Fahamu hapa,Masharti mapya ya kukabiliana na kipindupindu pamoja na ‘red eyes’
Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Tumaini Nagu amezitaka nyumba za ibada kusitisha utaratibu wa waumini wake kushikana mikono, ikiwa ni sehemu ya kupambana na magonjwa ya mlipuko ya viral keratoconjunctivitis (red eyes) na kipindupindu.
Profesa Nagu alisema hayo jana, wakati akiongoza kikao cha 10 cha Bodi ya Ushauri wa Hospitali Binafsi.
Pia, alitoa rai ya matumizi ya majisafi tiririka na sabuni maeneo ya mikusanyiko, ofisi za umma na binafsi, nyumbani na sehemu za biashara, huku akiwahimiza wanaotumia vyombo vya usafiri kutumia vitakasa mikono.
Profesa Nagu alisema hayo baada ya kuwapo ongezeko la wagonjwa wa macho unaoambukizwa kwa kushikana mikono, kugusa sehemu aliyogusa mwenye maambukizo ambalo kwa sasa imefikia mikoa 17 na ugonjwa wa kipindupindu umesambaa katika mikoa 14.
“Muhimu kuzingatia usafi wa mtu binafsi na mazingira, tuepuke kushikana mikono, hasa katika nyumba za ibada sitisheni huu utaratibu kwa muda,” alisema Profesa Nagu.
“Maeneo ya mikusanyiko tusishikane mikono, wekeni miundombinu ya kunawa maji tiririka na sabuni, agizo hili ni kwa watu wote wa majumbani, sehemu za biashara, kwenye mikusanyiko, ofisi za umma na binafsi.”
Januari 29, Wizara ya Afya ilisema jumla ya mikoa 17 imeathirika na ugonjwa wa macho mekundu.
Akitoa taarifa hiyo, Mkurugenzi wa Tiba Wizara ya Afya, Profesa Paschal Rugajjo alisema hadi kufikia Januari 26 mwaka huu, idadi ya waliofika kwenye vituo vya afya walikuwa 5,359 kutoka 1,109, Januari 19.
“Ugonjwa huu umesambaa zaidi, ingawa ni wachache ndio wanafika vituo vya huduma za afya, mpaka sasa ugonjwa huu umesambaa na kuongezeka katika mikoa 17, ikiwamo ya Singida, Katavi, Kilimanjaro, Mara, Iringa, Njombe, Ruvuma, Simiyu, Mtwara, Lindi, Songwe, Rukwa na Mwanza,” alisema Profesa Rugajjo.
Akizungumza jana, Profesa Nagu alisema Serikali imechukua hatua nyingi, ikiwamo kuhakikisha kuna upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo yote yaliyoathirika na kushughulikia miundombinu ya majitaka ili kuhakikisha inakuwa vizuri.
“Kwa sababu ya mvua, miundombinu mingine ya maji taka inafunikwa, hivyo jitihada kubwa zimefanyika kuhakikisha inafukuliwa na timu ya wataalamu wa elimu ya afya kwa jamii wapo maeneo yote wakihimiza usafi wa mtu binafsi na mazingira,” alisema Profesa Nagu.
Alisisitiza watumiaji wa usafiri wa vyombo vya moto vya kuchangia, kutembea na vitakasa mikono, huku akihamasisha unywaji wa majisafi na salama pamoja na kuosha matunda na mbogamboga kuepuka maambukizi.
Profesa Nagu alisema mlipuko wa magonjwa hayo umetokana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuwa kuna mvua zilizozidi kiwango, miundombinu imebadilika na kutokea kwa milipuko ya magonjwa duniani kote.
Alisema kipindupindu si Tanzania pekee, bali kimeathiri nchi kadhaa, ikiwamo Zambia ambayo mpaka sasa shule zimeshindwa kufunguliwa.
“Baadhi ya mikoa tumefanikiwa kudhibiti ugonjwa huu, lakini bado tunapambana katika mikoa michache ya Mwanza, Katavi na Kagera, hatua zinapaswa kuchukuliwa na wananchi wenyewe kwa kujikinga, mvua bado zinakuja,” alisema.
Imani potofu
Chanzo cha kusambaa kwa kipindupindu wilayani Sengerema Mkoa wa Mwanza hadi kufika watu 61, imeelezwa ni kutokana na kuwepo kwa imani potofu kwa jamii kuwa wakitumia dawa za kienyeji kujikinga zitasaidia kupona ugonjwa huo.
Sakata hilo liliibuka jana, kwenye kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Sengerema, kilichokuwa kikijadili na kupitisha rasimu ya bajeti ya mwaka 2024/25.
Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Binuru Shekidele alisema timu ya wataalamu wa afya ilikwenda maeneo yaliyoathirika kwa ajili ya kutoa huduma za afya na kujikinga na baadaye ilibaini wananchi wakitumia njia isiyo sahihi kujitibu na kujikinga.
“Kusambaa kwa ugonjwa huu, kumetokana na imani potofu kwa wananchi kutumia dawa za kienyeji za kuvaa kiunoni na kushindwa kufuata kanuni za afya, wakisema zitawasaidia,” aliseme Shikidele.
Tangu kuibuka kwa kipindupindu, Wilaya ya Sengerema wameripotiwa wagonjwa 61 kutoka Januari 30 hadi Februari 2, mwaka huu.
Kati yao, 27 wamepona na kuruhusiwa, huku 34 wakiendelea kulazwa kwa matibabu kwenye vituo vya afya wilayani humo.
Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Senyi Ngaga amepiga marufuku uuzwaji wa vyakula holela shuleni, sambamba na mikusanyiko kwenye misiba.
Ugonjwa huo kwa sasa unasambaa kwa kasi kwenye maeneo yaliyopo pembezoni mwa Ziwa Victoria, yakiwamo ya Chifunfu, Kijiji cha Kiweni, Kata ya Kasenyi, Kijiji cha Lugongo na Mbalagane na Kata ya Katunguru.
Kisababishi kingine kilichotajwa ni wakazi wa mwambao wa ziwa kujisaidia hovyo.
Mmoja wa wananchi wa Kata ya Kasenyi, Anastazia John alisema ni kweli jamii ya wananchi wa kandokando mwa Ziwa Victoria wanaamini dawa za kienyeji zinatibu kuzuia magonjwa mbalimbali kuliko dawa zinazopatikana kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.
“Elimu inahitajika kwa jamii kuachana na imani potofu na kufuata kanuni za afya ili kuepuka kupata magonjwa ya mlipuko,” alisema Annastazia.
Baadhi ya madiwani waliwaomba wataalamu wa afya kuweka nguvu kwenye maeneo yaliyoathirika na ugonjwa huo.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Thomas Rutachunzibwa yuko Sengerema na timu ya afya ya mkoa, wakishirikiana na ya wilaya hiyo katika kata zilizoathirika.
Alipoulizwa hali ya kipindupindu mkoani Mwanza, Mratibu Elimu ya Afya wa Mkoa huo, Renard Mlyakado bila kutaja takwimu za mkoa mzima, alisema ugonjwa huo bado upo, akiwataka wananchi waendelee kuchukua tahadhari.
Aliwaomba wananchi kuacha utaratibu wa kusalimiana kwa kushikana mikono ili kuepuka kula bakteria, akidai hawawezi kujua wanaoshikana nao kama wana bakteria mikononi au la.
“Muhimu ni usafi wa mazingira na vyoo bora. Hata kama mtu ana choo cha shimo basi ahakikishe anakifunika ili inzi asitoe bakteria kwenye kinyesi na kusambaza kwa wakazi husika,” alisema Mlyakado.