CHOO KIGUMU
• • • • • •
BAKTERIA NA CHOO KIGUMU
Siyo kila bakteria wanaopatikana kwenye mwili wa binadamu huwa ni wabaya kwa afya,kuna baadhi ya bakteria huwa ni wazuri na binadamu anawahitaji sana siku zote za maisha yake.Mfumo wa chakula wa binadamu huwa umebeba aina nyingi sana za bakteria wazuri wanaosaidia katika zoezi muhimu kabisa la kumeng'enya chakula.Bila uwepo wa bakteria hawa,matumizi sahihi ya vyakula tunavyokula yangekuwa mashakani.
Katika nyakati fulani,bakteria hawa wazuri huuliwa na dawa za viuavijasumu (antibiotics) pamoja na sababu zingine.Inapotokea bakteria hawa wamekufa mwili hauwezi kukimeng'enya chakula kikamilifu ndiyo maana watu wanaotumia dawa hizi za antibiotics husumbuliwa sana pia na tatizo la uwepo wa choo kigumu.Kuna baadhi ya watu pia katika nyakati fulani za maisha hujikuta wanapatwa na tatizo la choo kigumu bila sababu maalumu japokuwa wanakula vizuri hasa matunda pamoja na kunywa maji mengi kila siku.
Kama tatizo hili linakusumbua sana na huelewi chanzo ni nini basi tafuta maziwa mtindi (mgando),kwenye maziwa haya huwa kuna bakteria jamii ya Lactobacillus acidophilus,Lactobacillus bulgaricus au Streptococcus thermophilus.Hawa kwa lugha rahisi huitwa viranja wa mfumo wa mmeng'enyo wa chakula pamoja na mfereji wa uzazi wa wanawake.Kupitia maziwa haya utaurejesha mfumo wako wa chakula katika hali yake ya kawaida hivo kuondoa tatizo lako la choo kigumu,kwa wanawake hutoa pia faida nyingine ya ziada ya kuwakinga dhidi ya maambukizi mbalimbali yanayohusisha uke.
Jamii hii ya maziwa pia huongeza utengenezwaji wa cytotoxic lymphocytes ambazo kwa kiswahili kisicho rasmi sana tunaweza kuziita "seli zinazoua" (killer cells).Seli hizi hufanya kazi ya kuimarisha mfumo wa ulinzi wa mwili hasa katika kuzilinda seli zingine za mwili wako dhidi ya aina mbalimbali za saratani na maambukizi ya virusi.
Cr: @afyainfo
0 Comments
WEKA COMMENT HAPA..!!!