Ticker

6/recent/ticker-posts

Vita vya Urusi na Ukraine: Mke wa mkuu wa Ujasusi wa kijeshi wa Ukraine awekewa sumu



Mke wa mkuu wa upelelezi wa kijeshi wa Ukraine awekewa sumu ya metali nzito na anaendelea na matibabu, serikali ya Kyiv imefichua.

Msemaji wa shirika la ujasusi la kijeshi la Ukraine, au GUR, alisema Marianna Budanova, mke wa Kyrylo Budanov, alikuwa akipokea matibabu hospitalini.

“Ndiyo, naweza kuthibitisha taarifa hizo. Kwa bahati mbaya, ni kweli,” msemaji wa GUR Andriy Yusov aliambia Reuters siku ya Jumanne bila kufafanua ni lini sumu hiyo alipewa au ni nani aliyehusika.

Budanov amekuwa mtu maarufu nchini Ukraine kwa jukumu lake katika kupanga operesheni za siri dhidi ya Urusi, ambayo ilianzisha uvamizi wake kamili dhidi ya Ukraine mnamo Februari 2022.

Yusov alisema mwaka huu kwamba Budanov alinusurika majaribio 10 ya kuuawa na Shirikisho la usalama la Urusi, au FSB.

Bado haijabainika mara moja ni nani aliyehusika na tuhuma za kuwekewa sumu mke wake, lakini Yusov alisema kuwa maafisa wengine wa GUR wamepata dalili za sumu kali zaidi.

Hapo awali Urusi ilishutumiwa kwa kuwapa sumu wapinzani, akiwemo mwanasiasa Alexey Navalny na wahamiaji wawili wa Urusi waliohudhuria mkutano wa kilele mjini Berlin ulioandaliwa na mkosoaji wa Urusi.

Moscow pia imeilaumu Ukraine kwa kushukiwa kuhusika katika mauaji ya mwanablogu wa Urusi anayeunga mkono vita na mwandishi wa habari anayeunga mkono vita katika ardhi ya Urusi, madai ambayo Ukraine inakanusha.

Urusi iliivamia Ukraine mnamo Februari 24, uvamizi wake umesababisha hasara nyingi ikiwemo maisha kwa maelfu ya watu, pamoja na mamilioni ya watu kuyahama makazi yao.



Post a Comment

0 Comments