#PICHA:Wakunga kisiwani Zanzibar wakifurahia wakati wa maadhimisho ya siku ya wakunga duniani yaliyofanyika mjini Unguja.
Kwa mujibu wa miongozo ya afya, mkunga mmoja anatakiwa kuhudumia mjamzito mmoja, huku muuguzi mmoja akihudumia wajawazito wanne.
Unguja. Licha ya wakunga kuwa watendaji wakuu wa kutoa huduma kwa mama na mtoto kwenye sekta ya afya, wamesema wanakabiliwa na changamoto nyingi, hivyo kushusha morali ya utendaji wao.
Miongoni mwa changamoto hizo ni kushindwa kutambuliwa mchango wao wanapofanya vizuri, bali hupokea lawama wanapokosea kutokana na sababu za kibinadamu kama uchovu unaotokana na kufanya kazi nyingi kupitiliza muda wao wa kazi.
Wamebainisha hayo katika risala iliyosomwa leo Mei 5, 2024 na Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wakunga Zanzibar, Sanura Abdala Salim wakati wa maadhimisho ya siku ya wakunga duniani.
Ametaja changamoto nyingine ni ufinyu wa elimu ya utambuzi, upungufu wa vitendea kazi kama vifaa vya kupimia shinikizo la damu, vipimo vya mkojo, na vifaa vya kisasa vya kumfuatilia mtoto tumboni.
“Wakunga wakiwa ndio watendaji wakuu katika sekta ya afya ya uzazi bado wanakosa kutambuliwa wanapofanya vizuri, lakini hushushiwa lawama katika makosa ambayo mengine ni ya kibinadamu kutokana na uchovu wa kazi nyingi,” amesema.
Amesema changamoto nyingine ni upungufu mkubwa wa wauguzi na wakunga katika maeneo ya kutoa huduma za mama na mtoto ikiwemo wodi za wazazi, akieleza mkunga mmoja anahudumia zaidi ya watu 12.
Kwa mujibu wa miongozo ya afya, mkunga mmoja anatakiwa kuhudumia mjamzito mmoja, huku muuguzi mmoja akihudumia wajawazito wanne.
“Tunaomba viongozi wetu wa Wizara ya Afya kuwaangalia kwa jicho la tofauti na kuwapa motisha wauguzi na wakunga wanaofanya kazi katika wodi za wazazi, kwani wanahudumia idadi kubwa ya kina mama,” amesema.
Hata hivyo, kupitia risala hiyo wameahidi kuyaendeleza mazuri na kuyaboresha kila mwaka ili kutoa huduma bora za afya ya mama na mtoto.
“Pia niwaombe wakunga wenzangu wote kufanya kazi kwa bidii, weledi, heshima, mapenzi, lugha nzuri kwa kina mama, watoto na jamii kwa ujumla,” amesema.
Mkunga mstaafu, Sharifa Hawadh amesema wakunga na wauguzi ni wanasayansi, lakini ili waweze kutenda vyema kazi zao lazima wasome na kujiongezea elimu, ujuzi na maarifa.
Amesema kazi ya ukunga pamoja na uzito wake lakini inahitaji watu wenye upendo na kuwajali wagonjwa.
Mkunga Asha Mkamba amesema kabla ya kufikia kilele cha maadhimisho hayo walifanya shughuli mbalimbali ikiwemo uchunguzi wa lishe na saratani ya kizazi kwa vijana wa umri kati ya mikaa 18 hadi 25 na kubaini kuwapo changamoto.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk Habiba Hassan Juma amesema wizara ina mpango kuona watendaji wanaongezeka, kwani kuna upungufu mkubwa katika vituo vya afya.
Alisema kadri watakavyoruhusiwa na utumishi kuajiri watafanya hivyo ili kufikia uwiano sawa kati ya wauguzi na wagonjwa ili kuimarisha afya ya jamii.
“Tunatakiwa kuwa na subira kwani kazi hii ni nzito na ni ya wito wa kujitolea,” amesema.
Naibu Waziri wa Afya, Hafid Hassan, akisoma risala kwa niaba ya Mariam Mwinyi, mke wa Rais wa Znzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema amepokea changamoto zinazowakabili lakini wasivunjike moyo.
Ameiagiza Wizara ya Afya kuzifanyia kazi na kutatua changamoto hizo kama zilivyojieleza katika risala yao.
Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo katika mikakaki ya kuimarisha afya ya uzazi kwa kuzuia na kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga.
Amesema ili kukamilisha malengo hayo wanahitaji kuwatumia wakunga ambao wana mchango mkubwa wa kufanikisha malengo ya nchi.
Ofisa uzazi salama kitengo shirikishi cha afya ya uzazi na mtoto, Safia Haidhuru Ramadhan amesema takwimu za mwaka 2022 zinaonyesha kulikuwa na vifo vya uzazi 52 ikilinganishwa na vifo 70 vilivyotokea mwaka 2021.
Kwa upande wa vifo vya watoto vilivyotokana na changamoto za uzazi amesema ni 1,727 kiwango ambacho kinaonekana kuwa bado kipo juu.