DCEA kufanya operesheni dhidi ya dawatiba zinazogeuzwa kuwa dawa za kulevya
DCEA kufanya operesheni dhidi ya dawatiba zinazogeuzwa kuwa dawa za kulevya.
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania (DCEA), imetangaza kuanza operesheni dhidi ya matumizi ya dawa tiba zinazogeuzwa kuwa dawa za kulevya.
Kulingana na DCEA, operesheni hiyo itahusisha uchunguzi wa maduka yanayouza dawa hizo kiholela, kwa maana yale yasiyo na vibali vya kufanya biashara hiyo.
Hayo yameelezwa jijini Dar es Salaam leo Desemba 27, 2023 na Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretus Lyimo alipozungumza na waandishi wa habari.
Operesheni hiyo, amesema imechagizwa na kukithiri kwa matumizi ya dawa tiba zinazogeuzwa kuwa dawa za kulevya.
“Kwa sasa tumefanikiwa kukamatwa mtandao mkubwa wa dawa za kulevya, hakuna tena mfanyabiashara mkubwa wa dawa hizi.
“Kwa sababu dawa za kulevya hazipatikani, kumeibuka matumizi ya dawa tiba zinazogeuzwa za kulevya na hili ndilo linalotusumbua sasa,” amesema.
Kutokana na hali hiyo, Lyimo amesema hivi karibuni operesheni dhidi ya maduka yanayouza dawatiba kiholela itaanza na watuhumiwa watakamatwa.
Kilo 3,000 za heroin zakamatwa
Katika mkutano huo, Kamishna huyo amebainisha kukamatwa kwa kilogramu 3,182 za dawa za kulevya aina ya Heroin na Methamphetamine.
Iwapo dawa hizo zingeingizwa mtaani, amesema zaidi ya watu milioni 76.386 wangeathirika kwa siku.
Kwa mujibu wa Lyimo, dawa hizo zilikamatwa katika operesheni iliyofanyika kuanzia Desemba 5 hadi 23, mwaka huu katika Mikoa ya Dar es Salaam na Iringa.
“Watu saba wamekamatwa kuhusika na dawa hizo ambapo wawili wana asili ya Asia,” amesema Lyimo.
Kati ya dawa hizi za kulevya zilizokamatwa katika Wilaya za Ubungo, Kinondoni, Kigamboni kwa Dar es Salaam na Wilaya ya Iringa mkoani Iringa, amesema kilogramu 2,180.29 ni aina ya Methamphetamine na kilogramu 1001.71 ni aina ya Heroin.
Hata hivyo, amesema kiasi cha dawa kilichokamatwa kwenye operesheni hiyo, ndiyo kikubwa zaidi kuwahi kukamatwa tangu kuanza kwa shughuli za udhibiti wa dawa hizo.
“Watuhumiwa waliokamatwa ni miongoni mwa mitandao mikubwa ya wauzaji wa dawa za kulevya inayofuatiliwa nchini na duniani,” amesema.
Aidha, amesema katika mtandao huo, watuhumiwa wengine waliokimbilia nje ya nchi ikiwemo Afrika Kusini wanaendelea kufuatiliwa ili watiwe nguvuni.
“Tumeshawasiliana na nchi mbalimbali kuhakikisha watuhumiwa wote wanakamatwa na wakiwakamata watatujulisha,” amesema.
Ukubwa wa tatizo
Alipotafutwa na Mwananchi Digital kuzungumzia ukubwa wa tatizo la matumizi ya dawatiba kama dawa za kulevya, Mkurugenzi wa Pili Misana Foundation Sober House (inayoshughulika na kuwaponya waathirika wa dawa za kulevya), Pili Missanah amesema changamoto ni kubwa.
Kwa sasa amesema waathirika wa Heroin na Cocaine wamepungua, lakini wanaotumia dawatiba kuzigeuza dawa za kulevya ni wengi zaidi.
“Kwenye Kituo changu kwa siku moja naweza kumpokea mraibu mmoja wa unga, lakini nikapokea wathirika 10 wa dawatiba,” amesema.
Kulingana na Pili, wengi wao wanaanzia kwenye matumizi ya dawa za maumivu na baadaye wanapata uraibu.
“Ni dawa hizi za kupunguza maumivu ndizo hasa zinazowaathiri, mtu anatumia kupitiliza hadi inamjengea uraibu. Anajikuta hawezi kufanya lolote bila kupata hizo dawa,” amesema.
Kwa kiasi kikubwa, amesema hali hiyo inasababishwa na uuzwaji holela wa dawa hizo za kulevya.
Kuhusu mpango wa DCEA, amesema ni sahihi na umekuja wakati muafaka, isipokuwa kuna changamoto ya kuwabaini wanaouza kwa njia haramu na halali, kwa kuwa dawa hizo haziuzwi kwa kibali.
“Kwa uelewa wangu dawa hizi haziuzwi kwa kibali yeyote anauza tu dukani, kumjua anayeuza zikatumike vibaya na vizuri ni vigumu.
“Kikubwa ni kuwaelimisha wananchi, pia wapo madaktari wasio waaminifu, mtu akijisikia vibaya anamchoma sindano ya kupunguza maumivu, kesho akienda anamchoma tena na tena na tena hadi anakuwa mraibu,” amesema.
0 Comments
WEKA COMMENT HAPA..!!!