Zaidi ya watu 45 wamefariki dunia nchini Kenya baada ya bwawa kupasua kingo zake kufuatia mvua kubwa na mafuriko, maafisa wamesema.
Watu katika vijiji karibu na Mai Mahiu, yapata kilomita 60 kutoka mji mkuu, Nairobi, walisombwa na maji walipokuwa wamelala.
Zaidi ya watu 100 wameuawa katika mafuriko ambayo yameharibu sehemu za Kenya katika mwezi uliopita.
Vikosi vya waokoaji vinachimba matope kusaka manusura katika vijiji kadhaa, vikiwemo Kamuchiri na Kianugu kaunti ya Nakuru.
Maelezo ya video,Makumi ya watu wamepoteza maisha baada ya bwawa kuvunja kingo zake nchini Kenya
Kati ya miili 42 iliyopatikana mapema wasubuhi 17 ilikuwa ya watoto, kamanda wa polisi Stephen Kirui alisema, akinukuliwa na shirika la habari la Reuters.
“Maji yalikuja kwa kasi kutoka Bwawa la Old Kijabe na kusomba nyumba na magari mengi. Hatujawahi kuona mafuriko makubwa kama haya tangu tulipozaliwa hapa Mai Mahiu,” David Kamau aliiambia BBC.
Mkazi mwingine, Peter Muhoho, alisema kuwa wengi wa majirani zake walisombwa na maji katika kijiji cha Kianugu chenye takriban nyumba 18.
“Nilikuwa nimelala niliposikia kishindo kikubwa na mayowe. Maji yalikuwa yamefurika eneo hilo. Tulianza kuokoa watu,” Bw Muhoho aliambia BBC.
Akionyesha begi alilokuwa ameshikilia, Bw Muhoho aliongeza: “Mkoba huu ni wa mtoto niliyemfahamu. Alisombwa na maji. Niliupata [mfuko huo] chini ya mkondo.”
Serikali imeahirisha kufunguliwa kwa shule kote nchini Kenya huku mvua zaidi ikitarajiwa kunyesha, kulingana na idara ya utabiri wa hali ya anga .
Zaidi ya watu 130,000 wamekimbia makazi yao kutokana na mafuriko hayo, huku watu wengi wakipata hifadhi shuleni.
Mvua kubwa pia imenyesha katika nchi jirani za Tanzania na Burundi.
Takriban watu 155 wameuawa nchini Tanzania tangu Januari.
Nchini Burundi, karibu watu 100,000 wamekimbia makazi yao.
Idadi ya waliopoteza maisha haijulikani, lakini tovuti inayohusishwa na Umoja wa Mataifa inaripoti kuwa watu 68 waliuawa katika mji mkuu, Bujumbura, tarehe 10 Februari pekee baada ya mvua kubwa kuharibu nyumba 3,500.
Mwandishi wa BBC anayeshughulikia utabiri wa hali ya hewa Chris Fawkes anasema kuwa mojawapo ya vichochezi vikubwa vya mvua ni Dipole ya Bahari ya Hindi (IOD).
IOD – ambayo mara nyingi huitwa “Indian Niño” kwa sababu ya kufanana kwake na sehemu yake ya Pasifiki – inaelezea tofauti ya halijoto ya uso wa bahari katika sehemu tofauti za Bahari ya Hindi.
Wakati wa awamu chanya, maji katika Bahari ya Hindi magharibi yana joto zaidi kuliko kawaida na hii inaweza kuleta mvua kubwa bila kujali El Niño.
Hata hivyo, wakati wote IOD chanya na El Niño hutokea kwa wakati mmoja, kama ilivyokuwa mwaka jana, mvua katika Afrika Mashariki inaweza kuwa kali.
Mojawapo ya mifumo chanya ya IOD kwenye rekodi ililingana na mojawapo ya mifumo thabiti zaidi ya El Niño mwaka wa 1997 na 1998, huku mafuriko makubwa yakiripotiwa. Haya yalisababisha vifo zaidi ya 6,000 katika nchi tano katika eneo hilo.
Mada: Via BBC