Wataalamu wasema zinachangia kuongeza maumivu, waonya zaweza kusababisha uoni hafifu na upofu.
Wataalamu wa afya na madaktari bingwa wa macho wamesema wanapokea idadi kubwa ya wagonjwa wakiwa katika hali ya ugonjwa mkali, kutokana na matumizi ya njia mbadala kutibu macho, ikiwamo matumizi ya mkojo na chumvi.
Hali hiyo imebainika siku 15 tangu kutangazwa kuibuka ugonjwa huo ujulikanao viral keratoconjunctivitis (red eyes) Januari 13, 2024 mkoani Dar es Salaam.
Wataalamu waliozungumza na Mwananchi Digital jana Januari 28, 2024 wameeleza wagonjwa wanaotumia chumvi, mkojo, chai ya rangi na kitunguu saumu kama tiba, macho yao huvimba na kuuma zaidi pamoja na kupatwa homa. Athari hasi zaidi zinazotajwa ni kusababisha vidonda kwenye kioo cha jicho.
Tiba hizo mbadala zinaelezwa zinaweza kusababisha kovu kwenye jicho litakalomfanya mgonjwa apate uoni hafifu au kupoteze uwezo wa kuona kabisa.
Daktari bingwa na mkuu wa kitengo cha macho kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Sarah Mrema ameisema idadi ya wagonjwa wanaohudhuria hospitalini hapo kutibiwa macho imekuwa ikiongezeka na kupungua.
Amesema wamekuwa wakipokea wagonjwa wakiwa tayari walianza kutumia tiba za majani ya chai, vitunguu saumu na chai ya rangi.
“Si kwamba wanapona wakitumia tiba mbadala, maumivu yanazidi, wakija hapa wanakuwa na maumivu makali. Ukihoji anakwambia alitumia mkojo, chumvi na njia nyingine nyingi. Unampa dawa anatumia, kisha anapona,” amesema Dk Sarah.
Kwa mujibu wa Dk Sarah, takwimu za hospitali hiyo zinaonyesha tangu Desemba 22, 2023 wagonjwa 105 walifika kutibiwa na kuna siku orodha ya wagonjwa inapanda na siku nyingine inapungua.
Daktari bingwa wa macho katika Hospitali ya Muhimbili-Upanga, Neema Moshi amesema unapotumia vitu vikali kutibu macho, ni rahisi kuharibu kioo cha mbele cha jicho na maumivu yanayotokea huwa makali.
“Maji ya chumvi yanaweza kusababisha michubuko au kidonda kwenye kioo cha mbele cha jicho, hivyo kutengeneza kovu litakalopunguza uwezo wa jicho kuona au ulemavu wa kutoona wa kudumu,” amesema.
“Matumizi ya chai ya rangi katika kutibu macho yanaweza kusababisha vidonda kwenye kioo cha jicho na kusababisha kovu kwenye jicho litakalosababisha uoni hafifu