Soma hapa Sababu za watoto kuwa na uzito mkubwa
Uzito sahihi wa mtoto wako unaotakiwa ni ule wa namba za umri wake ukazidisha mara mbili ukajumlisha na nane (yaani miaka 4×2+8= 16), zaidi ya hapo ni kiashiria cha uzito uliokithiri.
Imekuwa ni kawaida kwa wazazi wengi kufurahia hali ya watoto wao kuwa na uzito mkubwa, hata hivyo wataalamu wa afya wanasema ni uzito uliopitiliza au ni kiashiria cha homoni za mtoto kutokuwa sawa.
“Mtoto mwenye umri wa miaka minne anapaswa kuwa na uzito wa kilogramu 16 na mwenye umri wa miaka sita anapaswa kuwa na uzito wa kilogramu 22, hii haijalishi anaishi Ulaya au Tanzania, hii ndiyo kanuni ya afya,” alisema Mtaalamu wa Afya ya Jamii, Dk Ali Mzige.
Uzito wa kuzaliwa
Licha ya wale wanaonenepa kutokana na kutokuwa na mpangilio mzuri wa chakula, kuzaliwa na uzito mkubwa kupita kiasi (fetal macrosomia) au kile kinachojulikana kama uzito wa juu wa kuzaliwa ni hali ambayo mtoto anazaliwa na uzito wa kilogramu 4 au zaidi.
Daktari bingwa wa magonjwa ya watoto kutoka Idara ya Mafunzo na utafiti na magonjwa ya ndani Hospitali ya Kanda ya Rufaa Mbeya, Ernest Winchislaus anasema hali hiyo inaweza kuwa na athari kubwa kwa afya ya mtoto na mama na mara nyingi inahitaji ufuatiliaji wa karibu na matibabu.
Anataja sababu zinazochangia watoto kuzaliwa na uzito mkubwa ni pamoja na maumbile, mlo wakati wa ujauzito na hali ya kiafya ya mama.
“Hapa tunachunguza baadhi ya sababu na athari za watoto kuzaliwa na uzito mkubwa kupita kiasi. Tutaangalia ugonjwa wa kisukari cha mimba, wanawake wenye tatizo hilo wako katika hatari ya kumzaa mtoto mwenye uzito mkubwa,” anasema.
Dk Winchslaus anasema kisukari cha mimba husababisha kiwango kikubwa cha sukari katika damu ya mama, ambayo inaweza kusababisha ukuaji wa kichanga kuzidi kupita kawaida, wanawake wenye unene kupita kiasi au wenye uzito mkubwa kabla ya ujauzito wako katika hatari kubwa ya kumzaa mtoto mwenye uzito mkubwa.
“Hali hii inaweza kuhusishwa na tatizo katika kemikali ya kuchakata sukari mwilini ambayo inaweza kuchochea ukuaji wa kichanga kwa kiasi kikubwa,” anasema.
Maumbile
Dk Winchslaus anasema uzito wa mtoto unaweza kuathiriwa na mambo ya maumbile, ikiwa ni pamoja na jeni zinazohusiana na ukuaji wa kichanga.
Watoto ambao wazazi wao wana uzito mkubwa wanaweza kuwa na hatari kubwa ya kuzaliwa na uzito mkubwa.
“Baadhi ya matatizo ya kijenetikia katika mwili wa kichanga yanaweza pia kuchangia tatizo la uzito mkubwa, baadhi ya haya yanafahamika kitaalamu kama Beckwith-Wiedemann Syndrome, Sotos syndrome, Fragile x syndrome,” anasema.
Anataja historia ya watoto wenye uzito mkubwa katika mimba za awali, akisema tafiti zinaonyesha ikiwa hapo awali umeshazaa mtoto mwenye uzito mkubwa, una hatari kubwa ya kuzaa mtoto mwingine mwenye uzito mkubwa.
“Pia, ikiwa wewe mwenyewe ulizaliwa na uzito mkubwa zaidi ya kawaida, una uwezekano mkubwa zaidi wa kuzaa mtoto mwenye uzito mkubwa pamoja na kupitiliza kwa tarehe ya matazamio ya kujifungua,” anasema.
Dk Winchslaus anasema ikiwa ujauzito unazidi kwa zaidi ya wiki mbili baada ya tarehe ya kutarajia kujifungua, mtoto ana hatari kubwa ya kuzaliwa na uzito mkubwa, lakini pia huchangiwa na umri wa mama mjamzito.
Anasema wanawake wenye umri zaidi ya miaka 35 wana uwezekano mkubwa wa kupata watoto wenye uzito uliozidi.
Daktari bingwa wa watoto, Deashisaria Rimoy anasema mambo mengi yanaweza kusababisha mtoto kuzaliwa na uzito mkubwa au mtoto akazaliwa kawaida na kuendelea kukua katika uzito mkubwa zaidi.
“Kuna vinasaba, homoni, pia kuna uwezekano mtoto aliyezaliwa na uzito wa kawaida akaanza kuongezeka uzito, yanayochangiwa na kupangilia mlo, mtindo wa maisha, magonjwa, masuala ya kisaikolojia kama sonona wanakula sana na kunenepa, pia baadhi ya dawa hunenepesha,” anasema Dk Deashisaria.