukata tamaa juu ya wazo lako la kuwa mama au kuendelea kupata watoto. Kwa nchi ya Tanzania na duniano kote, kuna wanawake wengi sana wamefanikiwa kupata ujauzito na kujifungua salama wao pamoka na watoto wao bila kuwaambukiza kwa kufuata utaratibu wa kitabibu. Maendeleo katika matibabu ya HIV yamefikia hatua ambapo hii ni ndoto inayowezekana. Hatari ya kuzaa mtoto aliye na HIV sasa ni ndogo sana.
Kupanga Ujauzito:
Kama unafikiria kupata mtoto, ni muhimu kuzungumza na daktari wako au muhudumu wa Afya anayejihusisha na masuala ya Ukimwi/VVU aliye karibu nawe kuhusu nia yako. Ikiwa imethibitishwa ya kwamba muathirika wa VVU ana idadi finyu ya chembechembe za VVU mwilini, basi utumiaji wa ARV utazuia kuambukiza mtu ambaye hana VVU. Hii idadi ndogo ya chembechembe za VVU inapaswa kwanza kuthibitishwa kwa miezi kadhaa kabla ya kuamua kusitisha matumizi ya kondomu (condom).
Kuamua kupata ujauzito kwa kutumia njia ya kukutana kimwili ni jambo ambalo washirika wote wawili wanastahili kulijadili na kukubaliana. Daktari wako anaweza kukuelimisha uelewe lini unapoweza kupata ujauzito kulingana hasa na mzunguko wako wa hedhi na hali yako kiafya. Daktari atakushauri kuhusu mambo kama: –
Wakati bora wa kupata mimba, ikizingatiwa hali yako ya Ukimwi na mzunguko wako wa hedhi.
Chaguo salama zaidi kwa mwenzi wako ambaye hana HIV (kama vile kujikinga au kujihimilisha).
Jinsi ya kupunguza hatari ya kuambukiza mtoto wako virusi vya Ukimwi (VVU).
Matibabu salama ya Ukwimwi kwa wewe na mtoto wako (baadhi ya dawa sio salama wakati wa ujauzito).
Ujauzito Usiopangwa:
Kama ujapanga kupata ujauzito au umegundua una VVU wakati wa ujauzito, ni muhimu kuzungumza na daktari haraka iwezekanavyo. Kuna njia za kuzuia mtoto wako asiambukizwe VVU katika kila hatua ya ujauzito.
Kupunguza Hatari ya Kuambukiza Mtoto Wako na HIV: Kuna hatua nne zinazopendekezwa:
Kutumia matibabu ya HIV wakati wa ujauzito ili kupunguza idadi ya chembechembe za VVU katika damu (HIV Viral Load).
Kutonyonyesha.
Matibabu ya HIV kwa mtoto wako.
Kufikiria kujifungua kwa upasuaji.
Kujua Kama Mtoto Wako Ana HIV:
Kuna uwezekano mkubwa sana wa kujifungua mtoto asiye na maambukizi ya VVU. Lakini, ili kuthibitisha hali ya mtoto, mtoto wako atafanyiwa vipimo mara kwa mara kwa miezi sita ya kwanza ya maisha yake. Watoto wanaotambuliwa kutokuwa na VVU wanathibitishwa kipimo kwa kipimo mpaka wanapofikisha miezi 18. Hospitali: Hospitali zote nchini zina wahudumu wenye weledi kuhusu matunzo kabla ya kujifungua kwa wanawake wenye wanaoishi na VVU. Viwango vya uzoefu vinaweza kutofautiana kulingana na hospitali.
Msaada:
Ujauzito na kuwa mama kunaweza kuwa changamoto lakini pia ni furaha kubwa. Kupata msaada kutoka kwa familia, marafiki, au wafanyakazi wa msaada unaweza kusaidia sana. Unaweza pia kutaka kuongea na wanawake wengine wanaoishi na VVU kubadilishana uzoefu.
Credits:TanzMed
• Soma Pia hapa kuhusu Sababu za kupumzika wakati wa Ujauzito(BedRest)