Uhaba wa vifaa wachochea ongezeko la vifo vya watoto Kenya
Uhaba wa vifaa vya msingi, maambukizi na ukosefu wa wataalam wa afya vimetajwa kuwa chanzo kikuu cha ongezeko la vifo vya watoto wachanga kati ya mwaka 2017 hadi 2022 nchini Kenya .
Ripoti mpya ya mkaguzi mkuu wa serikali imebaini kuwa Chanzo kikuu cha maafa ya watoto ni kuzaliwa kabla kutimiza siku zao, maambukizi, kukosa hewa ya Oxygen na damu kwenye ubongo.
Asilimia 60 ya hospitali hizo hazina vifaa vya msingi vya kutoa huduma za uzazi. Kulingana na tathmini, vifo vya kina mama vimeongezeka kutoka 409 mwaka 2017 hadi 1053 kati ya mwaka 2020/21.
Vifo vya kina mama vilisababishwa na kuvuja damu kupindukia baada ya kujifungua, maambukizi na shinikizo la juu la damu wakati wa ujauzito.
“Kuvuja damu wakati wa kujifungua ndio sababu kuu ya kina mama kufariki. Na sababu nyingine inayosababisha vifo hivi ni ukosefu wa dawa katika vituo vyetu vya afya hapa Afrika na nchi zinazoendelea,” amesema Michael Mwiti, Mkunga na Mtaalam wa afya ya uzazi katika hospitali ya kaunti ya Makueni nchini Kenya.
Kimsingi, hospitali ya uzazi inapaswa kuwa na wodi ya kusubiri kujifungua, ya kujifungua, wadi ya waliojifungua bila upasuaji, ya waliopasuliwa na ya kina mama waliojifungua na kuanza kunyonyesha.
Wajawazito hutibiwa kwenye vyumba vya kawaida kutokana na uhaba wa vyumba maalumu
Hata hivyo tathmini ya mkaguzi mkuu wa serikali imebaini kuwa hospitali zilizochunguzwa hazina wodi hizo na kina mama hulazimika kulala zaidi ya wawili kwenye kitanda kimoja jambo linaloongeza uwezekano wa kuambukizwa magonjwa.
Hospitali za rufaa za Garissa na Isiolo,kwa mfano, ni miongoni mwa zisizokuwa na vifaa kabisa.
Tathmini imeonyesha hospitali 7 za rufaa hazina sehemu maalumu ya upasuaji inapotokea dharura za uzazi na badala yake wanatumia chumba cha kawaida cha upasuaji hali inayotatiza utoaji huduma na kina mama mara nyingine kufariki.
Chumba cha upasuaji wa wazazi kwenye hospitali ya Uthiru, kwa mfano hakina vifaa na hakitumiki.
Tathmini ya mkaguzi mkuu wa serikali imebaini pia kuwa ni hospitali 29 kati ya zote 67 zilizochunguzwa zenye vitengo maalumu vya watoto wachanga.
Baadhi hazina vitengo kwa ajili ya huduma ya Kangaroo kwa kina mama waliojifungua kabla ya kutimiza muda wao na nyingine hazina vitanda vya kutosha na kwenye baadhi ya hospitali kina mama hulazimika kulala kwenye magodoro yaliyotandikwa sakafuni.
– Ripoti mpya ya mkaguzi mkuu wa serikali Kenya
– Via Dw
– Editor&Reviewer: @afyaclass
– Soma Zaidi pia Kuhusu Chanzo cha Vifo kwa Mama Wajawazito:Soma hapa