Mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994;Waliuawa wote nikabaki peke yangu: Nathalie Uwamaliya
Nathalie Uwamaliya, manusura wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994, akizungumza na Afisa Habari wa Umoja wa Mataifa kwenye mji mkuu wa Rwanda, Kigali.
Leo ni siku ya kimataifa ya kumbukumbu ya Mauaji ya Kimbari ya 1994 dhidi ya Watutsi nchini Rwanda ambapo mwaka huu ni miaka 30 tangu kutokea kwa mauaji hayo yaliyokatili Maisha ya watu milioni 1 wengi wakiwa ni Watutsi na watuhutu wenye msimamo wa wastan na wengine waliopiga mauaji hayo.
Kutana na Nathalie Uwamaliya mmoja wa mamilioni ya manusura wa mauaji hayo ambapo wakati yanatokea 1994 alikuwa na umri wa miaka 10 tu.
Akizungumza na afisa habari wa ofisi ya mratibu mkazi wa ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Rwanda Eugene Uwimana Nathalie ambaye kwa sasa anaishi mjini Kigali na familia yake ya watu watano inayojumuisha mumewe na watoto watatu anakumbuka kilichojiri “Nilikuwa na umri wa miaka 10 na nilikuwa ninaishi Kwenye familia ya watu 7 mjini Kigali na tulikuwa na furaraha. Wote walikufa na mimi pekeyangu ndiye niliyenusurika.”
Sasa ni miaka 30 imepita ana jihisi vipi?
Nathalie anasema “Baada ya miaka 30 tangu mauaji hayo kwanza ninahisi hisia za shukrani kwa sababu kuna watu wengi walipoteza Maisha yao katika janga hilo nami nkanusurika. Lakini siku zote kuna jeraha na machungu ndani ya moyo ambavyo vinahitaji mchakato wa kupona.”
Ameendelea kusema kwamba “Bado tuna safari ndefu ya kujijenga upya na kuboresha Maisha yetu na kupigania mabadiliko yetu. Hata hivyo nnatambua jitihada kubwa zilizofanyika katika kuleta maridhiano na umoja ili kufikia lengo la kuhakikisha asilani mauaji hayo ya kimbari hayatotokea tena.”
Ubaguzi wa rangi au wa kikabila umetumika kupandikiza woga au chuki dhidi ya wengine, jambo ambalo mara nyingi husababisha migogoro na vita, kama ilivyokuwa katika mauaji ya kimbari ya Rwanda mwaka 1994.
Dunia bado iko kwenye machafuko ikishuhudia mauaji katika maeneo mbalimbali duniani, je, hilo linakutia wasiwasi?
“Kwa hakika hilo linatia hofu kubwa anasema Nathalie akiongeza kuwa “Nikisikia kuwa kuna mauaji yanaendelea sehemu mbalimbali duniani ina mana kwamba watu wanaendelea kupoteza maisha yao. Kila mtu ana haki ya kuishi na kuishi kwa Amani na usalama. Na nadhani hakuna mtu anayechagua kuishi kwa hofu.”
Kwa mujibu wa Nathalie endapo kuna mauaji yanaendelea “Zinahitajika hatua za haraka na inaonyesha dunian haijayapa kisogo mauaji ya kimbari kwa sababu mpaka leo hii bado tunasikia kuhusu mauaji katika maeneo mbalimbali na yanayokana na ukabila, rangi, dini au lugha, tukio ambalo liliacha kovu baya sana, katika jamii kwa ujumla kwa familia na kwa watu binafsi.”
Pia amesema mauaji hayo ya kimbari yaliacha “Athari kubwa sana kwa manusura na baadhi ya athari hizo zinaonekana na nyingine hazionekani.”
Je, unadhani dunia imeliacha jinamizi la mauaji yakimbari na kusonga mbele?
Akijibu swali hilo Nathalie amesema “Mauaji ya kimbari yanapaswa kuwa jinamizi na sio tukio halisi linalopaswa kutokea.”