Kenya;Bingwa Marathon Kelvin Kiptum afariki kwa kujeruhiwa kichwani
Uchunguzi wa maiti umebaini kuwa bingwa wa rekodi ya dunia ya mbio za marathon nchini Kenya Kelvin Kiptum alifariki kutokana na majeraha mabaya kichwani katika ajali ya barabarani mapema mwezi huu.
Mwanapatholojia mkuu wa serikali ya Kenya Johanssen Odor aliambia vyombo vya habari kuwa majeraha hayo yalikuwa sawa na yale wanayopata watu katika ajali za barabarani.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 na kocha wake Mnyarwanda Gervais Hakizimana walifariki katika ajali iliyotokea usiku wa kuamkia tarehe 11 Februari karibu na nyumbani kwake kaskazini-magharibi mwa Kenya.
Mazishi ya Hakizimana yamefanyika nchini Rwanda.
Kiptum atazikwa Ijumaa katika kijiji cha nyumbani kwake, Chepkorio katika Kaunti ya Elgeyo-Marakwet, kwenye hafla inayotarajiwa kuwa ya kiserikali.
Kiptum alipata umaarufu mwaka jana aliposhinda mbio za marathon za Chicago na kuweka rekodi mpya ya dunia ya saa 2:00:35.
Alishinda rekodi ya awali iliyokuwa ikishikiliwa na Eliud Kipchoge kwa sekunde 34 – na kumfanya Kiptum kuwa mpinzani mkuu wa Kipchoge msimu wa 2024.
Wawili hao walikuwa wametajwa katika timu ya Kenya ya mbio za marathon kwa ajili ya Michezo ya Olimpiki ya Paris baadaye mwaka huu.
Timu yake ilikuwa imetangaza kwamba Kiptum angejaribu kukimbia umbali wa kilomita 42 chini ya saa mbili katika mbio za Rotterdam marathon – hatua ambayo haijawahi kufikiwa katika mashindano ya wazi.