Kila mtu aeleza alivyoguswa na Mtanzania aliyeuawa Israel

Wanafunzi waliokuwa wakisoma Chuo Kikuu cha Sokoine (Sua) pamoja na marehemu Clemence Mtenga (22), ambaye aliuawa nchini Israel, wameelezea namna walivyoishi naye huku wakidai wataukosa upendo na namna alivyojali wengine.

Wametoa simulizi hiyo leo Novemba 28, 2023 nyumbani kwa marehemu Kirwa, wilayani hapa, wakati walipofika kushiriki maziko ya Clemence ambayo yanafanyika leo.

Akizungumza Mwananchi Digital, Anthony Kanyanza mmoja wa wanafunzi hao, amesema kuwa kifo hicho kimewasikitisha na kuwashtua kwa kuwa kilitokea ghafla na kimewapa wakati mgumu kukubali ukweli huo.

“Mimi ni miongoni mwa wanafunzi tuliobahatika kusoma na kukaa na Clemence, kwa kweli taarifa za kifo chake tulizipokea kwa masikitiko makubwa maana zilikuwa za ghafla na za kushtua na muda si mrefu tulikuwa tumewasiliana naye.

“Hatukuweza kuzipokea kwa wepesi na ilikuwa ni ngumu kukubali na kwa kiwango kikubwa mpaka sasa bado kuna ugumu wa kupokea na kuzikubali taarifa za kifo chake, ila ni mipango ya Mungu hatuna budi,”amesema Kanyanza.

Kwa mujibu wa simulizi hiyo, Kanyanza amesema marehemu alikuwa mtu mwenye upendo kwa wenzake na alijijengea utaratibu wa kuwapigia simu rafiki zake kila ilipofika saa moja usiku, kwa lengo la kuwajulia hali.

Ameongeza kuwa, “Aanaweza kukupigia tu akakuuliza vipi umeshindaje, siku yako imeendaje na ni kitu ambacho alikuwa nakifanya mara kwa mara, kila siku alitamani kujua marafiki zake wana hali gani na wanaendeleaje.

Aidha Kanyanza amesema marehemu ukimueleza tatizo lako, si mtu wa kusikiliza na kuacha, alikuwa akikupa moyo na kupiga hatua moja katika kuangalia namna ya kukusaidia, “kwenye masuala ya uongozi alikuwa mfuatiliaji sana.

Amesema pia marehemu alikuwa mwanakwaya, na kwamba alishiriki kikamilifu shughuli za kitaaluma, kidini na kijamii. Kwa upande wake Jovin Shirima ambaye mbali na kuwa mwanafunzi mwenzake hapo Sua, aliimba naye kwaya.

“Kifupi marehemu nimefahamiana naye tangu tunasoma kidato cha tano na sita ambapo marehemu alikuwa kiongozi wa TYCS Umbwe Sekondari, wakati mimi nikiwa kiongozi wa TYCS Lyamungo Sekondari na baadaye tukakutana Sua,” amesema.

Mwili wa Clemence uliwasili nchini jana Novemba 27, 2023, saa 2:51 usiku, kwa ndege ya Shirika la Ndege la Uholanzi (KLM), kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) ambapo ulipokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu aliyekuwa ameongozana na kamati ya usalama mkoa na kuukabidhi kwa familia.

Novemba 17, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ilithibitisha kupokea taarifa za kifo cha Clemence Mtenga, ambaye alikuwa miongoni mwa Watanzania wawili ambao pamoja na raia wa mataifa mengine walikuwa hawajulikani walipo baada ya kuanza kwa vita kati ya Hamas na Israel.

Taarifa hiyo iliyotolewa na kitengo cha mawasiliano ya Serikali cha wizara hiyo, ilieleza Clemence alikuwa miongoni mwa vijana wa Kitanzania 260, waliokwenda Israel kushiriki mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa vitendo, chini ya mpango wa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Israel.

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!