Wanaume wenye Vipara wakimbilia Muhimbili
Daktari Bingwa wa Upasuaji Rekebishi na Upasuaji Urembo, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Dk. Edwin Mrema, amesema kuwa Wataalamu wanafanya upasuaji kwa wagonjwa 12 hadi 15 kwa wiki , huku idadi kubwa ya wanaohitaji huduma ya Upasuaji rekebishi ikiwa ni wanaume wenye kipara.
Huduma zinazofanywa mara kwa mara ni pamoja na upasuaji rekebishi kwa majeruhi wa ajali za viwandani, barabarani, matukio ya moto; kukiwa na wastani wa wagonjwa sita hadi wanane kwa siku.
Dk. Mrema pia amesema mpaka sasa nchi ina wataalamu 10 ,waliobobea katika upasuaji rekebishi na upasuaji wa urembo.
Upasuaji wa urembo kuotesha nywele kwenye kipara wafanyika muhimbili
Watalaam wa upasuaji Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa kushirikiana na wenzao kutoka nchini Marekani wamekamilisha kambi maalum ya siku tano iliyohusisha upasuaji wa urembo na upasuaji wa matibabu (Cosmetic and Reconstructive Surgery) kwa wagonjwa nane.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha kambi hiyo na kwa niaba ya timu nzima iliyoshiriki, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa MNH, Dkt. Ibrahim Mkoma, amesema upasuaji uliofanyika ni wa matibabu kwa wagonjwa waliokuwa na changamoto mbalimbali ikiwemo waliopata ajali ya kuungua moto na wenye misuli iliyokakamaa kutokana na majeraha n.k.
Amesema, kuna mtoto ambaye kichwa chake kilizaliwa kikiwa na vinundu vidogo vidogo mithili ya visunzua (skin tag) ambavyo viliondolewa na kufanya sehemu kubwa ya kichwa chake kuwa na kipara, hivyo amefanyiwa upasuaji wa kuwekewa puto (tissue expander) kwenye kichwa sehemu yenye nywele karibu na kipara ili ngozi ya eneo hilo iweze kuongezeka na kukuza nywele ambazo baada ya mwezi mmoja zitakuwa zimeota sehemu kubwa na kuruhusu kufanyiwa upasuaji wa kuvuta ngozi hiyo ikiwa na nywele na kufunika sehemu yenye kipara hivyo kumwezesha mtoto huyo kurudi katika hali yake ya kawaida.
Upasuaji huo umefanyika kwa kushirikiana na Watalaam wa Upasuaji kutoka Shirika lisilo la Kiserikali la Marekani ReSurge International ambao wana uzoefu mkubwa duniani katika kujenga uwezo wa kufanya upasuaji wa matibabu na urembo.