Fanya haya ikiwa mtoto wako amepata Degedege na mwili unakakamaa sana.
Ukuaji wa kila mtoto unatofautiana haijalishi ni wangapi umelea au uliobarikiwa nao kama mzazi.
Kila mtoto hukua kivyake na hakuna vile unavyoweza kusema kwamba aliyetangulia nilimfanyia hivi na naye huyu nitamfanyia vivyo hivyo.
Katika makala hii, tunaangazia moja ya hali ambazo zinaweza kuwa changamoto kwa mzazi wakati inapomkumba mtu wako lakini hasa kwa watoto.
Hali hii inafahamika kama degedege ambayo humfanya mtu kuanza kutetemeka mwili, kupoteza fahamu, au hata mdomo na macho kuanza kucheza cheza.
Tunachanganua hii ni hali gani? chanzo chake na tiba ya kwanza kwa mgonjwa tukiwa na daktari wa watoto na mwananurolojia yaani mtaalam wa neva Dkt. Yusuf Jamnagerwalla kutoka Tanzania.
Mara nyingi watu huchanganya degedege na kifafa lakini kulingana na daktari Jamnagerwalla ni hali mbili tofauti kama anavyosema.
“Degedege haifanani na kifafa, hapana, hiyo si kweli. Degedege zote sio kifafa lakini kifafa ni ugonjwa wa degedege”.
Anachomaanisha daktari Jamnagerwalla ni kwamba unaweza kupata degedege sababu isiwe eti ni ugonjwa wa kifafa, hapana, badala yake ikawa ni kwa sababu nyingine kwa mfano kama umepungukiwa glukosi kwenye mwili, pengine shida ya madini fulani, kama ini au figo imefeli, kama una kiharusi na sio lazima degedege hizo zitageuka na kuwa kifafa.
Visababishi vya degedege kwa watoto
• Kuwa na joto la kiwango cha juu (zaidi ya selsiasi 38)
• Pengine kama mtoto aliumia ubongo wakati akiwa bado tumboni
• Au kama alikosa oksijeni wakati mama anajifungua. Na hali hii inaweza baadaye kugeuka na kuwa kifafa
• Akipata maambukizi yakaingia kwenye ubongo, mfano, kupata ajali.
Dalili jumla za degedege
Unaweza kumuona mtoto ametoa jicho anaangalia juu tu, au ukaona shingo yake ni kama inageuka isivyo kawaida, inapinde vile;
– Mtoto anaweza kukakamaa kabisa au akageuka tu upande mmoja na akasalia hivyo
– Mtoto anaweza kupoteza fahamu kabisa
– Mtoto kuwa na hisia za kupitiliza kama kucheza au kulia sana, furaha isiyo ya kawaida, hofu au hata uwoga
– Mtu anaweza kuanza kuzungumza mambo yasiyoeleweka hata ukahisi kama akili yake imeanza kuwa na matatizo
– Kuchezesha macho, kutoa nyute, mate au hata povu
– Misuli kukakamaa, inaishiwa na nguvu na kupelekea kuanguka
Lakini pia anaweza kutokewa na dalili zingine;
Daktari Jamnagerwalla anasema asilimia kubwa ya watoto kuanzia umri wa miezi 5 hadi miaka 5 au 6. Wanapata degedege ya homa kali.
Na wakati joto linaongezeka kwa kasi mwilini, kuna uwezekano mkubwa mtoto akapata degedege, lakini pia huwezi kuhitimisha kwamba moja kwa moja mtoto atapata kifafa.
Daktari anafafanua kuwa: “Degedege inaweza kuwa kiwango fulani cha kifafa ikiwa tu degedege inajirudia zaidi ya mara mbili ndani ya saa 24”.
Aina nne kuu za degedege kwa watoto
Mtoto anaweza kupiga kelele na kuanza kulia na ghafla akaanza kuchezesha macho au yakaenda juu, kisha ataanza kukakamaa na kutetemeka viungo vyote vya mwili na wakati huo akapoteza fahamu kabisa.
Mara nyingi hali hii inatokea kwa dakika mbili au tatu na inapozidi dakika 5, hiyo inakuwa ni hatari kwa maisha ya mtoto. Aina hii ya degedege kwa kiingereza inajulikana kama ‘Generalized tonic-clonic seizure’.
Aina ya pili, sehemu ya nusu ya mwili wa mgonjwa aidha itakakamaa au itacheza cheza. Kwa kiingereza inajulikana kama focal seizure. Katika aina hii ya degedege, sio lazima mtu apoteze fahamu.
Aina ya tatu ya degedege, unakuta mtoto au mtu mzima ghafla anatulia, yaani kama akili inasimama kidogo. Pengine kwa sekundę 20 au 30. Daktari Jamnagerwalla anasema ‘’Mwalimu anaweza kusema mtoto hana makini darasani lakini ukweli ni kwamba kipindi hicho huwa amepoteza fahamu na hatambui kilichotokea.” Aina hii ya degedege inafahamika kama absence seizure.
Atonic seizure ni aina nyingine ambapo ghafla misuli hulegea na mtu anadondoka. Hii inasemekana kuwa hatari sana kwa watoto kwa sababu akianguka anaweza kuumia kwenye ubongo au hata kupata majeraha kutokana na vitu vilivyokaribu naye.
Hadi kufikia hapo, ni dhahiri kwamba degedege ni hali ambayo inaweza kumtokea mtoto ama mtu yeyote.
Kama mzazi, unaweza kushtuka usijue la kufanya hasa ikiwa ni mara yako ya kwanza kuona hali ya mtoto ikibadilika kwa namna hii.
BBC imezungumza na mzazi ambaye hakutaka kutajwa jina lake, na tumempa jina Maya, watoto wake wawili wametokewa na hali hii.
‘’Hakika hali hii inapotekea huwa inatisha. Sio jambo rahisi kwa anayelishuhudia na huwezi kusema kwamba sababu uliwahi kuiona siku nyingine, basi leo utakuwa umezoea, moja kwa moja linalokujia akilini kama mzazi, unaanza kuona ni kama unaweza kumpoteza mtoto ndani ya sekundę chache sana.”
Huduma ya kwanza kwa mtoto
Dkt. Yusuf Jamnagerwalla daktari wa watoto na mwananurolojia kutoka Tanzania
Mara nyingi wazazi huwa wanashtuka. Lakini Daktari Jamnagerwalla anasihi walio na mtoto kipindi hicho, wasishtuke au kuanza kukimbia huku na kule, badala yake kukaa karibu na mgonjwa.
Fuatilia muda wa degedege unapoanza, na iwapo hali itazidi dakika tano unatakiwa kumkimbiza mtoto hospitalini.
‘’Degedege mbaya ni ile ya kukakamaa na kupoteza fahamu kwa mwili mzima, na ikipita muda wa dakika tano mpeleke mtoto katika kituo cha hospitali kilicho karibu na wewe wala sio kituo ulichozoea.
‘’Pia ni muhimu kumkinga mgonjwa akiwa katika hali hii asipate majeraha. Mfano, kunaweza kuwa na vitu vya ncha kali, visongeshe mbali vitu hivyo kwani vinaweza kumdhuru, anasema daktari Jamnagerwalla.
‘’Legeza kitu chochote kilichozunguka kwenye shingo yake, mfano, tai au kitambaa.
‘’Usiweke kitu chochote mdomoni. Sijawani kuona mtoto yoyote akikatika ulimialiye kwenye hali hii,” anasema daktari.
‘’Pia uzimzuie mtoto asikakamae. Hii ni makosa
‘’Na mgeuze mtoto upande mara tu unapoona degedege inakaribia kuisha.”
Ni wakati gani muafaka wa kumuona daktari?
Unachostahili kufanya ni kumkimbiza mgonjwa kwa daktari haraka iwezekanavyo, punde tu anapopata degedege kwa mara ya kwanza hata kama itakuwa ni kwa sekundę chache.
Pia hata kama itakuwa sio mara ya kwanza, lakini hali hii inapozidi dakika 5. Ni muhimu kumuona daktari kwa sababu inaweza kuwa hatari zaidi kwa mtoto.
Unapofika hospitali, kunakuwa na fursa kupata matibabu ya kwanza ya kusitisha degedege na kufanyiwa uchunguzi kubaini hasa kiini cha hali hiyo na kupata matibabu.
Imani potofu
1. Kurogwa
Kulingana na daktari Yusuf Jamnagerwalla idadi kubwa ya wazazi au waangalizi wa watoto huwa wanapata mshtuko mtu akiwa katika hali hii. Kuna wale ambao moja kwa moja hufikiri kwamba mtoto amerogwa.
Daktari anasema: ‘’Tuna shtuka kwa sababu tuna imani potofu. Tunaogopa mtoto amepata mashetani, au shida fulani au amerogwa”. Ukiwa na dhana hii unaweza kushindwa kutoa huduma ya kwanza kwa mtoto.
2. Mgonjwa atakula ulimi wake
Hii inatokana na dhana kwamba mtoto atang’ata ulimi.
Daktari anasema kamwe hili haliwezi kufanyika. ‘’ Ndio ataumia ulimi lakini sio kwamba utakatika. Kwahivyo, unapoweka vitu kama vile peni na kijiko, ulimi utarudi nyuma na hivyobasi, unaendelea kuziba mfumo wa kupitisha hewa kwenye mwili wake. Hii inamaanisha kuwa unahatarisha maisha ya mgonjwa zaidi hata kuliko ile degedege”.
3. Unapaswa kumzuia mgonjwa kukakamaa
Kamwe usimshike mtu au mtoto wakati anapitia hali hii kwa nia ya kumzuia kukakamaa. Kumshikilia kunaweza kusababisha jeraha la mfupa au misuli. Badala yake, hakikisha eneo linalozunguka halina vitu vinavyoweza kumdhuru.
4. Wakati wa kukakamaa, mtu huwa kwenye maumivu
Ukweli ni kwamba wakati wa degedege, mtu hana fahamu na hapati maumivu yoyote. Hata hivyo, watu wengine wanaweza kuwa na maumivu ya misuli na kupata uchovu baadaye.
5. Wenye degedege ni wagonjwa wa akili
Huo sio ukweli, haimaanishi kuwa mwenye degedege ana ugonjwa wa akili. Wanaakili timamu kabisa kama mtu mwingine yeyote.
6. Walio na degedege, wana kifafa
Hizi ni hali mbili tofauti. Degedege inaweza kuwa inatokana na chanzo tofauti kabisa wala sio kifafa.
7. Degedege ni ugonjwa wa kuambukiza
Hilo halina ukweli wowote. Unaweza kumtokea mtu yeyote, wakati wowote kulingana na visababishi tofauti.
Mada:Via Bbc